Kitaifa
TRA kutatua changamoto za wajasiriamali
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema kupitia jukwaa la kongamano la wafanyabiashara na wajasiriamali lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) linalofanyika katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki jijini Dar es Salaam watafahamu changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati na kuzitafutia ufumbuzi.
Meneja Utafiti wa TRA, Saada Ally ndiye ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 27, 2023 katika kongamano hilo ambapo amesema kupitia kongamano hilo watatambua changamoto za kurasimisha biashara, usajili na kulipa kodi zinazowakabili wafanyabiashara.
Amesema milango yao iko wazi ndiyo maana wameweka vituo mikoani ili wafanyabiashara wenye sifa waende kujisajili tayari na kuanza kulipa kodi.
Ally amesema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 54.5 ya Watanzania wote ni walipakodi wakiwemo wafanyabiashara lakini anawahimiza wajisajili zaidi ili walipe kodi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
“Ndio maana kila mkoa tuna vituo vya usajili ambavyo mfanyabiashara mwenye sifa anaweza akaenda akasajiliwa kwa ajili ya kuanza kulipa kodi baada ya miezi sita,” amesema Ally.
Kongamano hili linaendelea katika ukumbi wa wa The Dome, uliopo Masaki jijini Dar es Salaam, limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media, Kampuni ya matangazo ya Ashton na ukumbi wa mikutano wa The Dome.