Kimataifa
Hali bado tete Kenya
Nairobi, Kenya. Idadi ya watu waliouawa kwenye maandamano Kenya imeongezeka na kufikia wawili hadi jana jioni.
Ofisa mmoja wa hospitali aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), baada ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kuwataka Wakenya kujitokeza barabarani kupinga nyongeza ya kodi.
Juzi, polisi walirusha mabomu ya machozi katika mji mkuu Nairobi, wakilenga msafara wa Odinga na kuchukua hatua kama hizo dhidi ya maandamano katika miji ya Mombasa na Kisumu.
“Tulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa amejeruhiwa na sasa amefariki dunia na kufanya idadi ya vifo kufikia watu wawili kutokana na maandamano jana,” alisema George Rae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga, iliyoko Kisumu ambako ni ngome ya upinzani kwenye Ziwa Victoria.
Jana, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya wawakilishi wa mashirika ya kiraia, akiwamo Jaji Mkuu wa zamani, Willy Mutunga, waliokuwa wakitaka kuachiwa kwa makumi ya watu waliotiwa rumande wakati wa maandamano.
“Siyo haki hata kidogo kwa polisi kuturushia mabomu ya machozi wakati tumekuja kwa amani kutaka kuachiwa kwa wanaharakati wasio na hatia waliokamatwa na kuwekwa rumande tangu jana (juzi)” alisema Wakili Lempaa Suyianka.
“Baadhi yao walijeruhiwa na wanahitaji matibabu.”
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, ukiwamo ukurasa wa Amnesty International wa Kenya, juzi walilaani polisi kwa kile walichodai ni kukamata watu kiholela na kutumia nguvu kupita kiasi.
Dennis Onyango, ambaye ni msemaji wa Odinga, jana alisema Muungano wake wa Azimio unapanga kufanya angalau tukio moja la maandamano kila wiki, huku mengine yakitarajiwa kufanyika Jumatano ijayo.
Odinga (78), alishindwa na Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti, 2022 na mara kadhaa amekuwa akilalamika aliibiwa kura.
Katika kikao na wanahabari kilichohudhuriwa na kiongozi wa ODM, Odinga, kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi alisisitiza wataendelea na maandamano hadi sauti zao zisikike.
“Tumewaarifu (polisi) Jumatano ijayo shughuli nchi nzima zitasimama, huku Wakenya wa tabaka mbalimbali wakishiriki maandamano makubwa katika kila upande wa nchi,” alisema.
Wiki iliyopita Ruto alitia saini muswada wa fedha kuwa sheria inayotarajiwa kuzalisha zaidi ya Dola 2.1 bilioni za Marekani kwa ajili ya hazina ya Serikali na kusaidia kuimarisha uchumi uliokumbwa na madeni makubwa.
Sheria ya Fedha imeleta kodi mpya au ongezeko la bidhaa muhimu kama vile mafuta na chakula, uhamishaji wa pesa kwa njia ya simu, pamoja na ushuru wenye utata kwa walipa kodi wote.
Serikali inasema ushuru utasaidia kuongeza ajira na kupunguza haja ya kukopa kwa ajili ya kufadhili shughuli za maendeleo.
Mahakama Kuu ya Nairobi mwezi uliopita ilisitisha utekelezaji wa sheria hiyo baada ya Seneta Okiya Omtatah kupeleka kesi kupinga uhalali wake wa kikatiba.