Connect with us

Kitaifa

Shule binafsi zalia na utitiri wa kodi

Dar es Salaam. Wakati Bunge likiipitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2023/24, wabunge wamebainisha changamoto lukuki zinazozorotesha ubora wa elimu nchini, ukiwamo utitiri wa kodi kwenye shule binafsi.

Changamoto nyingine zilizoainishwa na wabunge wakati wakichangia bajeti ya wizara hiyo ni uwepo wa nyaraka nyingi zinazotolewa na sekta hiyo, huku shule za sekondari na msingi zikipata fedha ndogo ya ruzuku.

Akichangia wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jason Rweikiza aliitaka Serikali kutozichukulia shule binafsi kama washindani wao, badala yake kuondoa changamoto zinazowakabili.

Alisema kuna kodi 18 ambazo Serikali inatoza kwa shule binafsi, zikijumuisha kodi ya mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ya kulipia mabasi ya shule yaliyoandikwa.

“Basi lako mwenyewe uandike jina unalipia TRA. Ushuru wa huduma unalipia wakati sheria inakataza kodi hii kwa shule. Kuna michango ya Umitashumta na Umisseta, usipotoa unakipata cha moto,” alisema.

Rweikiza, ambaye pia ni mmiliki wa shule za St Anne Maria Academy alisema kodi hizo zinafanya shule kufa kwa sababu zinashindwa kujiendesha.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo alitaka wizara hiyo kukaa chini na wenye shule binafsi na kutatua changamoto zao kwa sababu wanafunzi walioko katika shule hizo ni watoto wa Tanzania.

“Leo kuna walimu 25,926 wapo shule binafsi za msingi na 21,343 za sekondari, zisingekuwepo wangekuwa mitaani wanasotea ajira za Serikali. Lakini katika shule hizo binafsi kuna wanafunzi 591,005 wapo katika shule za msingi na 291,882 wapo sekondari,” alisema.

Akichangia mada hiyo pia, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Oscar Ishengoma alisema wizara hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa nyaraka zinazotolewa mara kwa mara, jambo ambalo linaashiria kuwa kuna tatizo kwenye Sheria ya Elimu.

“Zipo nyaraka nyingi sana Mwenyekiti, unaweza ukafanya utafiti wa PhD (shahada ya uzamivu), kwenye maeneo 13 kuna nyaraka lukuki, nidhamu na malezi zipo tisa, kamati ya bodi za shule kuna nyaraka sita,” alisema.

Alitaja maeneo mengine na idadi ya nyaraka kuwa ni udahili wa wanafunzi (17), mihula na siku za masomo (3), michezo (5), elimu ya ualimu (9), kufukuza, kurekebisha na kuhamisha wanafunzi (11). Maeneo mengine ni uendeshaji wa mitihani (19), masharti ya usajili wa shule (6), kukuza uzalendo (1), ajira za nje (1), ada na michango (14), taaluma, ufaulu na ufundishaji wa lugha (28).

Ruzuku ndogo

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Yustina Rahhi alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya Sh10,000 kwa mwaka kwa mwanafunzi wa shule za msingi ambapo Sh4,000 hutumika kugharamia vitabu.

“Ukigawanya hiyo Sh6,000 kwa mwaka ina maana ni Sh500 kila mwezi kwa mwanafunzi. Ruzuku hii ni ndogo,” alisema.

Alishauri Serikali kuongeza ruzuku hiyo kufika angalau Sh25,000 kwa mwaka kwa wanafunzi wa shule za msingi ili kutatua changamoto hiyo inayorudisha nyuma ubora wa elimu nchini.

Wadau wafunguka

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MENT), Ochola Wayoga alisema madhara yanayotokana na utitiri wa kodi katika shule hizo, ni kufanya gharama kwa wazazi wanaochagua kwenda upande huo kuwa kubwa.

Alisema pia uwepo wa kodi nyingi unamaanisha Serikali imeshindwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika kupunguza msongamano, kutoa ajira na kuchangia kuendeleza rasilimali watu nchini.

“Ni ubaguzi, elimu haipaswi kuwa na ubaguzi inapoletwa wala inapopokelewa. Kwenda shule binafsi haimaanishi mzazi ana uwezo sana na isiwe kama adhabu kwa walioamua kuzianzisha,” alisema.

Kwa upande wa mdau wa elimu kutoka Jukwaa la Sera la wamiliki wa shule binafsi, Benjamin Nkonya alisema kitendo cha Serikali kuweka kodi nyingi katika sekta hiyo, kunawafanya baadhi yao kukata tamaa kutoa huduma hiyo. “Wanakata tamaa, wanaamua kuwekeza kwenye maeneo mengine kimyakimya, sio kama hawa wafanyabiashara wa Kariakoo (jijini Dar es Salaam), waliojitokeza na kusema mbele ya Waziri Mkuu kinachowasibu kwenye masuala ya kodi.

Naye Mbunge wa Songwe (CCM), Philip Mulugo alitaka Serikali kuondoa mzigo wa tozo kwa shule binafsi.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema: “Nilikaa na kamishna wa elimu kwa sababu yuko kisheria akaniambia atatoa mwongozo wa shule binafsi, kwani hazilazimishwi kufanya hiyo mitihani lakini tunaweza kuzishawishi zifanye, zikiona ni mzigo zinaweza kuachana nayo”.

Alisema hiyo ni namna moja ya kuondoa tozo, lakini mengine ni mchakato wa Serikali kwa upana wake, hivyo asingeweza kuutolea ahadi. “Mchakato wa Serikali unahitaji muda, siwezi kuahidi chochote,” alisema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi