Connect with us

Kitaifa

Azimio la Bunge laibua mapya

Dar/mikoani. Siku mbili baada ya Bunge kubariki makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji wa bandari nchini, wanasiasa, wanasheria na wachumi wamezidi ‘kuuchana’ mkataba huo huku wakisema kilichofanyika bungeni hakijakidhi matarajio ya wananchi na kinaficha makosa ya wakubwa.

Wamesema, mikataba ya kibiashara haistahili kupata ridhaa ya Bunge na endapo itahitaji kupewa ridhaa hiyo, maana yake inakuwa inahitaji ama mabadiliko ya sheria au utengenezaji wa sheria mpya.

Jumamosi, Bunge lilipitisha azimio hilo licha ya uwepo wa ukinzani mkali nchini, ukiwahusisha wanasiasa, wanasheria na wadau wengine wabaohoji manufaa ya uwekezaji huo wa bandari huku wengine wakitahadharisha Bunge kutopitisha azimio hilo.

Azimio hilo linahusu mapendekezo ya kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari nchini Tanzania.

Mjadala huo uliibuka baada ya kusambaa taarifa, kwamba Serikali ya Tanzania imeingia mkataba wa kuipa Kampuni ya Dubai Port World (DPW) fursa ya kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam na nyingine kwa muda wa miaka 100 na wengine wakienda mbali zaidi wakibainisha makubaliano hayana kikomo, taarifa ambazo Serikali ilizikanusha ikisema mkataba hali haujasainiwa.

Kabla ya Bunge kuridhia ndoa hiyo, Kamati ya Bunge ya pamoja ya Miundombinu na ile ya Uwekezaji wa Mitaji (PIC) ilishauri mikataba ya utekelezaji itakayosainiwa itaje muda maalumu ya utekelezaji wa miradi ambao utazingatia masilahi mapana ya nchi.

Baada ya Bunge kuridhia, tayari maombi ya kupinga uwekezaji huo yamefunguliwa mtandaoni Channge.org ambapo watu mbalimbali wanajiandikisha kupaza sauri na hadi jana saa 11.34 jioni waliokuwa wamejiorodhesha walikuwa 1,928.

Wakati hayo yakiendelea Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshalla alilieleza Mwananchi kuwa kilichofanyia Katika Bunge ni kufunika makosa ya wakubwa.

“Huwezi kugawa mali ya nchi kwa namna hiyo. Hakuna mtu anayepinga uwekezaji lazima kuwe na mpango mzuri wa uwekezaji na mali ibakie ya kwetu, akikosea uwe na haki ya kumtimua, sasa hata akikosea huwezi kumtimua huo ni mkataba gani,” alihoji.

Dk Nshala ambaye ni mtaalamu wa sheria za kimataifa na uwekezaji wa kimataifa alisema Azimio la Bunge “limevuruga mamlaka na himaya ya Tanzania”.

Alisema kilichofanywa na wawakilishi hao wa wananchi ni kukosa uaminifu kwa tafsiri sahihi ya Katiba kwani mkataba huo unaigawa nchi kwa DP World.

Baada ya azimio hilo la Bunge, Dk Nshala alisema kinachofuata sasa ni Kampuni ya Dubai Port (DPW) kuingia kuwekeza.

“Wao wanasema kuna awamu ya pili ya kuanza kujadiliana ili kuanza kuingia mikataba ya maeneo lakini kwa sehemu kubwa mkataba huu ni kinyume cha Katiba. Umekiuka ibara ya 8(1); 26(1), 27(1) & (2), 28(1) na 29 (5) za Katiba ya nchi, maana yake mtu amesaini kukabidhi maeneo ya nchi kwa nchi nyingine au kampuni binafsi, hii si sawa.

“Huu ni mkataba mama, kinga zote zilipaswa kuwepo humu ili hizo kinga zihamie kwenye mikataba midogomidogo, sasa tunasubirije hiyo mingine wakati tayari mkataba mkubwa umekosewa,” alihoji Dk Nshalla.

Mbali na Dk Nshalla, Wakili mwingine Bashir Yakub alieleza kushangazwa na uamuzi wa Bunge kujadili azimio la mkataba na si mkataba wenyewe ambao ungeonyesha kilichomo kwenye uwekezaji huo.

Alisema wabunge wameshindwa kutekeleza jukumu lao la kusimama kwa niaba ya wananchi kuhoji kuhusu mkataba huo badala yake wameishia kusifia.

“Karibu wabunge wote wamesema mkataba huu una tija kubwa kwa taifa. Halafu wanasema mkataba wenyewe ambao ni “HGA” bado haujaingiwa na Serikali. Sasa watuambie hayo masilahi ya Taifa waliyoyasema wameyaona katika mkataba upi”

“Kama mkataba umeshaandaliwa na upo kwa nini haujawekwa wazi ili ujadiliwe na Watanzania na kwa nini haujapelekwa bungeni ili ujadiliwe kama ambavyo limejadiliwa hilo azimio la ushirikiano?” alihoji Yakub.
“Shida yetu ni kujua Tanzania imeingia makubaliano ya nini, tutapata nini,

kwa muda gani, thamani ya makubaliano ni ipi, maeneo gani, ajira ni ngapi kwa namba, miundombinu ipi inaboreshwa, thamani yake ni ipi, tulikuwa tunapata nini na baada ya makubaliano tutapata nini, uchumi wetu utakua kwa asilimia ngapi,”alisema Yakub

Si wanasheria pekee waliokosoa hatua hiyo, Profesa wa Ibrahim Lipumba, yeye alisema kilichofannywa na Serikali ikishirikiana na wabunge ni sawa na kuweka kando uzalendo na kuruhusu mkataba wa upande mmoja utumike kuipoka bandari.

Profesa Lipumba ambaye ni mchumi mmbobevu, alisema mhimili wa Bunge ulipaswa kusimama kwa niaba ya wananchi na kufanyia kazi maoni yaliyotolewa kuhusu makubaliano hayo lakini wenyewe uimepitisha bila kujali wananchi wanasema nini.

“Tangu suala hili lilipoanza kujadiliwa watu walitoa maoni yao na hasa kuhoji kuhusu huu mkataba ambao kiuhalisia ni wa upande mmoja na inavyoonekana uliandaliwa na hiyo kampuni, halafu Serikali yetu ikasaini tu,” alisema Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)

“Kilichofanyika bungeni ni kama kiini macho maana hakuna kilichobadilishwa, hata vile vifungu vilivyoonekana kuleta shaka, nilitegemea wabunge wangehoji au kupendekeza vifanyiwe maboresho ila na wao wakaridhika kupitisha hivyohivyo,” aliongeza.

Alipotafutwa Katibu wa Bunge kuzungumzia hoja hizo za wadau kwa simu jana, alimtaka mwandishi wa Mwananchi awwandikie maswali, jambo ambalo lilifanyika lakini hadi tunakwenda mitamboni hakuna majibu yoyote yaliyotolewa.

Serikali yajibu

Alipoulizwa kuhusu maoni hayo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema juzi mjadala bungeni ulikuwa wazi na hivyo kuhoji ni makosa yapi ya Serikali wanayosema yamefichwa? “Mjadala bungeni ulikuwa wazi kipengele kwa kipengele, juzi lilikuwa kama semina watu walielimishana kipengele kwa kipengele sasa unavyokuja kusema umeficha makosa ya Serikali ni makosa yapi,” alihoji Msigwa.

Wakati Msigwa akieleza hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchuzi, Profesa Makame Mbarawa alizungumza na watendaji wa menejimenti wa wizara hiyo mkoani Tanga jana, alisema mkataba huo unalenga kuboresha utendaji kazi wa bandari hiyo (ya Dar es Salaam) ambayo ni moja ya maeneo makuu ya vyanzo vya mapato vya Serikali. Alisema bandari hiyo kwa sasa inachangia asilimia 37 ya bajeti ya nchi, lakini utendaji ukiboreshwa mchango wake unaweza kuongezeka maradufu hadi asilimia 67.


Zitto aibana Serikali

Jana, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara viwanja vya Furahisha jijini Mwanza alisema mjadala huo umeisha bungeni baada ya kupitishwa kwa azimio lakini kwa wananchi bado haujakwisha.

Kutokana na hilo, alisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kutoa tafsiri sahihi kwa wananchi kuhusu mkataba huo kwa kuwa bado wananchi wana hofu na mkanganyiko mkubwa kuhusu suala hilo.

“Kazi ya uongozi ni kutoa maana, kiongozi yeyote wajibu wake ni kutoa maana. Serikali ina wajibu wa kutoa maana kwa Watanzania kuhusu bandari ili kuondo hofu iliyopo,” alisema Zitto.

Alisema watu wanajadili masuala ya msingi ya nchi kwa ushabiki kama vile timu za mpira wa miguu za Simba na Yanga pasipo kutazama ukweli badala inaangaliwa hisia zaidi.

“Hata bungeni jana (juzi), kwa kiwango kikubwa mjadala ulikuwa wa kishabiki, haukuwa wa kutazama faida na hasara ili Bunge kutoa maelekezo ya namna ya kushughulikiwa suala hili,” alisema Zitto.

“Kwa kuwa sheria zetu zinataka anayeendesha bandari awe na hisa za wazawa, tunapendekeza DPW itakayoingia majadaliano na TPA itatakiwa kuunda kampuni Tanzania itakayofanya kazi pamoja.

“Tunataka hiyo kampuni itakayoundwa imilikiwe Tanzania na Dubai kwa asilimia 50 kwa 50. Kwa maana nyingine kampuni itakayoundwa iwe na hisa asilimia 50 na TPA iwe asilimia 50 itakuwa kampuni ya wote,” alisema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi