Kitaifa
IMF yaikopesha Tanzania Sh358.9 bilioni ya utekelezaji wa bajeti
Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) imeridhia kuikopesha Tanzania dola 153 milioni (Sh358.9 bilioni) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa bajeti yake ya Serikali huku ikiitaka kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kujiimarisha zaidi kiuchumi.
Taarifa ilitolewa jana Jumatatu Aprili 24, 2023 na Shirika hilo kupitia kwenye tovuti yake, imeeleza kuwa fedha hizo zinafanya jumla ya mkopo kufikia dola milioni 305 (Sh715.5 bilioni) kati ya dola bilioni 1.04 (Sh2.4 trilioni) zilizoidhinishwa kwa Tanzania, 2023.
“Licha ya kuwepo kwa changamoto za kiuchumi duniani lakini Tanzania inachukua hatua nzuri kwenye eneo hilo, mamlaka zinapaswa kufanya kazi ili kuongeza mapato ya ndani, kupunguza urasimu na kukabiliana na rushwa,”taarifa hiyo imeeleza.
Aidha, IMF imetoa angalizo kwa Tanzania kuimarisha kwa kuboresha ufanisi wa matumizi ya fedha na kukwepa malimbikizo ya madeni ya ndani.
“Mamlaka inapaswa kufuta malimbikizo ya madeni ya ndani na kuzuia mkusanyiko wa madeni mapya kwa kuimarisha usimamizi wa fedha”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa IMF, Antoinette Sayeh amesema kwa sasa deni la Tanzania bado ni himilivu na la wastani.
“Deni la Tanzania bado ni la wastani na himilivu, lakini ni muhimu kuendelea kuweka kipaumbele katika mikopo yenye riba nafuu,”amesema.
Kamishina Msaidizi wa Idara ya Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Yudica Saruni amesema fedha hizo zilizoidhinishwa ni awamu ya pili na ya mwisho kwa mwaka huu ambazo zitaingia kwenye mfuko wa bajeti kutimiza malengo ya kibajeti.
“Za kwanza ziliingia Agosti, 2022 ni ule mkopo nafuu wa miaka mitatu kila mwaka wanatuingizia karibu Sh700 bilioni,” amesema Saruni na kuongeza kuwa mkopo huo una riba ndogo na marejesho yake ni ya baada ya muda mrefu.