Connect with us

Kitaifa

Biteko aanza na agizo la siku 90

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ametoa siku 90 kwa vituo vya kulelea watoto na wazee visivyo na usajili vikamilishe kwa mujibu wa sheria na watakaoshindwa wachukuliwe hatua.

 Wakati Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati akitoa maelekezo hayo, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa naye ametoa siku 90 kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa), kubadilika kifikra kwa kujiendesha kama sekta binafsi na kuondoa malalamiko.

Mawazri hao walitoa maagizo hayo jana jijini hapa kwa nyakati tofauti, ambapo Dk Biteko alizungumza alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa maofisa ustawi wa jamii nchini, huku Bashungwa akitoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa wakala hao.

Dk Biteko ambaye alikuwa akimwamwakilisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango. Pia, alitoa maagizo tisa kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima ili kuboresha sekta ya ustawi wa jamii.

Miongoni mwa maagizo hayo ni kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia sera, sheria na miongozo, wamiliki wa makao ya watoto wanaogeuza vitega uchumi kuacha mara moja, waendelee kusuruhisha migogoro, kuwatambua na kuwapatia huduma watoto walio katika mazingira hatarishi.

Mengine ni maofisa ustawi wa jamii kuendelea kutoa elimu ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia, ulinzi na usalama wa watoto kwenye mikusanyiko, kuimarisha kampeni zihusuzo masuala ya ukatili, viongozi wa dini na wazee wa mila kukemea matendo maovu na mwisho wazazi na walezi kuzingatia wajibu wao.

“Waziri mwenye dhamana shirikiana na vyombo vya sheria ili kuwabaini wamiliki hao na kuwachukulia hatua za kisheria, natoa rai kwa watu na taasisi zote zinazotoa huduma za ustawi wa jamii katika vituo visivyosajiliwa kuvisajili haraka na mwisho ni siku 90 kuanzia leo,” alisema Dk Biteko.

Naibu waziri mkuu huyo alisema mmomonyoko wa maadili unasababisha madhara mengi katika jamii ikiwemo ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, migogoro ndani ya familia na ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Kwa upande wa maofisa ustawi wa jamii aliagiza kuwapokea waathirika wa matendo ya ukatili, migogoro ya ndoa na mirathi na wahitaji wote wa huduma za ustawi wa jamii kwa upendo na kuwasikiliza ili kubaini kiini cha matatizo.

Kwa mujibu wa Dk Biteko, changamoto wanazopitia baadhi yao zinasababisha waanze kuathirika na tatizo la afya ya akili, hivyo ni jukumu la maofisa ustawi wa jamii kuwahudumia kwa upendo na kuwaonyesha utu.

“Nakemea tabia ya baadhi ya wanaume ya kutelekeza familia zao na pengine kutowajibika kutunza watoto waliowazaa wenyewe, nawakumbusha wanaume kuwa wana wajibu kuhakikisha familia zao zinakuwa salama na kuzipatia mahitaji ya kila siku ili kuziongoza vema,” alisema Dk Biteko.

Awali, Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima alisema huduma za ustawi hutolewa kwa mtu mmoja, familia, makundi na jamii kwa lengo la kuzuia na kutatua changamoto ili kuboresha ustawi wa mtu kiakili, kimwili, kihisia na kimaadili hasa kwa makundi maalumu ambayo hayana uwezo wa kukidhi mahitaji ya msingi.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la PACT Tanzania na Mkurugenzi wa Mradi wa ACHIEVE, Dk Levina Kikoyo alisema ni msingi wa jamii yenye haki na ustawi wa kuzungumza masuala yahusuyo jamii.

Dk Kikoyo alisema kila jitihada ndogo ina umuhimu wake hivyo kwa pamoja watu wakiamua wanaweza kufanikiwa na mambo yakawa makubwa.

Naye Bashungwa katika maagizo yake alitoa miongozo na kutaka aanze kuona matokeo yake ndani ya miezi mitatu.

“Mwongozo huo ni kuanzia suala la mikakati ya maboresho ya utoaji huduma kwa Watanzania kupitia Tamesa na mkakati huo utakapokuwa tayari tutawaambia Watanzania namna ambayo wakala tunajipanga kuhakikisha tunabadilika,”alisema.

Bashungwa alisema pamoja na kazi nzuri inayofanyika na Tamesa lakini kumekuwa na changamoto kwenye upande wa utengenezaji wa magari ya Serikali na mitambo.

Hata hivyo, alisema kwa namna ambavyo Tamesa ilivyoundwa na dhamira na malengo yake bado ni taasisi muhimu, na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inakuwa bora inayotoa huduma bora pia kwa Watanzania.

“Mbadilike hasa hasa kifikra iwe ya kisekta binafsi na inabidi iwe ya huduma kwa mteja, alisema.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Tamesa, Lazaro Kilahala alisema wamepokea maelekezo ya Serikali ambayo wanatarajia kuona wanakuwa wa kisasa zaidi, kujiendesha kwa ufanisi na tija.

“Tunajielekeza huko na tunauhakika tutakuwa Tamesa ya tofauti…Serikali inataka Tamesa mpya, yenye ufanisi, tija na uadilifu. Tufanye kazi kwa kumjali mteja na thamani ya kile tunachokifanya. Tuyapokee na kuyafanyia kazi,”alisema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi