Kitaifa
Samia ampa ‘zigo’ Waziri Mkuu
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amemwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anakuwa na namba moja ya utambulisho inayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
Rais Samia ametoa wito huo leo Alhamisi Agosti 10, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizindua huduma mpya ya intaneti ya 5G iliyoanzishwa na kampuni ya simu ya Airtel Tanzania pamoja na uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa baharini.
Vilevile, Rais Samia ameelekeza kwamba taarifa za Mtanzania zianze kuchukuliwa baada ya mtoto kuzaliwa na apewe namba yake ambayo ataitumia katika kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo ikiwa imepita wiki moja tangu Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliposhauri kuongeza wigo wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa kuanzia mtoto anapozaliwa ili Watanzania wajumuishwe kwenye huduma rasmi za kifedha.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Samia alisema wizara na taasisi zote zinazotoa huduma kama vile Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, zikatumie namba moja ya Mtanzania (utambulisho wa kitaifa).
“Anapoambiwa Samia ni namba 20, basi taarifa zangu zote, taasisi zote zikivuta namba 20, awe ni Samia Suluhu mmoja yule yule, taarifa zile zile kwa sababu sasa hivi naweza nikawa namba 20 Nida lakini nikienda benki kuna taarifa zingine, nikienda afya ninakotibiwa, taarifa nyingine, shule nilikosajiliwa taarifa zingine,” amesema na kuongeza;
“Hii inafanya hata usalama ndani ya nchi unakuwa na wasiwasi kidogo, unataka kujuana nani ni nani, mwenyeji wa Tanzania ajulikane ni mwenyeji wa Tanzania, mgeni aliyepo tumjue huyu ni mgeni aliyepo.”
Rais Samia alieleza kwamba hiyo itasaidia hata kupunguza usumbufu kwa wananchi wanapokwenda kupata huduma, wakiambiwa wapeleke taarifa lukuki kutoka kwenye Taasisi tofauti au barua ya Serikali ya mtaa anapoishi.
“Kwa hiyo nikitumia namba moja inayonitambulisha Samia Suluhu, kila taasisi ikifungua ni namba ileile, ni Samia yuleyule. Hii itatupunguzia ninapokwenda kutaka huduma, kuambiwa lete hiki, lete hiki, lete barua ya mtendaji,” amesisitiza.
Rais Samia alimtaka kila Mtanzania ahakikishe taarifa zote alizozitoa Nida ni sahihi, kama haziko sahihi aende akarekebishe ili atambulike kwa taarifa hizo alizozitoa na hapo wataweza kujua nani ni nani ndani ya nchi.
“Kwa hiyo nitoe wito huo kwa taasisi zote zinazotoa huduma kwa Watanzania kutumia namba moja ya Nida, na hii itarahisisha huduma…kwamba akizaliwa leo (mtoto), akipewa tu kile cheti na hospitali, kwamba Mtanzania kazaliwa, wa kike au wa kiume, ameingizwa kwenye mtandao, automatically (moja kwa moja) apate namba yake na taarifa zake tuanze kuzikusanya kuanzia siku ile kuzaliwa,” amesema Rais Samia.
Kwa upande mwingine, Rais Samia, pia alimwelekeza Waziri Mkuu Majaliwa, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha Taasisi za Serikali zinaunganishwa na mawasiliano ya mtandao.
“Serikalini kwetu bado hatujajipanga vizuri, matumizi ya mtandao huu bado hatujayatumia vizuri, naomba tujipange tufanye tathmini, tunahitaji kiasi gani kuziunganisha wizara na taasisi za Serikali kutumia mitandao
Rais Samia aliongeza kuwa: “Lazima tuelekee huko, hatuwezi kuimba kwenye majukwaa ‘uchumi wa kidigitali’, maofisini kwetu bado tuna hizo traditional methods (njia za kizamani) za kufanya kazi, haiwezekani.”
Awali, Rais Samia alizungumza na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa njia ya mtandao akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupita mazungumzo hayo, Kikwete alimpongeza kwa hatua hiyo ambayo itachochea mafunzo kwa wanafunzi chuoni hapo.