Connect with us

Kitaifa

Serikali yatoa Sh1.4 bilioni kutekeleza mradi wa EBARR Kishapu

Shinyanga. Serikali imetoa Sh1. 4 bilioni kwaajili ya mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi (EBARR) kwa wakazi wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga itakayowasaidia kujiongezea kipato na kuachana na uharibifu wa mazingira.

Miradi inayotekelezwa chini ya EBARR ni mradi wa unenepeshaji Mifugo katika Kijiji cha Muguda, mashine na jengo la kusaga mahindi na kukamua Alzeti, Bwawa la Maji Kijiji cha Kiloleli na Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi.

Mingine ni ujenzi wa Majosho, Majiko Banifu yatakayosaidia kupunguza matumizi ya kuni, ufugaji wa nyuki na kilimo cha zao la Mkonge.

Wakizungumza leo Jumamosi Mei 6, 2023 kwenye ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk Selemani Jafo wakati akitembelea kuona utekelezaji wa miradi hiyo, mnufaika wa EBARR na mkazi wa Kijiji cha Muguda, John Charles ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi hicho cha fedha.

Diwani wa kata ya Kiloleli wilayani humo, Edward Manyama amesema wakati wa kiangazi walikuwa wakipata shida ya maji kutokana na kutokuwa na bwawa la kuhifadhia maji ya mvua kwa muda mrefu, lakini Serikali imewakumbuka na kuwachimbia bwawa lililoondoa shida ya maji eneo hilo.

“Naishukuru Serikali kwa kutukumbuka. Wanawake walikuwa wanahangaika sana lakini kwa sasa Rais Samia amewaona, kwa niaba ya wananchi wote tutaitumia vizuri miradi hii na kuhakikisha inadumu kwa muda mrefu,”amesema Manyama

Mkazi wa kata ya Lagana, Luhende Nyangindu amesema miradi hiyo itawasaidia kujikwamua kimaisha kwa kujiongezea kipato na wanaamini mashine ya kukamua alzeti itasaidia wananchi kulima zao hilo kwa tija.

Amesema kutokana na miradi hiyo wananchi wilayani kishapu hawatakata miti hovyo kwa ajili ya kuchoma mkaa kwa sababu watakuwa na shughuli za kuwaingizia kipato.

Naye Dk Jafo amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kutekelezwa miradi hiyo ili wananchi wawe na shughuli mbadala za kufanya ambazo zitawaingizia kipato na kuacha kuharibu mazingira.

Amedai kuridhishwa na miradi hiyo kwakuwa imetekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa huku akiagiza miradi ambayo bado haijakamilika ikamilishwe na iwe tayari kwa matumizi kabla ya Julai mwaka huu.

Waziri huyo ameziagiza halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la upandaji miti 1.5 milioni kila mwaka pamoja na kuhamasisha kampeni ya soma na mti ambayo kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude amesema Serikali ilipeleka Sh1.4 bilioni kutekeleza miradi hiyo katika Kata mbili ya Lagana na Kiloleli ambayo imeleta tija kwenye suala la utunzaji mazingira.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi