Connect with us

Kitaifa

Samia, Kagame wajadili biashara, miundombinu

Dar es Salaam. Tanzania na Rwanda zimekubaliana kukuza biashara na kuimarisha miundombinu ya kukuza biashara baina yao sambamba na ulinzi na usalama katika Afrika Mashariki.
Hayo yalibainishwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na mawaziri sita wa Tanzania pamoja na wenzao wa Rwanda, miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye. Wengine ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Angelina Mabula.Akizunguza na vyombo vya habari kuhusu masuala waliyoyajadili na mgeni wake, Rais Samia alisema wamebaini kwamba kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo mawili hakiendani na kiwango cha rasilimali walizonazo na uhusiano mzuri uliopo. “Hivyo tumeona haja ya kukuza biashara na katika kuikuza, nimempa taarifa Mheshimiwa Rais (Kagame), Tanzania sasa tunafanyia kazi suala la kuimarisha bandari zetu, hasa za Dar es Salaam na Tanga ambazo Rwanda inazitumia,” alisema Rais. Pia walizungumzia umuhimu wa kuimarisha njia nyingine za mawasiliano ili Tanzania iweze kutoa huduma kwa ufanisi kule Rwanda na nchi nyingine zinazoizunguka. “Tumezungumzia pia mradi wa Rusumo ambao unakwenda vizuri na tumekubaliana kwenda kuuzindua kwa pamoja,” alisema.

Katika mazungumzo hayo, alisema wamezungumzia suala la ulinzi na usalama na kufikia makubaliano kuwa vyombo vya ulinzi vya Tanzania na Rwanda viendelee kuhakikisha nchi hizo zinakuwa salama. “Tumekubaliana vyombo vyetu viendelee kufanya kazi kwa pamoja tuhakikishe nchi zetu zinakuwa na usalama, lakini pia kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki,” alisema Rais Samia. Hata hivyo, alisema kuna masuala wameshayafanyia kazi, lakini bado hayajakamilika vizuri.

Hivyo, alisema wameiagiza Tume ya Kudumu ya Ushirikiano na ile ya kufuatilia utekelezaji wayamalizie kisha wakutane haraka kusaini makubaliano ili kazi ziendelee.
Kwa upande wake, Rais Kagame alisema Tanzania ni mshirika mzuri wa Rwanda katika biashara na usafirishaji. Aliishukuru kwa utayari wake wa kuimarisha uhusiano uliopo ili kuchochea maendeleo ya haraka na kampuni za mataifa hayo kuchangia katika soko la dunia.

“Nakushukuru kwa uongozi wako katika kutafuta suluhisho la kudumu katika mgogoro ndani ya kanda yetu, hasa mgogoro wa Mashariki ya DRC pamoja na wanachama wengine wa Afrika Mashariki. “Kujenga amani na usalama katika kanda yetu kunahitaji kujizatiti kwetu sote, wakiwemo wale wanaoathirika moja kwa moja,” alisema Kagame.
Alisisitiza amani na utulivu ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya Afrika Mashariki, huku akimshukuru Rais Samia kwa mapokezi mazuri.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi