Kitaifa
Hoja nane za Rais Samia kuleta tabasamu kwa watumishi wa umma
Morogoro. Hoja nane za Rais Samia Suluhu Hassan zimeamsha hamasa ya wafanyakazi nchini, huku Serikali ikiahidi kuendelea kuboresha maslahi yao, ikiwa ni pamoja na kuyafanyia kazi madai yao.
Akizungumza katika kilele cha sherehe za Siku ya Wafanyakazi duniani, ambapo kitaifa kimefanyika mkoani Morogoro, huku zilishajiishwa na kaulimbiu isemayo, “Mishahara bora na ajira za staha, ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi, na wakati ni sasa,” Rais Samia amesema, serikali yake haitawatupa wafanyakazi.
Akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na viongozi wa wafanyakazi kuhusiana na nyongeza ya mishahara, Rais Samia amesema serikali yake inakusudia kurejesha nyongeza ya mshahara ya kila mwaka, lakini pia; kwa mwaka mpya wa fedha, wafanyakazi watapata nyongeza posho kama ilivyotangazwa mwaka jana.
“Serikali itahakikisha inaendelea na utaratibu wake wa kuwapandisha vyeo na madaraja watumishi wanaostahili. Suala la nyongeza ya mishahara ya kila mwaka pia litaanza mwaka huu wa fedha na litakuwa ni zoezi endelevu kama ilivyokuwa hapo awali,” amefanunua.
Hata hivyo, Rais Samia hakuweka wazi kiasi cha nyongeza hiyo huku akitaadharisha kuwa ukimya huo unatokana na ukweli kwamba kumekuwepo na mazoea kwa jamii ya wafanyabiashara nchini ambapo ikitangazwa kupanda kwa mishahara, bei za vitu pia hupanda.
“Watu wamezoea, tukitaja kiwango basi wapandishe bei madukani, mara hii hakuna, tunakwenda kufanya mambo pole pole ili wasione tumeongezeana kiasi gani maana hii itasaidia mwenedo wetu wa bei, uwe salama,” amefafanua.
Kwenye suala la kodi kwenye marupurupu na makato zaidi ya mara moja, Rais amelitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Mawaziri wa Fedha na Ajira, kukaa pamoja na kufanya uchambuzi ambao utabainisha kipi kikatwe na kipi kisikatwe kodi.
“Katika kikao changu na Tucta, waliniambia mama hata zile zawadi unazotupatia zinakatwa kodi, lakini leo nimeshudia mtu anatoka na Sh12 milioni hapa, kwanini asikatwe kodi jamani, hiyo kodi ndiyo inarudi tena, tunakuja kuilipa kwenye marupurupu mengine,” amesema.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amemwagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kulifanyia kazi suala la waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi, huku akisema: “Lazima wawasilishe michango, hasa wale ambao serikali imewapa wao hawawasilishi, waende wakaitoe hiyo michango mara moja ili wafanyakazi walipiwe.”
Kwa mujibu wa Rais, tatizo la ucheleweshaji michango ya wafanyakazi katika mifuko ya jamii limekuwa sugu, hata hivyo amesema: “Mifuko hii ilifanya kazi kubwa ya kutaka wale wenye madai ya aina hiyo wayapeleke.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika wito huo, jumla ya madai 14,516 yalipokewa ambapo kati ya hayo, madai 13,523 (asilimia 93 ya madai yaliyopokewa), yamefanyiwa kazi na kwamba ni asilimia tatu ndiyo inatakiwa kushughulikiwa na ofisi ya Waziri Mkuu.
Kuhusu suala la wafanyakazi kukosa huduma za bima ya afya kutokana na malimbikizo ya malipo kwa watoa huduma, Rais amesema: “Sheriaya Bima ya Afya sura 395 inaelekeza kuwa madai ya watoa huduma yanatakiwa kulipwa ndani ya muda wa siku 60 tangu kupokewa.”
Hivyo basi, kwa kuwa Serikali haijatoa agizo jingine, Rais amewaagiza waajiri kuhakikisha wanalipa madai hayo ndani ya siku sitini kuanza Jumatatu Mei Mosi, 2023.
“Waziri Mkuu nenda kasimamie hili, kama mtu alijilimbikizia, ndani ya siku sitini alipe malimbikizo yote, wafanyakazi wafaidike na bima zao za afya. Na kuna wale waliokatwa asilimia tatu huku mwajiri hapeleki, naomba kalifanyie kazi ili waajiriwa wapate haki yao ya matibabu,” aliagiza.
Kuhusu upungufu wa watumishi na vitendea kazi, serikali yakiri kutambua hilo na kwamba iko kwenye mchakato wa kuongeza siyo tu watumishi, bali pia kuwapatia vitendea kazi ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Na kwamba ili kuimarisha Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (Osha), watumishi wapya 18 wameajiriwa na magari 13 yamenunuliwa. “Kwa upande wa idara ya kazi, tumenunua magari 17 na tuko kwenye mchakato wa kuongeza wafanyakazi ili vitengo hivi vifanye kazi zao vizuri.”
Rais Samia pia amezungumzia madai ya malimbikizo ya mishahara kwenye hospitali teule za mikoa na wilaya, huku akitaka uhakiki wa madai hayo kukamilika haraka na hivyo watumishi wanaostahiri basi walipwe stahiki zao kama inavyotakiwa.
“Ni kweli kuna madai mengi kutoka hospitali hizi, tumekuwa tukiyafanyia uhakiki ili kuona uhalali wa madai hayo. Watu ambao Serikali tulisema tutalipa mishahara na maslahi yao ni wale wanaoshughulika kwenye sekta, wale wanaofanya za kidaktari na za kitabibu,” amefanunua.
Kwa mujibu wa Rais, kwenye madai yaliyowasilishwa, kuna watumishi ambao hawafanyi kazi za kitabibu kama vile wapiga chapa, madereva na maofisa utumishi ambao kimsingi, hawahusiani na watumishi ambao Serikali inapashwa kulipa stahiki zao.
“Hivyo basi,” amesema Rais, “Niwahakikishie tutalipa madai yote baada ya kuyafanyia uchambuzi wa kina. Lakini pia, ili kuondoa utata huu uliopo kwenye hospitali zetu za DDH, tunafikiria kuingia mikataba ya kihuduma (service oriented contracts) na hivyo kurahisha utambuzi wa watumishi ambao serikali itawalipa.
Kwa upande wa walimu, serikali imeahidi kulifanyia kazi ombi lao la kurejeshwa kwa posho ya kufundishia kwa kadri ya uwezo wa kiuchumi, huku ikiahidi kufufua mpango wa elimu mtandao (e-education).
Mpango huu kwa mujibu wa Rais Samia, utahakikisha walimu wanapata mafunzo juu ya matumizi bora vya vishkwambi, sambamba na hilo, Serikali inaendelea na mazungumzo na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kila mwalimu nchini anapata kishkwambi chake.