Kitaifa
Zambia, Malawi kushirikiana na Tanzania sherehe za Muungano
Mbeya. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Khamis anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika katika mji wa Tunduma Mkoa wa Songwe mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Sherehe hizo ambazo zimeratibiwa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa kushirikiana na Kampuni ya Edwin Luvanda Branding Entertainment zitashirikisha watu zaidi ya 1,300 wakiwepo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, watumishi wa Serikali na raia zaidi 150 kutoka nchi jirani ya Zambia na Malawi.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Aprili 21, 2023 mratibu wa sherehe hizo, Furaha Mapunda amesema lengo ni kuenzi Muungano sambamba na kijadili masuala mbalimbali ya fursa za kiuchumi kwa maslai mapana ya Taifa ikiwepo mmonyoko wa maadili.
“Hili ni tukio la kwanza kufanyika katika Mikoa ya Nyanda za juu kusini na sababu ya kufanya katika mji wa Tunduma ni kujenga mahusiano mazuri baina ya viongozi,wananchi wadau kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe sambamba na raia wa nchi jirani ya Zambia ambao kuna mashirikiano ya shughuli za kiuchumi kupitia mpaka wa Tunduma,”amesema.
Mapunda amesema katika kuadhimisha sherehe hizo wanatarajia kuwa na makundi makubwa mawili la kwanza litafanyika mchana litashirikisha watu zaidi ya washiriki 1,000 ambao watafanya masuala mbalimbali ikiwemo maonyesho ya makabila na tamaduni, michezo huku kundi la watu 300 watashiriki usiku wa Muungano.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni Luvanda branding Entertaiment, Edwin Luvanda amesema kutokana na ukubwa wa tukio kushirikisha raia kutoka nchi zinazopakana na Tanzania hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa.
“Ni tukio la kwanza kukutanisha viongozi wa Mkoa wa Mbeya, Songwe na raia wa nchi jirani za Malawi na Zambia, ambao watajifunza mambo mbalimbali ikiwepo amani iliyopo ambayo inakutainisha viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, dini na wadau mbalimbali pamoja,”amesema.
Luvanda amesema miongoni mwa viongozi watakaoshiriki ni pamoja Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, viongozi wa kisiasa kutoka vyama mbalimbali Mkuu wa Mkoa wa Songwe, huku Mkoa wa Mbeya wa Mbeya Juma Homera atawakilishwa na Mkuu wa Wilaya Beno Malisa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Daudi Shubata amesema wameamua sherehe za Muungano katika Mkoa wa Songwe ni kuenzi tunu zilizoachwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na Amani Abeid Karume na kuonyesha mataifa na nchi jirani kuona umoja wa nchi ya Tanzania katika kujenga ushirikiano ulioachwa na wahasisi.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Ofisa elimu Mkoa wa Songwe, Michael Lugola amesema tayari wameanza maandalizi na wanatarajia kupokea wageni kutoka nchi za Malawi na Zambia kushiriki sherehe za Muungano Aprili 26 mwaka huu.
“Hii ni fursa pekee za kiuchumi katika Mkoa wa Songwe kwa wafanyabishara kwani watapokea ugeni mkubwa ambao pia utachoche kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma,”amesema.