Kitaifa
Mvua yakata mawasiliano ya usafiri Kilimanjaro na Arusha
Hai. Mawasiliano kati ya Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha yamekatika asubuhi ya leo Jumanne Aprili 25, 2023 baada ya maji kujaa barabarani katika eneo la Kwa Msomali wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Tangu asubuhi magari yameshindwa kupita katika eneo hilo baada ya mto Biriri kujaa maji na kusababisha mafuriko na kupelekea kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro (RTO), Pili Misungwi amewatahadharisha madereva wanaopita katika maeneo hayo na kuwataka kuwa watulivu na wavumilivu kwa muda huu mpaka hali itakapokaa sawa.
“Tunawatahadharisha watumiaji wa barabara hii toka Hai kuja Moshi na wanaotoka Moshi kwenda Hai kuwa watulivu, pia wawe na subira, tukumbuke maji ni hatari na hayajaribiwi,”amesema.