Kitaifa
Rais Samia: Mabadiliko ya viongozi siyo adhabu
Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri, amesema uamuzi huo umelenga kuimarisha maeneo ya utendaji, mageuzi katika ahadi walizotoa kwa wananchi, huku akisisitiza si adhabu.
Katika mabadiliko hayo, mbali na kumteuwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko, mkuu huyo wa nchi aliteuwa Mawaziri wanne, Naibu Mawaziri watano, Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu wakuu watatu.
Kadhalika, aliwahamisha wizara baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu.
Rais Samia ametaja sababu ya mabadiliko hayo leo Septemba 1, 2023 alipohutubia hafla ya uapisho wa viongozi hao iliyofanyika katika Ikulu ndogo ya Zanzibar.
Amesema mabadiliko aliyofanya yamelenga kurekebisha baadhi ya maeneo kwa shabaha ya maendeleo nchini.
“Kwa wale wapya nadhani mnayaona yanayotokea bungeni na mmekuwa mkipaza sauti kubwa kwa mawaziri sasa yale mliyokuwa mnapazia sauti kayafanyeni ninyi.
“Wanasema ukitaka uhondo wa ngoma, sasa mpo kwenye ngoma tunatarajia mcheze kweli kweli na mlete yale mabadiliko mliyokuwa mkiyashauri,” amesema.
Amesema msingi wa mabadiliko hayo si adhabu bali yanalenga kuimarisha maeneo mbalimbali ya utendaji na anachokitarajia ni jitihada za wateule na utumishi unaostahili.
“Kuna mwingine akipata anasema sasa yule atanijua mimi nani, sisi ni watumishi wa watu,” amesema.
Katika utumishi wa watu, amesema mahusiano ni jambo muhimu na atakayejikweza hataweza kuwatumikia watu.
“Upole si ujinga, upole wakati mwingine ndiyo maarifa unatulia unalitafakari jambo,” amesema.
Hata hivyo, amesema mabadiliko hayo yamelenga kuona mageuzi katika ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi.