Kitaifa
Mkakati kudhibiti wasomi wasio na vigezo vyuo vikuu
Dar es Salaam. Unasoma au unataka kusoma shahada ya uzamili na uzamivu? Basi unatakiwa kujiandaa katika masomo kutokana na mbinu mpya ya Serikali inayokusudia kuanza kunasa wahitimu wasiokuwa na uwezo unaoendana na hadhi ya madaraja hayo ya elimu ya juu nchini.
Tayari Serikali imeshaagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kabla ya mhusika kutunukiwa shahada hizo, aitetee hadharani, huku mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ikiimarishwa kubaini uhalali na wizi wa kazi zilizowahi kufanywa na wasomi na kuhifadhiwa mitandaoni.
Katika hatua za kufanikisha ubora huo, Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda ameelekeza vyuo vyote kuhakikisha wahitimu hao wanatetea utafiti wao hadharani ili kuthibitisha uhusika wao kwenye tafiti hizo.
Mbinu hiyo ni miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda na wadau wa elimu, waliotoa angalizo kuhusu anguko la ubora wa elimu nchini.
Jana wadau hao waliunga mkono mbinu hiyo itakayokuwa tofauti na ilivyo mazingira ya sasa yenye uwezekano wa kufanya udanganyifu.
“Wakati unatetea thesis yako itakuwa hadharani, hata waandishi wa habari wanaweza kuwepo, lengo hapa ni kuhakikisha kama ni wewe kweli ndiyo umefanya hiyo kazi. Tutapunguza haya mambo ya watu kununua digrii au kufanyiwa kazi na watu wengine,” alisema Profesa Mkenda.
Mkenda alitoa agizo hilo juzi, alipokutana na wenyeviti wa mabaraza ya vyuo vikuu katika warsha iliyoandaliwa na TCU, huku akiwaagiza wenyeviti hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vyao. “Tunataka vyuo vyenyewe vianze kujihoji na kutafuta majibu ya kuongeza ubora katika kuhakikisha tunatoa elimu inayoakisi mahitaji ya watu. Nataka tuhakikishe wahitimu wetu wakimaliza wawe na ubora unaotarajiwa,” alisema Profesa Mkenda.
“Tunataka tuongeza umakini wa kusoma hizi thesis, tukibaini mtu amenakili kazi ya mtu mwingine tunaifuta hiyo PhD au Masters halafu tutakitangaza kile chuo kuwa hakifanyi vizuri, hili suala sio kwa Tanzania tu, lipo dunia nzima, hivyo ni lazima tuhakikishe tunasimamia ubora,” alisema Profesa Mkenda.
Waliochangia maoni hayo kuhusu mkakati huo wa Serikali ni pamoja na Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwamba alichokisema waziri ndicho kinachofanyika kwa kuzingatia mwongozo wa TCU kwamba kila tasnifu inapaswa kuwasilishwa hadharani.
“Hivyo ndivyo inavyotakiwa na inavyofanyika, inawezekana isionekana kwa sababu ya wingi wa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu na wakati mwingine kumbi zinazotumika katika vyuo ni ndogo, hivyo kuishia kuingia watu wachache,” alisema Profesa Semboja.
“Kulingana na miongozo ya TCU, mtihani wa tasnifu ni lazima ufanyike ukiwahusisha watahiniwa ndani na nje, wanakuwepo pia wasimamizi na mwenyekiti. Watu wengine wanaruhusiwa kuingia, sasa hapa itategemea ukubwa wa ukumbi.”
Profesa Shani Mchepange wa chuo hicho alisema aina hiyo ya utetezi wa tasnifu ni nzuri na imekuwa ikifanywa na chuo chake kwa uwazi.
Alisema chuo hicho huwa na taarifa ya uwepo wa mwanafunzi yeyote anayetetea tasnifu na milango inakuwa wazi kwa anayetaka kuhudhuria kulingana na ukubwa wa chumba cha mikutano.
Profesa Mchepange, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) alisema mitihani hiyo ya utetezi wa tasnifu hutoa fursa pia ya wanafunzi wengine kujifunza na kujiandaa pale wanapokuwa na lengo la kufikia hatua hiyo ya elimu. “Kwa chuo chetu hili limekuwa likifanyika, nizungumzie hasa idara yangu ya Kiswahili hakuna tasnifu inapita bila mhusika kufanya mtihani wa utetezi. UDSM kuna mkurugenzi kabisa anayehusika na masomo ya uzamili, ofisi yake ndiyo inasimamia hili.”
Mhadhiri huyo, ambaye pia alipitia mchakato huo alipowasilisha tasnifu zake kwa shahada ya pili na ya tatu, alibainisha kuwa utaratibu huo ni mzuri kwa kuwa unamjengea mhusika hali ya kujiamini, kutunza muda na kuweza kuwasilisha mbele za watu.
“Jambo linalozingatiwa ni muda, katika mtihani huu wa utetezi muda ni jambo la msingi, hivyo kila kitu kimetengewa muda wake kuanzia kuwasilisha, maswali, majibu hivyo lazima uende ukiwa umejipanga na ukimaliza ukawa umefaulu inaleta raha fulani,” alisema Profesa Mchepange.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema hatua hiyo itawezesha wanafunzi na wasimamizi kuwa na umakini katika uandaaji wa tasnifu.
Alisema kwa hapa nchini vipo baadhi ya vyuo vyenye utaratibu huo, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilichoanza kuwa na mitihani ya wazi ya tasnifu kwa miaka mitatu sasa.
“Imesaidia kuongeza umakini kuanzia kwa walimu wenyewe ambao ndio wasimamizi, tofauti na zamani ilikuwa mtahini wa nje akishaisoma na kuridhika unaruhusiwa kuhitimu,” alisema.