Connect with us

Kitaifa

Chalamila RC mpya Dar, Makalla apelekwa Mwanza

Dar es Salaam. Uhamisho wa Albert Chalamika kutoka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera hadi kushika nafasi hiyo katika Jiji la Dar es Salaam, ni sawa na kusema, ‘upele umempata mkunaji.’

 Uhamisho wa mwanasiasa huyo, aliyepitia misukosuko ya uongozi akiponzwa na kauli zake, umetangazwa leo Jumatatu ya Mei 15, 2023 kupitia taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus.

Kulingana na taarifa hiyo, aliyekuwa na wadhifa huo Dar es Salaam, Amos Makalla anakwenda kuutumikia Mwanza, wakibadilishana na Adam Malima aliyehamishiwa Morogoro.

“Fatma Mwassa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amehamishiwa Mkoa wa Kagera,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kaliba ya uongozi hasa nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, imezoeleka kushikwa na mtu machachari wa maneno mdomoni, kusadifu kile kinachoelezwa kuwa ‘mtoto wa mjini’.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba, katika Jiji hilo, ni vigumu kusoma au kuendana na asili ya wakazi wake, kwa kuwa sehemu kubwa ya wanaoishi si eneo walilozaliwa.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, wamewahi kupita watu kama Yusuph Makamba, William Lukuvi, Abbas Kandoro, Said Meck Sadick na Paul Makonda, wote hao ni machachari kwa siasa za majukwaani.

Kabla ya Kagera, Chalamika aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kutenguliwa Juni 11, 2021.

Hatua ya kutenguliwa kwake, ilihusishwa na zilizowahi kutolewa naye.

Aprili 6 wakati wa hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu, Rais Samia alisema viongozi wa kitaifa wakikutana na mabango katika ziara zao, atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na mkuu wa wilaya husika.

Hata hivyo, Juni mwaka 2021 akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais Samia mkoani Mwanza, Chalamila aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo wakiwa na mabango mengi yaliyoandikwa chochote.

“Nachukua nafasi hii kwenu waandishi wa habari, kuwakaribisha wananchi wote tarehe 13, 14 na 15, tuweze kumpokea Rais kwa mabango mengi, ya aina yoyote ile hata kama ataandika tusi aandike, yoyote yale,” alisema Chalamila.

Uteuzi wake wa kwanza katika nafasi ya Mku wa Mkoa aliupata Julai 29, 2018 alipoteuliwa na Hayati John Magufuli.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi