Kitaifa
Rais Samia aeleza faida za mawasiliano vijijini
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha faida mbalimbali za kusogeza huduma za mawasiliano kwa wananchi wa vijijini ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za matibabu ya kimtandao.
Rais Samia ameeleza hayo leo Mei 13, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa minara ya simu vijijini kati ya serikali na watoa huduma ambao ni kampuni za Airtel Tanzania, TTCL, Vodacom Tanzania, Mic Tanzania (Tigo) na Vietel (Halotel).
Amesema huduma hizi za mawasiliano zinakwenda kuimarisha huduma za matibabu kimtandao vijijini, hivyo itarahisisha utoaji wa huduma hizo kwa wananchi wa pembezoni.
“Huduma hizi za mtandao zinakwenda kutusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua. Mradi mkubwa wa M-Mama ambao tuliuanza Tanzania na sasa unaibwa na wengine, tumekwenda kupunguza vifo hivi,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kwamba mifumo ya mawasiliano ikikaa vizuri kuanzia ngazi ya juu wizarani hadi kwenye vituo vya afya, inakwenda kuongeza usimamizi mzuri wa matumizi ya dawa na vifaa tiba katika vituo hivyo.
Rais Samia ameangazia pia suala la usalama akisema mawasiliano mazuri vijijini yatachochea na kukuza usalama wa nchi kwa watu kutoa taarifa za vitendo vinavyotishia usalama katika maeneo yao.
“Tunakwenda kukuza usalama ndani ya nchi yetu, ndani ya maeneo yetu kwa sababu lolote litakalotokea ni rahisi kufanya mawasiliano na hali za uharibifu wa usalama zinachukuliwa hatua,” amesema.
Mkuu huyo wa nchi amebainisha kwamba mradi huo wa mawasiliano vijijini utaiwezesha Serikali kutekeleza malengo endelevu ya maendeleo (SDGs) kama yalivyowekwa ikiwemo kupunguza hali ya kutokuwa sawa.
“Kuna lengo la 16 ambalo linazungumzia jinsi ya kutumia huduma na kuongeza uzalishaji. Hili nalo tunatekeleza, tunapopeleka huduma vijijini, wananchi wa huko wanatumia mitandao zaidi na kuongeza uzalishaji,” amesema kiongozi huyo.
Rais Samia amesisitiza kwamba wanakwenda kuongeza matumizi ya mitandao kwa huduma za kifedha kwa maeneo ya vijijini hasa yale ambayo hayakuwa na mtandao, jambo ambalo amesema litachochea shughuli za kiuchumi.
“Tunachokifanya leo kinakwenda kugusa sekta mbalimbali za nchi yetu, kinakwenda kugusa maendeleo mijini na vijijini ili watu tuende kwa kasi katika maendeleo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amemtaka Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kupeleka suala la mawasiliano na Tehama kwa wadau ili watoa maoni yao jinsi wangependa kuona mitaala inakuwa.
“Sasa hivi kuna semina ya elimu inaendelea, tunataka wananchi watoe maoni kuhusu mitaala yetu. Nenda kalipeleke hili huko tupate pia maoni ya wananchi na nadhani mtashirikiana kabla semina haijaisha.
“Niwaombe wananchi watoe maoni wanavyoona tunaweza kwenda vizuri na mitaala yetu ya elimu. Tehama hii inakwenda kukuza elimu yetu kwa watoto wetu,” ameeleza Rais Samia wakati wa hotuba yake.