Kitaifa
Spika wa Bunge aagiza tathimini ya kina Tasaf
Dodoma. Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameiagiza Serikali kufanya tathimini ya kina ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) ili kuondoa changamoto za muda mrefu ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wabunge.
Spika ametoa maagizo hayo leo Alhamis Aprili 20, 2023 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni baada ya wabunge wengi kulalamikia kuhusu changamoto.
Wabunge hao ni Aida Khenan (Nkasi Kaskazini-Chadema), Husna Sekiboko (Viti Maalum-CCM), Charles Kajege (Mwibara-CCM) na Mwita Waitara (Tarime Vijijini-CCM).
Akiuliza swali la nyongeza, Khenan amesema mchakato wa kuwapata wanufaika uligubikwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa vyama vya siasa
“Nini kauli ya Serikali yake kuhusu kupitia upya mchakato huo ili kuwapata wanufaika stahili,”amesema.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete amekiri kutokea kwa changamoto katika baadhi ya maeneo.
“Lakini Serikali imeshayafanyia kazi na tunaendelea kutambua katika baadhi ya maeneo ya changamoto. Na nikuhakikishie katika jimbo lako la Nkasi Kaskazini timu ya wataalam wa Tasaf watafika,”amesema.
Kwa upande wake, Sekiboko amehoji kama Serikali haioni imewaonea wazee na vikongwe walioondolewa katika utaratibu wa Tasaf ili hali hawawezi kujikimu maisha yao.
Akijibu swali hilo, Ridhiwan amesema utambuzi ni shirikishi na unaanzia katika kijiji na ngazi ya Serikali ni uhakiki tu.
“Sio nia ya Serikali kuwaonea wala kuwanyima haki zao, natoa wito kwa wenyeviti wa Serikali za vijiji na halmashauri wanaangaliwa ili Serikali iweze kufikia malengo yake ya kuwasaidia Watanzania,”amesema.
Maswali yanayofanana na hayo yaliulizwa na wabunge wengine akiwemo Waitara na Kajege.
Hali hiyo ilimfanya Dk Tulia kutoa agizo kwa Serikali kwa kusema kuwa changamoto za Tasafzimeshakuwepo kwa muda na kwamba anadhani changamoto hizo zinatakiwa kupungua na si kuongezeka.
“Kama huyo ni masikini anatakiwa kutumia nauli kwenda kufuata hiyo hela inakuwa tena mtihani na maswali ya wabunge wengine wapo wengine hawapo,”amesema.
Amesema kwa namna ambavyo Serikali imefanya vizuri kwenye mpango huo, inabidi kufanya tathimini ya kina ili changato hizo ziondoke kwasababu wameshafanya kazi hiyo kwa muda mrefu.