Kitaifa
Maswali Sita kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
Na Shemasi George Rugambwa
Seminari ya Ntungamo, Bukoba.
Leo TEC imetoa tamko lake kuhusu mkataba wa kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam kati ya Tanzania na Dubai. Tamko lake limeelezewa kwa ufupi kupitia Katibu wake Padri Charles Kitima na baadaye likasambazwa kama nyaraka kwa wanahabari.
Kiufupi TEC wanasema maaskofu wakatoliki wanapinga mkataba huo wa Tanzania na Dubai na wanataka sauti ya wengi isikilizwe wakiwa na maana asilimia kubwa ya Watanzania wanaungana na kauli hiyo ya TEC.
Baado naamini ufafanuzi wa Padri Kitima unaweza kuwa na maneno yake binafsi ya ziada kwani alijipambanua awali kuwa na maslahi na jambo hili. Nitaandika zaidi ziku zijazo lakini maswali yangu kwa TEC kwa sasa ni haya ..
1. TEC inafahamu kwamba mwaka 1992 wakati Serikali inapitisha mfumo wa vyama vingi ulikuwa umekataliwa na asilimia 77 ya Watanzania? Hata hivyo serikali ikaamua uruhusiwe. Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.
2. TEC inafahamu kwamba mwaka 2001 baada ya matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar na mauaji ya wafuasi wa CUF mwezi Januari, asilimia kubwa ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla walitaka kuwepo na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na SMZ na SMT chini ya Mkapa haikutaka? Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.
3. TEC inafahamu kwamba mwaka 2014 maaskofu wote Katoliki Tanzania akiwemo Kardinali Pengo na wasaidizi wake walipokea mamilioni ya shilingi pesa taslimu na nyingine kwenye akaunti zao kama Askofu Nzigilwa (milioni 80 benki) na Kilaini (milioni 40 benki). Inajua fedha hizo zilitoka katika kampuni yenye makando kando ya rushwa ya kihistoria Tanzania. Wananchi wengi walipiga kelele lakini fedha hizo hazikurudi wala hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.
4. Padri Kitima anasema kwa zaidi ya miaka 60 ama toka tupate uhuru bandari yetu haijawahi kuendeshwa na wageni. Hii ni kauli yake au ya maaskofu wa TEC? Ni kweli TEC haifahamu kwamba kwa zaidi ya miaka 22 Bandari yetu ya Dar imekuwa chini ya kampuni ya TICTS ikiendeshwa kwa ubia na kampuni toka Hong Kong (Hutchsons?). Kama wanafahamu, wanakumbuka wabia wazawa wa kampuni hiyo wanahusika kwenye kuwapa hela maaskofu kama Rugemalira na IPTL yake walivyofanya? Hili wamewahi kuwaambia waumini wao katika mimbari za ibada?
5. TEC wanafahamu kwamba mwaka 1998 kwenye mauaji pale Mwembechai walikufa wasio na hatia na ilikuwa rai ya mamilioni ya Watanzania kutaka kuwepo na suluhu ya kisiasa? Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.
6. Padri Kitima anasema wananchi wamelikataa Bunge? Ametumia kipimo gani cha Kikatiba? Maana wananchi wanalikataa Bunge kwa kutowachagua Wabunge kwenye Uchaguzi. Hii “Vox Populi Vox Dei” ya TEC imetumia kigezo gani? Wananchi wakikataa Bunge pia si wameikataa Serikali? TEC inaomba vipi busara ya Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo huo inasema serikali yake imekataliwa? Kuna kuchanganyikiwa na haraka kubwa kwenye tamko la TEC hata namna lilivyochapwa na kupangiliwa. Inanipa mashaka kwamba chombo hiki muhimu cha Kanisa kimekubali kutumika kwa maslahi binafsi bila tafakari ya kutosha.
Je hii “Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu” ni wengi wapi hasa? Na mungu anayetajwa hapa ni nani? Usikute mungu anayetajwa na kusemwa asikilizwe ni mungu au miungu watu waliokuwa wanaingiza miamala kwenye akaunti za baadhi ya maaskofu wetu na viongozi wengine wa dini miaka nenda rudi. Tujihadhari. Tusiigawa nchi kupitia madhabahu.
Mathayo 23:13
Ole wenu Mafarisayo wanafiki…