Connect with us

Makala

Takukuru kuelimisha wanahabari kuhusu rushwa ya ngono

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema iko tayari kutoa elimu kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo katika mapambano dhidi ya rushwa ya ngono sehemu za kazi.

Takukuru imekuwa ikitoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali katika jamii hasa yale yanayobainika kuwa katika mazingira yanayoshawishi vitendo hivyo kuchukua nafasi na kuathiri maisha yaw engine.

Mwaka 2021, ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Wanahabari Wanawake Afrika (WIN) ilibaini kuwa, unyanyapaa, kuhukumiwa kabla ya kujitetea, hofu na aibu ndicho chanzo cha wanahabari wengi kuogopa kuripoti matukio ya unyanyasaji wa kijinsia wanayofanyiwa.

Si WIN pekee waliofanya utafiti huu, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) nao walifanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 52 ya wanahabari wanaogopa kutoa taarifa za matukio ya unyanyasaji wa kingono kutokana na hofu na unyanyapaa zaidi.

Katika utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwaka 2018, ulionyesha kuwa rushwa ya ngono kazini na vyuoni bado ni changamoto kubwa, ikiwamo upande wa wanahabari wa kike.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani amesema wamekuwa wakifanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu masuala ya rushwa katika namna tofauti ikiwemo rushwa ya ngono.

“Tualikeni tuje kuelimisha, hiyo ndiyo kazi yetu. Tunahimiza mwenye malalamiko atoe taarifa Takukuru,” amesema Kapwani wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu rushwa ya ngono kwa wanahabari.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe amesema rushwa ya ngono ni janga katika taasisi mbalimbali ikiwemo katika vyombo vya habari ambavyo sasa vimeanza kuzungumzia changamoto hiyo.

Amesema tatizo la rushwa lipo katika vyumba vya habari na kwamba linatofautiana ukubwa wake kati ya chombo cha habari kimoja na kingine, pengine tatizo hilo ni kubwa sehemu moja lakini sehemu nyingine halipo kabisa.

“Tamwa tuliwahi kufanya utafiti ikaonekana kuna hilo tatizo lakini sasa hivi, Tamwa inaendelea kufanya huo utafiti. Changamoto bado ipo, kwa bahati mbaya mambo haya hayazungumzwi, vyombo vingi vya habari havina sera ya jinsia, kama ipo utekelezaji wake ni hafifu,” amesema.

Ameongeza kwamba wanawake wako kwenye hatari kubwa lakini wanaume nao hawako salama katika jambo hili kwa kuwa nao wanakumbana na rushwa ya ngono. Amesema wataendelea kupigia kelele jambo hilo.

Mwandishi wa habari wa kujitegemea, Anold Kambi amesema hajawahi kushuhudia moja kwa moja rushwa ya ngono lakini kwa mazingira ya kazi kwa wanahabari wanawake wako hatarini kwa sababu wengi wao wanaona wasipofanya hivyo watapoteza kazi.

“Takukuru itoe elimu kwa wanahabari ili kuwawezesha kutambua kwamba rushwa ya ngono nayo ni rushwa kama nyingine. Pia, waelimishwe kutoa taarifa kwenye mamlaka husika,” amesema Kambi

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi