Kitaifa
Stendi ya Magufuli haina mfumo wa uhifadhi maji
Dar es Salaam. Wakati ukusanyaji wa mapato katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli ukiongezeka, kumekuwa na changamoto ya mfumo uliopo kutoruhusu kuhifadhi maji pindi yanapokatika.
Kwa mwezi mmoja stendi hiyo imeongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Sh3 milioni kwa siku hadi kufikia Sh5.7 milioni baada ya Manispaa ya Ubungo kuanza matumizi ya N-Card Februari 20 mwaka huu ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Kutokana na ukubwa wa stendi hiyo inayohudumia watu 17,000 kwa siku, imekuwa ikisababisha adha kwa watumiaji wa stendi hiyo wanapohitaji kwenda chooni pindi maji yanapokatika kama ilivyotokea hivi karibuni ka siku mbili.
Inaelezwa kuwa ilipaswa kuwa na kisima kinachojitegemea ili inapotokea changamoto ya maji, isiathiri shughuli za usafirishaji na kusababisha adha kwa watumiaji.
Hata hivyo, Meneja wa stendi hiyo, Isihaka Waziri alisema kutokana na maelezo ya wataalamu, eneo hilo halifai kuchimbwa kisima kutokana na maji yaliyopo kutokuwa rafiki kwa matumizi.
Waziri alisema stendi hiyo ina visima viwili vyenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 600,000, lakini kutokana na uhitaji uliopo kunapotokea changamoto yanakuwa hayatoshi.
“Kwa siku matumizi yetu ni zaidi ya lita 200,000, endapo kukitokea changamoto ya maji kwa zaidi ya siku tatu itawalazimu kununua maji sehemu nyingine na kujaza kwenye visima hivyo,” alisema Waziri.
Alisema unaponunua maji na kuyajaza kwenye kisima, gharama inakuwa kubwa ukilinganisha na mfumo wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), gharama ya gari moja ni Sh40,000, ili yatoshe ni lazima ununue gari zisizopungua 60.
“Kuna uzembe ulifanyika, wakati wanajenga kituo hawakuweka mfumo wa kuteka maji ya mvua, tayari tumeshamtafuta mhandisi kwa ajili ya kufanya utafiti wa namna gani ya kuvuna haya maji na kuyaingiza kwenye kisima,” alisema Waziri.
Hata hivyo, alisema kituo hicho hakijaanza kutoa huduma zote, endapo kitakamilika kwa asilimia 100 ni lazima miundombinu ya maji iongezwe.
“Hakuna changamoto inayonisumbua kama hii, maji yanayotumika ni mengi sana, tunataka tuangalie ni namna gani ya kuongeza visima vya kuhifadhia maji ya akiba, lakini pia ununuzi wa mantenki makubwa,” alisema Waziri.
Baadhi ya abiria na watumiaji wengine wa stendi hiyo wameelezea kushangazwa namna stendi hiyo ya kisasa inavyokosa maji.
“Ni kitendo cha aibu kuona stendi kama hii inakosa maji, kwanza wasingetakiwa kutumia maji ya Dawasa, wangetakiwa wawe na vyanzo vyao wenyewe au wavume maji ya mvua badala ya kununua na kwenda kujaza kwenye visima,” alisema Miraji Msangi ambaye ni mfanyabiashara.
Doreen Haule alisema kwa siku mbili kumekuwa na tatizo kubwa la maji, miongoni mwa watu walioathirika sio wafanyabiashara tu, hata abiria wapo wanaosubiri usafiri wakati mwingine zaidi ya saa mbili au tatu.
“Stendi hii pamoja na ukubwa wake, inahudumia watu mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara, abiria na mafundi, ilipaswa kuwa njia mbadala kama ilivyo umeme unapokatika, kukosekana maji kwa zaidi ya siku moja inaweza kusababisha mlipuko wa magojwa,” alisema Haule.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii wa Dawasa, Neli Msuya akizungumza na Mwananchi kwa simu alisema kulikuwa na changamoto ya kiufundi, lakini imeshatatuliwa na tayari mitambo imeshawashwa, hali imerejea kama kawaida.
Stendi hiyo kubwa na ya kisasa ilijengwa kwa Sh50.9 bilioni na kuzinduliwa Februari 2021 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli.