Connect with us

Kitaifa

TMA yatoa tahadhari ongezeko la mvua kubwa za vuli Oktoba hadi Disemba

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kutokana na tahadhari ya uwepo wa El-Nino nchini, mvua kubwa zinatarajiwa kuonyesha katika msimu wa vuli mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu.

Tahadhari ya uwepo wa El-Nino, inatokana mabadiliko ya tabianchi ambapo hali ya joto la bahari la juu ya wastani, inaendelea kuongezeka katika eneo la kati la kitropiki la Bahari ya Pasifiki.

Utabiri huo wa TMA wa mvua za vuli, unatarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na ukanda wa Ziwa Victoria, pamoja maeneo ya machache ya Mashariki mwa Ziwa Victoria ambazo zitakuwa na vipindi hivyo vya mvua.

 Akieleza hayo mbele ya waandishi wa habari leo Agosti 24 Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli 2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Ladislaus Chang’a, amesema mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023.

“Mvua zitaanza maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa maeneo mengine Oktoba, kwa kawaida mvua hizi huisha Disemba na mvua nje ya msimu zitaendelea Januari 2024,” amesema.

Mikoa ya ukanda wa Ziwa Victoria ambako kunaelezwa kutakuwa na mvua hizo, ni pamoja na Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Pia Dk Chang’a amesema ukanda wa Pwani Kaskazini utajumuisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam, Unguja na Pemba pamoja na  Tanga ambapo mikoa yote inatarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani.

Ametaja kuwa Nyanda za juu Kaskazini Mashariki zinahusisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro ambapo inatarajiwa kupata mvua wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Oktoba na kutamatika wiki ya pili ya Januari 2024.

Kufuatia utabiri huo, Dk Chang’a ametoa tahathari kwa wakulima kutokana na uwepo wa unyevunyevu unaotarajiwa kuathiri ukuaji wa mazao.

Hivyo basi, wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda na kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati kutokana na magonjwa kama vile ukungu ambao huathiri mazao.

“Pia kwa wafugaji tunawashauri kutunza malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadae,” amesema.

Kuhusu usafiri na usafirishaji, Dk Chang’a amesema kutokana na utabiri huo miundombinu ya usafiri inaweza kuathirika kutokana na na hali ya hewa hivyo wadau wa sekta hiyo wanatakiwa kuchukua hatua stahiki na kukagua mara kwa mara miundombinu hiyo.

Eneo afya, Dk Chang’a amesema kutatokea magonjwa ya mlipuko kutokana na uharibifu wa miundombinu ya maji taka unaosababishwa na maji kutuama na kutiririka hivyo wananchi wanapaswa kutibu maji ya kuyatumia.

Ufafanuzi zaidi El-Nino

Dk Chang’a amesema El Nino inapotokea huambatana na hatari katika maeneo yote duniani.

“Kwa upande wa Afrika Mashariki hali hii huambatana na ongezeko la mvua japo si mara zote na hii ni kwasababu inategemeana na mifumo ya hali ya hewa katika bahari ya hindi na sehemu nyingine,” amesema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi