Connect with us

Kitaifa

Dola kuongeza deni la Taifa kwa karibu Sh2 trilioni

Dar es Salaam. Tanzania huenda ikatumia gharama kubwa kugharimia deni la Taifa, ikiwa ni miongoni mwa athari zinazosababishwa na kuongezeka kwa thamani ya Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi.

Hali hiyo ina athari hasi katika uchumi wa nchi kwa sababu hivi sasa inahitajika shilingi nyingi zaidi ili kupata Dola ya Marekani.

Mpaka jana Agosti 21, 2023, wastani wa kiwango cha ubadilishaji wa dola kilikuwa Sh2,439.67 kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku bei kwa baadhi ya maduka ya fedha, kiwango cha ubadilishaji kikiwa kikubwa zaidi hadi kufikia Sh2,550.

Kitaalamu, ongezeko lolote la kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni kinaongeza mzigo wa kulipa kwa Serikali, kwani deni la nje kwa sehemu kubwa lipo katika sarafu ya Dola, hivyo zinahitajika dola nyingi kuendelea kulihudumia.

Hadi mwisho wa Juni 2023, deni la Taifa lilifikia takriban dola 42.44 bilioni (Sh103.5 trilioni). Asilimia 70.7 ya deni hilo sawa na dola 30.01 bilioni ni deni la nje.

Ripoti ya tathmini ya uchumi ya kila mwezi ya Benki Kuu kwa Julai, ilibainisha kuwa muundo wa deni la nje kwa kiasi kikubwa lipo katika Dola ya Marekani, ikiwa ni asilimia 66.9 sawa na dola18.27 bilioni.

Kwa kuzingatia kiwango cha ubadilishaji cha Sh2,334.3 kwa Juni, deni la Dola lilikuwa na thamani ya Sh42.67 trilioni.

Hata hivyo, kutokana na thamani ya dola kuongezeka hadi Sh2,439.67 hadi kufikia jana, deni hilohilo sasa lina thamani ya Sh44.5 trilioni na kusababisha nyongeza ya Sh1.83 trilioni.

Mchanganuo wa deni la Taifa unaonyesha karibu nusu ya deni lote la nje linadaiwa na taasisi za kimataifa, ikifuatiwa na wadau wa kibiashara, huku fedha nyingi zikitumika kufadhili miradi na shughuli za miundombinu ya usafirishaji, mawasiliano, ustawi wa jamii, elimu, nishati na madini.

Kauli za wataalamu

Wakizungumzia jambo hilo jana, wataalamu wa masuala ya fedha, walisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kulinda uchumi dhidi ya kushuka kwa thamani ya fedha.

Mkuu wa Utafiti wa Chuo cha Uhasibu (TIA), Dk Gorah Abdallah, alisema uimarishaji wa viwanda vya ndani, kuhamasisha uwekezaji kutoka nje na kuongeza mauzo ya nje, kunaweza kusaidia kuleta utulivu wa kiwango cha ubadilishaji kwa muda mrefu.

Alisema kutokana na uwezo mdogo wa uzalishaji, nchi imekuwa ikiingia gharama kubwa kwa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, hivyo kusababisha uhitaji mkubwa wa fedha za kigeni kuliko zinazopatikana kwenye mzunguko.

“Ni dhahiri kwamba unapokuwa na mahitaji makubwa kuliko usambazaji wa fedha hizi, bila shaka utahisi uhaba. Ufumbuzi endelevu ni kuongeza uzalishaji wa ndani ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje,” alisema.

Aliongeza: “Nchi yetu bado haijitegemei, lakini tunamiliki rasilimali kama vile mazao ya kilimo. Kwa kuongeza tija katika sekta kama kilimo, tunaweza kuuza zaidi na kuzalisha fedha za kigeni.”

Takwimu za BoT zinaonyesha wakati mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yalifikia Dola12.76 bilioni mwaka unaoishia Juni 2023, uagizaji ulikuwa Dola 17 bilioni.

Mhadhiri Msaidizi na Mshauri wa Biashara katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Godsaviour Christopher alisema changamoto ya dola pia ina kuwa fursa kwa Tanzania kuvutia uwekezaji wanje.

Alisema kuna wawekezaji ambao wanaweza kushindwa kuwekeza Marekani kutokana na gharama kuwa juu hivyo kukimbilia nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi