Kimataifa
Wanaume wanaotafuta vipimo vya DNA waongezeka – Wizara
Uganda. Idadi ya wanaume wanaotafuta vipimo vya vinasaba (DNA) kwa watoto wao imeongezeka, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani amesema.
Simon Mundeyi amesema asilimia ya wanaume wanaodai huduma ya DNA kwa watoto wao imeongezeka kwa asilimia 70. “Hivi majuzi, idadi ya watu wanaoomba huduma za DNA imeongezeka. Wiki iliyopita pekee, tulikuwa na takriban watu 40, ambao walikuwa wakitafuta huduma za DNA kupitia wizara kwa sababu wanajua kwamba tunadhibiti Maabara ya Uchambuzi ya Serikali,” amesema Mundeyi.
Kwa mujibu wa mtandao wa Monitor, vipimo hivyo vya DNA huonyesha uhusiano kati ya spishi au vitu (species or objects) na kwamba matokeo ya uchunguzi wa DNA mara nyingi hutumiwa na madaktari ili kuthibitisha kama mzazi ana uhusiano na watoto.
Maabara ya Uchambuzi ya Serikali ni kituo cha kupima chenye makao yake makuu Wandegeya, Jijini Kampala. Hata hivyo Msemaji huyo wa wizara hiyo hakutoa takwimu za miaka iliyopita. Hata hivyo, alisema miaka mitatu iliyopita wastani wa watu watatu wangetafuta huduma hizo kwa mwezi, lakini sasa idadi hiyo inakaribia mamia.
Mundeyi metanabaisha kuwa hajui ni kwa nini idadi ya wanaume wanaotafuta vipimo vya DNA kwa watoto wao inaongezeka. Hata hivyo mwezi Aprili, Askofu Mkuu wa Kanisa la Uganda, Dk Stephen Kaziimba, ameeleza kuwa asilimia 10 ya wanaume wanakana kuwa baba wa watoto wao.
Hivi karibuni, mmoja wa wafanyabiashar awa ndani, aliwapima watoto wake na kugundua kuwa wengi wao sio wake. Wiki iliyopita, Mahakama ya Wilaya ya Mukono iliamuru kufanyiwa uchunguzi wa DNA wakili Male Mabiriizi na ndugu zake ili kubaini ikiwa ni wa baba mmoja.
Mahakama inasikiliza kesi ambayo wahusika wanapigania mali ya Marehemu Mohamed Bazindule Lulibedda Mutumba.
Mtandao wa Monitor, umeendelea kueleza kuwa vipimo vya DNA vinavyohusiana na uzazi vimekuwa na utata nchini. Mnamo mwaka wa 2013, baada ya ajali mbaya huko Namugoona iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 38, miili saba iliteketezwa bila kutambuliwa na Polisi walilazimika kufanya DNA kwa jamaa za marehemu.
Hata hivyo, vipimo vya DNA vya baadhi ya watu waliojitokeza kuwa baba au kaka, havikulingana na marehemu. Lakini vipimo vya DNA kwa akina mama vililingana na vya marehemu.