Connect with us

Kitaifa

Fumbo Dola za mauzo ya nje hazionekani

Kwa miezi kadhaa sasa nchi nyingi duniani zimekumbana na changamoto ya uhaba wa Dola za Marekani na kuongezeka kwa thamani ya sarafu hiyo dhidi sarafu zake.

Sababu kubwa zinazotajwa kusababisha changamoto hiyo ni vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine, kufufuka kwa shughuli za kiuchumi baada ya mlipuko wa Uviko-19, Sera ya Marekani ya kupambana na mfumuko wa bei na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

Hali imekuwa mbaya katika mataifa mengi, hususan ya Afrika ambayo yana utegemezi mkubwa wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kuwa sarafu hiyo ya Marekani inahusika kwa asilimia 85 katika miamala yote ya kimataifa.

Tanzania nayo imelipata joto la uhaba wa Dola, lakini ikilinganishwa na mataifa mengine, yenyewe ina unafuu kwani manunuzi ya nje hayajasimama licha ya kutatizwa na ongezeka la bei, litokanalo na kuimarika kwa Dola dhidi ya Shilingi.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) juzi ilieleza matumaini ya kuimarika zaidi kwa hali ya mambo, ikisema akiba ya fedha za kigeni hadi siku hiyo ilikuwa Dola za Marekani 5.41 bilioni ambayo inatosha kuagiza bidhaa za nje kwa miezi minne na siku 27.

Mkurugenzi wa masoko ya fedha wa BoT, Alexander Nwinamila alitoa mchanganuo wa akiba hiyo akisema asilimia 77 ni Dola za Marekani, asilimia 16 Yuani ya China, asilimia 4.78 Pauni ya Uingereza na asilimia 1.72 Dola ya Australia.

Swali linalowasumbua wengi ni kuwa licha ya sababu za kuadimika kwa Dola za Marekani, ni jambo la dunia nzima, fumbo ni kwa nini Tanzania ipate athari kwa kiwango kilichoshuhudiwa wakati ina vyanzo vingi vya fedha za kigeni?

Vyanzo vya Dola kwa Tanzania ni pamoja na uuzaji wa madini, shughuli za utalii, uchukuzi kupitia bandari, mauzo ya bidhaa za viwandani na mazao na vinginevyo na mara kadhaa mamlaka zimesikika zikielezea mwenendo mzuri wa sekta hizo.

Agosti 16, Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko alisema ni aibu kwa wizara hiyo kutoisaidia Serikali kupata fedha za kigeni wakati inaongoza kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.

Waziri huyo alisema katika kipindi cha mwaka jana, Tanzania iliuza nje madini kwa thamani ya Dola 952.9 milioni, lakini utafiti unaonyesha kiasi kilichoingizwa nchini ni kidogo ukilinganisha na mauzo yenyewe wakati sheria inataka wauzaji kuingiza fedha za kigeni na kuzibadilishia nchini.

Alisema kuna wajanja wachache wanaofanya kazi ya udalali wa madini na hao ndio wanaumiza Taifa kwa kutoingiza fedha za kigeni.

Waziri Biteko alisema hataki kuonyeshana ubabe na wauza madini, lakini akiamua kufanya hivyo hakuna kinachoshindikana, bali anatamani kumalizana kwa majadiliano.

Katika kukabiliana na hilo, Dk Biteko alieleza kuwa, wizara hiyo imewapunguza mawakala wa uuzaji wa madini kutoka 700 hadi 150 baada ya kubaini wengi wao ni wadanganyifu.

Katika mkutano wa Biteko na wauzaji wa madini, Katibu wa wafanyabiashara ya madini, Leopold Kimaro alisema bado kuna mianya mingi ya utoroshaji wa fedha za madini, ikiwemo kutowafuatilia wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kujua namna wanavyoendesha biashara zao.

Alieleza kuwa baadhi ya watu hukata leseni zaidi ya moja katika madini ya aina moja, hata kama hawana mtaji na kuzungumza na watu kutoka nje, wakifika wanashirikiana nao kufanya biashara bila kufuata utaratibu uliowekwa.

Aliomba watu wa uhamiaji na maeneo ya viwanja vya ndege kuwa macho, akisema watu wanakuja nchini na fedha nyingi kwa madai ya kununua madini, lakini wakitaka kuondoka hawana fedha wala madini na hawasemi fedha walizoingia nazo zimekwenda wapi.

Mfanyabiashara Salma Kundi, miongoni mwa wafanyabiashara wanaosafirisha nje madini ya vito kwa zaidi ya miaka 10 kwenda mataifa mbalimbali, anasema changamoto inayosababisha mazingira hayo ni kukosekana ulazima wa kuwa na akaunti inayopokea miamala ya malipo kwa thamani ya dola.

“Si kila mfanyabiashara anasafiri kwenda nje kuuza, wengi wanasafirisha hiyo mizigo, ikifika sokoni anafanyiwa malipo kwenye akaunti yake ambayo lazima iwe Tanzania, lakini hailazimishi malipo hayo yaingie kwa Dola au shilingi, sasa sijui huenda eneo hilo Serikali imeliona,” anasema Salma.

Vilevile Salma anasema changamoto nyingine ni ushirikiano wa kibiashara kati ya Mtanzania na mfanyabiashara wa kigeni waliopo kwenye migodi mingi nchini. Kwa sababu ya changamoto ya kukosa mikopo ili kukuza mitaji, wazawa wengi wanaungana na wageni kimitaji ili kufanya biashara,” anasema.

“Kwa hiyo wanapokwenda kuuza nje, sina hakika kama wageni wanalazimika kuwa na akaunti nchini. Ndiyo maana tunashauri wawezeshwe kimitaji ili wakiuza wabanwe warejeshe dola nchini,” anasema Salma, ambaye pia ni katibu mkuu wa Chama cha Wanawake wachimba Madini Tanzania (Tawoma).

Hata hivyo, suala la mauzo ya nje kutochangia katika kapu la fedha za kigeni linaonekana si tu kwa wauzaji wa madini au katika sekta hiyo pekee, bali pia katika maeneo mengi na ili kulishughulikia, BoT imewataka wauzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kuweka fedha zao katika akaunti za ndani.

Uchunguzi mdogo uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanachepusha malipo yao na mchezo huo hufanywa zaidi na wanunuzi wa kigeni.

“Akija Mchina au Mhindi raia mwenzake anayefanya biashara au kazi nchini, anamwambia ampe shilingi afanye manunuzi kisha atamlipa kwa fedha ya nyumbani kwao kupitia akaunti za nchi yao na kwa wazawa hivyo hivyo katika mataifa mengine,” kilieleza chanzo cha taarifa.

Kuondokana na hilo, Mkurugenzi Utafiti wa kiuchumi na Sera wa BoT, Dk Suleiman Misango anaweka msisitizo kuwa fedha zitokanazo na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ziwekwe katika mabenki yaliyopo nchini.

“Fedha hizo zinatakiwa ziwekwe katika mabenki ndani ya siku 90 tangu siku ya kusafirishwa. Hii ni kwa mujibu wa kanuni na. 7(4) ya fedha za kigeni 2022. Lengo ni kuongeza ukwasi wa fedha za kigeni nchini,” alisema Dk Misango.

Aliongeza kuwa hata wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje wafanye malipo kwa kutumia mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini, kwa mujibu wa kanuni 13 (1) ya fedha za kigeni.

“Lengo ni kupata takwimu sahihi za uagizaji wa bidhaa ili kujua mahitaji ya fedha za kigeni. Aidha, taarifa hizi zinasaidia wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato kupata taarifa sahihi za malipo ya kodi husika,” alisema Dk Misango.

Meneja wa biashara za uchumi wa kimataifa na sekta ya bidhaa, Villela Waana anasema kwa masilahi mapana ya Taifa wauzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi wanapaswa kuweka malipo yao katika benki za ndani na kama wote wangekuwa wanafanya hivyo, suala la changamoto ya uhaba wa Dola za Marekani lisingekuwepo.

“Mfano, hadi Juni mzigo uliopita kama bidhaa kwenda nje una thamani ya Dola 7 bilioni, hivyo tunatarajia kuwe na fedha zenye thamani hiyo nchini baada ya hayo mauzo, lakini hazionekani. Kama zingekuwa zinarudi tusingekuwa tuna tatizo hili, maana hizo tu ni zaidi ya akiba yetu ya fedha za kigeni, hata ingekuwa nusu yake tu tungekuwa mbali sana,” alisema Waana.

Akichangia hilo, Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema hali ya mauzo ya nje thamani yake kutorekodiwa yote katika soko la fedha la ndani ni ishara ya kuwepo biashara ya magendo ambayo ina athari za moja kwa moja katika uchumi.

Hata hivyo, kwa upande wa sekta ya madini, alisema kuna uwezekano mkubwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wa ndani wakawa wanawezeshwa kimtaji na wale wa nje, hivyo mauzo yanaenda kwa wenye mtaji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya NBS, takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la nakisi katika urari wa biashara kutoka Sh8 trilioni mwaka 2018 hadi kufikia ongezeko la Sh20.6 trilioni mwaka jana.

Hata hivyo, takwimu za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade) zinaonyesha ongezeko la naksi katika urari inayofikia Dola 8.82 bilioni, huku ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ikionyesha nakisi ya Dola 4.7 bilioni.

Chanzo cha takwimu cha BoT ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na inatumia vigezo vya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

Ili kupunguza nakisi katika urari wa biashara Katibu Mkuu wa Chama cha Wadau wa Ngozi Tanzania (LAT) Fred Kabala pengo hilo linaweza kupunguzwa kwa kuongeza thamani katika bidhaa, kuzingatia ubora wa viwango vya kimataifa ikiwamo vifungashio na uwekezaji wa matangazo ya bidhaa za ndani.

“Lakini pia tulime bila kutumia viuatilifu kwa sababu ni changamoto kwa wakulima wengi, tuwe na mkakati kabambe wa matangazo na watu mashuhuri duniani au vikundi, tuanzishe kanzi data ya mahitaji ya soko ya kimataifa na kulinda bidhaa kwa kutumia nembo maalumu,” anasema Kabala.

“Kuna baadhi ya nchi hutumia maparachichi yetu, na inaonekana wao ndiyo wazalishaji kumbe sivyo. Sababu ni kutokuwa na nembo ya utambulisho wa bidhaa za Tanzania, Tanzanite tunajua lakini chai, korosho, karafuu, kahawa ni nzuri zinatofautiana ubora na ladha”

Kuhusu mbinu kuchangamkia fursa hizo za nje, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, John Ulanga anasema kwanza ni kuendelea kushirikiana na balozi za Tanzania huko nje, kushirikiana na vyama na taasisi zinazolingana na TPFS katika nchi hizo mbalimbali ili kuzitambua fursa pamoja na kushughulikia ubora.

“Kuna kampuni kubwa zilizopata vyeti vya ubora wa Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Viwango (ISO) , hawa tayari wana uwezo katika ushindani , yale ambayo bado hayafikii uwezo huo, waulizwe namna gani wasaidiwe ili kufikia viwango vya juu,” anasema Ulanga.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi