Kitaifa
Ubora wa elimu vyuoni shakani, wahadhiri tatizo
Dar es Salaam. Ubora wa elimu ya vyuo vikuu nchini unatajwa kuwa kwenye hatari kutokana na uhaba wa wahadhiri.
Baadhi ya wadau wa elimu waliotoa maoni juu ya takwimu mpya zilizotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) walisema jitihada za haraka zinatakiwa kufanyika kunusuru sekta ya elimu ya juu.
Takwimu hizo zinaonyesha bado idadi ya wahadhiri wanaotambulika na taasisi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wa ngazi hiyo.
Takwimu hizo zilizotolewa na ripoti ya ‘Vitalstats 2022’ zinaonyesha wahadhiri na wafanyakazi wengine wa kitaaluma katika taasisi za elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2022/23 ni 8,507, huku wakihudumu katika kada 17 na programu mbalimbali 2,160 katika vyuo hivyo.
Kwa mujibu wa kijitabu cha mwongozo wa elimu ya juu toleo la mwaka 2019 kilichotolewa na TCU, kwa masomo ya sanaa na sayansi ya jamii wastani wa mhadhiri mmoja anapaswa kufundisha wanafunzi 50.
Takwimu za TCU zinaonyesha kada ya masomo ya biashara kukumbwa zaidi na uhaba huo ambao wastani wa mhadhiri mmoja anafundisha wanafunzi 112, ikifuatiwa na kada ya elimu ambayo mhadhiri mmoja ana wastani wa kufundisha wanafunzi 75 na zaidi.
Katika kada ya sheria wastani wa mhadhiri mmoja anafundisha wastani wa wanafunzi 51 na zaidi.
Hata hivyo, mzigo unaoelemea wahadhiri wa kada ya sanaa unakaribia kuingia katika kada za sayansi na afya ambako miongozo ya TCU inataka mhadhiri mmoja afundishe wanafunzi 10 hadi 25, huku kwa sasa akifundisha wastani wa wanafunzi 23 na zaidi.
Pia, uhaba unakaribia kuikumba kada ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma ambayo kwa sasa ina wanafunzi 4,125, huku wahadhiri wakiwa 84 nchi nzima, sawa na wastani wa mhadhiri mmoja kwa wanafunzi 49.
Hatari ya wahadhiri kuzidiwa miaka ya karibuni inaonekana kwa kuangalia ongezeko la wanafunzi kuwa kubwa ikilinganishwa na wahadhiri.
“Mwaka 2022/2023 ongezeko la asilimia 7.2 ya wanafunzi limerekodiwa ikilinganishwa na waliosajiliwa mwaka 2021/2022, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.6 la wahadhiri katika kipindi hicho,” ripoti inaonyesha.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dk Paul Loisulie alisema uhaba wa watumishi katika vyuo vikuu nchini umekuwa ukisababisha walimu kubeba mzigo mkubwa katika ufundishaji na kusahau shughuli nyingine wanazopaswa kuzifanya.
Alisema ongezeko kubwa la wanafunzi limefanya walimu kuweka nguvu katika kufundisha peke yake na kuachana na shughuli nyingine kama kufanya utafiti na ushauri kwa umma.
“Mwisho wa siku utafiti ndio unakifanya chuo kitambuliwe na dunia, hili pia linaathiri ubora wa elimu inayotolewa,” alisema Dk Loisulie.
Alisema wakati mwingine upungufu wa walimu unasababishwa na kukosekana kwa watu wenye sifa ya kuziba nafasi hizo zinapotangazwa, huku akitolea mfano wa nafasi takribani 2,000 zilizotolewa mwanzoni mwa mwaka jana, wakiwemo wakufunzi wa vyuo ambazo mpaka leo hazijajazwa.
Naye Dk Luka Mkonongwa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alisema uhaba huu wa wahadhiri umekuwa ukifanya watafute namna nzuri ya kuhudumia wanafunzi ili kurahisisha kazi kutokana na mzigo mkubwa walionao.
“Hii inaanzia hata katika utungaji mitihani, mtu anatunga mitihani isiyokuwa na hadhi ya chuo kikuu ili kumrahisishia usahihishaji, huwezi kusahihisha easy 2,000 ndani ya siku 10, ni ngumu, mtindo huu sidhani kama tunaweza kuzalisha wahitimu wenye sifa ya kushindana kimataifa,” alisema Dk Mkonongwa.
Alisema kama hali hii isipodhibitiwa kwa haraka, nchi inaweza kuanza kuzalisha wahitimu wasiokidhi vigezo katika soko la ajira.
Kauli ya Serikali
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Juma Kapanga alisema licha ya kufahamu kuwapo kwa upungufu, Serikali imekuwa ikijitahidi kutafuta mbinu mbalimbali, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika kufundishia.
“Pia kama TCU imekuwa ikisaidia kudhibiti uhaba huu kwa kuhakikisha kila chuo kinachokuwa na kozi fulani basi kinakuwa na rasilimali watu ya kutosha, wamekuwa wakilisimamia hili na kama wanaona kuna upungufu wamekuwa wakizuia isifundishwe,” alisema Kipanga.
Wanafahamu kuwapo kwa upungufu huo ambao pia upo katika maeneo mengine, ikiwemo walimu shule za msingi na sekondari, huku akieleza kuwa haijawahi kutokea kujitosheleza
Septemba 13 mwaka jana akizindua mradi wa HEET, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali itahakikisha inawasomesha wahadhiri wa vyuo vikuu nje ya nchi ili kusaidia kutoa elimu ujuzi yenye kiwango bora kuendana na soko la ajira kimataifa.
Kupitia mradi huo wa miaka mitano uliozinduliwa, wahadhiri 1,100, wakiwamo 623 katika shahada ya uzamivu, wahadhiri 477 katika shahada za umahiri wanatarajiwa kusomeshwa katika nchi mbalimbali, ikiwemo Denmark, Ufaransa na Ubelgiji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu na Huduma za Jamii, Profesa Kitila Mkumbo alivyotafutwa kuzungumzia uhaba huo alisema ni vyema waulizwe TCU wenyewe kwa ufafanuzi zaidi.
Mitazamo tofauti
Wakati uhaba wa walimu katika vyuo ukitajwa kupunguzwa na walimu wa muda wanaoajiriwa na vyuo, wachambuzi wa elimu wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya matumizi yao. Wapo walioelezea athari zake na wengine wakisema ni jambo zuri.
Akizungumzia athari za walimu, Dk Loisulie alisema wakati mwingine wanakuwa hawawaandai wanafunzi vizuri kwa sababu ya muda mfupi walionao, hivyo inawafanya hata mazoezi wanayowapatia wanafunzi kuwa machache kuliko walimu walioajiriwa.
“katika utunzaji wa kumbukumbu ni ngumu pia na ni rahisi siri za chuo husika kuvuja, kutoa mrejesho kwa wanafunzi pia inachukua muda mrefu na wengine wasipolipwa hawatoi matokeo na hii inaweza kufanya chuo kuingia gharama nyingine mpya,” alisema Dk Loisulie.
Wakati wao wakiyasema hayo, kwa wanafunzi ni tofauti, kwani wanasema matumizi ya walimu wa nje wakati mwingine yamekuwa yakifanya wakose nafasi ya kupata ufafanuzi zaidi pale unapohitajika.
“Walimu hawa hufundisha kuendana na muda, kama ni wiki mbili basi atakimbizana ili aweze kufundisha amalize ratiba, anakosa muda wa ziada wa kusikiliza wanafunzi, ukihitaji ufafanuzi labda umpigie simu au umtafute kupitia mitandao tofauti na yule aliyeajiriwa muda wote yuko pale,” alisema Asangama Masekepa, ambaye ni mwanafunzi Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Dar es Salaam.
Nini kifanyike
Dk Loisulie alishauri Serikali kwa ni njema kuangalia namna ya kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu, ikiwemo kuajiri walimu huku akivitaka pia vyuo kutafuta mbinu mbadala kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na walimu wa muda.
Dk Mkonongwa alishauri Serikali kuangalia maslahi ya wahadhiri ili kulinda wale waliopo kwa kile alichoeleza kuwa kumtengeza mtu wa kuziba pengo lililoachwa ni gharama na linachukua muda mrefu.
Wakati wastani wa wahadhiri kwa wanafunzi ukiendelea kuwa changamoto, bado vyuo vya Tanzania vimeendelea kuwa nyuma katika namba za ubora katika majarida mbalimbali.
Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya ‘Times Higher Education (THE)’ unaoitwa ‘World University Rankings 2023’ Chuo Kikuu cha kwanza kilichong’ara kutoka Tanzania ni Muhimbili, kikiwa katika kundi la nafasi za 401 hadi 500.
Takwimu hizo zinaonyesha vyuo 500 bora duniani na kwa Afrika chuo cha kwanza kinatokea Afrika Kusini (Chuo Kikuu cha Cape Town) kilichoshika nafasi ya 160 kidunia kati ya vyuo 500 bora.