Connect with us

Kitaifa

Dk Mpango aweka mkazo utoaji Nida

Dar es Salaam. Ili kuhakikisha Watanzania wanajumuishwa katika huduma rasmi za kifedha, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza msisitizo uwekwe katika maeneo matano muhimu, ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa kuanzia mtoto anapozaliwa.

Dk Mpango alizungumza hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mpango wa tatu wa Taifa wa huduma jumuishi za kifedha, utakaotekelezwa kati ya mwaka 2023 – 2028 ukilenga kuongeza matumizi ya huduma rasmi za fedha nchini.

Huduma jumuishi za kifedha zinazosimamiwa katika mpango huo, zipo katika maeneo sita ambayo ni benki, maduka ya kubadilishia fedha, taasisi ndogo za fedha, masoko ya mitaji, bima na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Utekelezaji wa mpango huo utahusisha makundi ya watu yaliyoachwa nyuma katika kupata fursa ya kufikiwa na watoa huduma au kutumia huduma za kifedha, makundi hayo ni wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu, wakulima wadogo, wavuvi na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dk Mpango (pichani), alisema huduma jumuishi za kifedha ni jambo linalotakiwa kupewa umuhimu mkubwa na kuhakikisha hakuna mtu anayebaki nyuma huku akitaka msisitizo kuwekwa kwenye teknolojia.

“Kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, nafikiri tunahitaji kuhakikisha watu wote wanakuwa na vitambulisho vya Taifa na kuongeza mawanda ya utoaji wa vitambulisho vya taifa kuanzia mtoto anapozaliwa.

“Ninaamini, hii itasaidia kutanua upatikanaji wa huduma rasmi za fedha kwa vijana wakiwemo wale walio na umri chini ya miaka 18,” alisema Dk Mpango katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi.

Alisema ni muhimu kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwenye mpango wa huduma jumuishi za kifedha wa mwaka 2023 yanafikiwa ifikapo mwaka 2028 ili kila mwananchi afikiwe na huduma hizo.

“Hilo litafanikiwa kama tutaelekeza jitihada zetu kwa kutatua changamoto za mahitaji jumuishi ya kifedha kwa makundi yaliyoachwa nyuma kama vile wanawake, vijana, biashara ndogo na za kati, watu wenye mahitaji maalumu, wakulima na wavuvi,” alisema.

Jambo jingine aliloshauri ni kuimarisha ulinzi wa walaji wa huduma za fedha hasa dhidi ya uhalifu wa kimtandao na vitendo viovu katika soko ili kuwajengea imani na kujiamini katika kutumia huduma za kifedha.

Pia kupunguza gharama za matumizi ya huduma za kifedha na kutengeneza miongozo na kanuni za udhibiti ili kuongeza huduma za kifedha kwa wananchi wanaojishughulisha katika shughuli mbalimbali.

Aliongeza kwamba kuna haja ya kuongeza jitihada katika kupanua miundombinu ya malipo ili kuchochea matumizi ya huduma rasmi za kifedha.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwataka wadau wote kushirikiana wakati wa utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha kila Mtanzania anatumia huduma rasmi za kifedha.

“Tunatarajia kufanya kazi pamoja ya kujenga sekta ya fedha yenye nguvu ili kuwawezesha Watanzania kuwa na uchumi imara unaoendana na mpango mkuu wa sekta ya fedha sambamba na mikakati ya uchumi wa kidigitali,” alisema Dk Mwigulu.

Awali, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Emmanuel Tutuba alisema mpango huu wa tatu wa huduma jumuishi za fedha, ni mwendelezo wa mpango wa pili na katika ujumuishi, wamefanikiwa kufikia malengo kwa kuwafikia Watanzania kwa asilimia 76 ukilinganisha na malengo ya asilimia 75.

Aliongeza kwamba malengo mapya waliyojiwekea katika mpango huu wa tatu ni kuwafikia Watanzania kwa asilimia 86 ifikapo mwaka 2028.

“Serikali itahakikisha inaweka mifumo ya usajili wa vijana na kuhakikisha wanafikiwa na huduma jumuishi za kifedha. Tutaweka mifumo itakayotambulisha kila kundi na kuliwezesha kufikia huduma za kifedha,” alisema Tutuba.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi