Connect with us

Kitaifa

Bunge lafunga mjadala suala la uwekezaji bandari, latoa mwongozo

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amezuia mjadala wa makata wa bandari kujadiliwa ikiwa tayari Bunge limeishamaliza majukumu yake ya awali, huku akisema linaweza kujadiliwa endapo litaletwa katika utaratibu mwingine wa kibunge.

Spika Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 29, 2023, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu ya wabunge ambapo amesema kuwa Bunge lilishamaliza mjadala huo hivyo wabunge wanatakiwa kuendelea kuwasikiliza wananchi.

Katika mkutano wa 11 wabunge walipitisha makubaliano ya mpango wa Serikali katika kuingia makubaliano na DP World katika kuendesha bandari, ambapo kumekuwa na mjadala mrefu ukihusisha wanasiasa, wanasheria, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla.

Huku Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kutumia mamlaka aliyo nayo na hivyo kusitishe wasilisho la ridhio la mkataba wa bandari, huku pia wakitaka hatua kama hizo zichukuliwe Bunge kwa kufuta ridhio lao.

Hivyo, Spika Tulia amesema katika kipindi ambacho wabunge walikuwa majimboni, wamewasikiliza watu wengi na kupokea mambo mengi ambayo yamezungumzwa kwa mawanda mapana hivyo wanapaswa kuyachukua na utakapofika wakati watayatumia kwa ajili ya kuishauri Serikali.

“Kuhusu suala la bandari tuendelee kuwasikiliza wananchi kwani sisi Bunge tulishamaliza kwa sehemu yetu, na kwa kuwa Bunge lilishafanya maamuzi yake basi wakati wetu ni pale tutakapohitaji mikataba iletwe bungeni ili tuipitie,” amesema Dk Tulia.

Kiongozi huyo wa mhimili huo wa Bunge amesema kuwa wataendelea kuishauri na kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi hivyo Watanzania wasiwe na hofu katika jambo hilo.

Kwa Mujibu wa Dk Tulia, watatumia hoja na maoni ya wananchi katika kuishauri Serikali utakapofika wakati huo lakini watatumia maoni na ushauri wa wananchi kwani kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali kwa maslahi ya wananchi.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi