Kitaifa
Rais Samia apangua vituo vya mabalozi, Kairuki apelekwa Uingereza
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewapangia vituo vya kazi mabalozi watatu na kumbadilishia kituo cha kazi Balozi Mbelwa Kairuki aliyekuwa China ambaye sasa anakwenda Uingereza akichukua nafasi ya Dk Asha-rose Migiro aliyemaliza mkataba wake.
Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu usiku wa kuamkia leo Alhamisi Agosti 17, 2023 ikiwa ni saa chache tangu Rais Samia awaapishe mabalozi wapya huku akizungumzia suala la utendaji usioridhisha wa baadhi ya wanadiplomasia hao.
Katika mabadiliko hayo, waliopangiwa vituo vya kazi ni pamoja na Balozi Khamis Mussa Omar anayekwenda China akichukua nafasi ya Kairuki ambaye amehamishiwa London, Uingereza.
Rais Samia amempangia kituo cha kazi Balozi Ceaser Waitara kwenda Namibia akichukua nafasi ya Dk Modestus Kipilimba ambaye amestaafu.
Mwingine ni Balozi Bernard Kibesse aliyepangiwa kuiwakilisha Tanzania nchini Kenya, akichukua nafasi ya Balozi John Simbachawene ambaye amehamishiwa Kampala, Uganda.