Kitaifa
Sh48.06 bilioni kumaliza kero ya maji Mafinga
Iringa. Hatimaye kero ya maji kwa wakazi wa mji wa Mafinga, Wilayani Mufindi inafika mwisho baada ya kuanzishwa kwa mradi mkubwa utakaogharimu Sh48.06 bilioni.
Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alitembelea mradi huo jana Mei 27, 2023 ili kukagua maendeleo yake na namna utakavyosaidia kumaliza tatizo la maji kwenye mji huo.
Kwa sasa maji yaliyo kwenye mji wa Mafinga yanatosheleza mahitaji ya wakazi kwake kwa asilimia 50 hadi 60.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Mashujaa, Chongolo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kero za wananchi zinamalizika na kazi hiyo, haiwezi kufanyika kwa mara moja.
“Nimetembelea kwenye mradi na nimeona tenki la lita milioni mbili linajengwa, tenki hili litaleta maji kwa wananchi wote na nyie wakazi wa Mafinga kwenye kata zote mmepewa kipaumbele,” amesema Chongolo.
Alisema kuna watu wamekuwa wakipinga kwamba Serikali ya CCM haifanyi kitu jambo linalopaswa kupuuzwa.
“Kuna mtu anaweza kufunga macho na kutamka nataka kuwa tajiri akawa tajiri kwa wakati huo huo? puuzieni watu wanaokuja na kupiga porojo, CCM hatujaja kupiga porojo ila ni kufanya kazi,” amesema Chongolo.
Kuhusu uhakika wa afya, Chongolo amesema wamekuwa wakiendelea na mkakati wa ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ili kupunguza msongamano kwenye hospitali za wilaya, mkoa na rufaa.
Mbunge wa Jimbo la Mafinga, Cosato Chumi alisema suala la maji ni miongoni mwa ahadi ambazo zilitolewa mwaka 2020 wakati wa kampeni hivyo, kukamilika kwa mradi huo kunaongeza imani kwa wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alisema ipo miradi mingi ya maji na afya inayoendelea kujengwa kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
“Utekelezaji wa ilani unaendelea na tunaendelea kuchapa kazi kuhakikisha kila fedha inayokuja kwenye mkoa wa Iringa inatumika kama ilivyopangwa ili kuleta maendeleo,” amesema Dendego.