Connect with us

Kitaifa

Samia abadilisha mawaziri, makatibu wakuu na manaibu

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu, huku akianzisha nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na kuifuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na badala yake kuunda wizara mpya mbili.

Kwa Tanzania, mamlaka ya Rais inaiunda nafasi hiyo ya Naibu Waziri Mkuu kwa mara ya tatu, wakati mara ya kwanza ikidumu kwa mitatu (1986 – 1989), ambapo Rais wa wakati huo Ali Hassan Mwinyi, alimteua aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya kwanza, Salim Ahmed Salim, kushika wadhifa huo.

Kwa mara ya pili, nafasi hiyo pia iliundwa na Rais Mwinyi, mwaka 1993 kwa kumteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, kushika wadhifa huo, ambao alidumu nao mpaka mwaka 1994 kabla hajajiengua kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Na kuhusu kuvunjwa kwa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Rais Samia ameamua kuunda wizara mbili zinazojitegemea, ambapo sasa kutakuwa na Wizara ya Ujenzi, pamoja na Wizara ya Uchukuzi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na kusambazwa kwa vyombo vya habari leo Jumatano Agosti 30, 2023; Dk Moses Kusiluka amesema kuwa Rais amemteua Dk Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, katika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu, Dk Biteko atakuwa anashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali, kabla ya uteuzi huo, Dk Biteko alikuwa Waziri wa Madini.

Aidha, katika mabadiliko hayo, Rais ameimarisha Wizara ya ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza nafasi ya Naibu Waziri na Katibu Mkuu watakaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Mbali na uteuzi wa Naibu Waziri Mkuu, amemteua Mawaziri wanne, Naibu Mawaziri watano, Makatibu Wakuu watatu, na Naibu Makatibu Wakuu watatu. Vilevile, amewabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu.

Katika mabadiliko hayo, Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akichukuwa nafasi ya Dk Angeline Mabula.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, ameteuliwa kuwa Waziri wa Madini, nafasi iliyokuwa kushikiliwa na Dk Doto Biteko, ambaye katika mabadiliko haya, anakuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Rais pia ameteua aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, kuwa Waziri wa Uchukuzi.

Kwa upande mwingine, mabadiliko hayo pia yamemgusa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa, kwani sasa ameteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Ujenzi, nafasi ambayo hapo awali ilikuwa inashikiliwa na profesa Mbarawa.

Balozi Kusiluka ameendelea kueleza kuwa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, huku Mbunge wa Misungwi, Alexander Mnyeti, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Pia Rais amemteua Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, David Kienzile, kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Judith Kapinga, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati, huku Mbunge wa Mkinga, Danstan Kitamndula, akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, imebainisha kuwa Mawaziri waliohamishwa ni pamoja na Januari Makamba, kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akichukua nafasi ya Stergomena Tax aliyehamishiwa Wizara ya Ulinzi.

Alyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, amehamishiwa Ofisi ya Rais – Tamisemi, huku Angela Kairuki, akitoka Tamisemi kwenda kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Taarifa ya Balozi Kusiluka pia imemtaja aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, ambaye sasa anakuwa Waziri Utamaduni Sanaa na Michezo, akibadilishana na Balozi Dk Pindi Chana.

Kwa upande wa Manaibu Mawaziri, Steven Byabato amehamishwa kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

“Hapa nisisitize, Mheshimiwa Rais ameamua kuimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza Naibu Waziri na Katibu Mkuu. Kwa hiyo katika hii wizara kutakuwa na Makatibu wakuu wawili, mmoja atakayeshughulikia kipekee masuala ya Afrika Mashariki,” amesema Balozi Kusiluka.

Kwa upande wa makatibu wakuu, Balozi Kusiluka amesema aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi.

“Mhandisi Cyprian John Luhemeja aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu atakayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Balozi Profesa Kennedy Gaston ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki,” amesema.

Amemtaja pia Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi aliyekuwa akishughulikia masuala ya Uchukuzi, Dk Ally Possi kuwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi.

Naye Ludovick Nduhile aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi aliyekuwa akizughulikia masuala ya Ujenzi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Mhandisi Mwajuma Waziri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji.

Kwa upande wa makatibu wakuu waliohamishwa, taarifa imemtaja Profesa Jamal Katundu, ikisema amehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu kwenda kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, huku Dk Seif Shekalaghe akihamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, akibadilishana ofisi na Dk John Jingu.

“Uteuzi huu unaanza leo Agosti 30, 2023 na viongozi wote walioteuliwa wataapishwa Septemba 1 Ikulu Ndogo ya Zanzibar saa 5:00,” amesema Balozi Kusiluka.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi