Kitaifa
Polisi wadaiwa kuua kwa kipigo, raia wachoma kituo
Chato. Wananchi wenye hasira wamechoma kituo cha polisi Mganza, Wilaya ya Chato mkoani Geita wakipinga uonevu unaofanywa na askari polisi wa kituo hicho, wanaodaiwa kumkamata mtuhumiwa na kumpiga, kitendo kinachodaiwa kusababisha kifo chake.
Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, japo hadi jana jioni gazeti halikufanikiwa kupata undani kuhusu tukio hilo, ikiwamo madai yaliyotolewa na wananchi.
Kabla ya kuchomwa kwa kituo hicho, wananchi walikataa kuuzika mwili wa Enos Misalaba (32) anaedaiwa kukamatwa Machi 27 mwaka huu, akituhumiwa kuiba betri ya gari na kupelekwa kituoni na kupoteza maisha siku iliyofuata ya Machi 28 akiwa kwenye kituo cha afya Mganza alipofikishwa kwa ajili ya matibabu.
Familia ya marehemu ilisema haijui tatizo lililosababisha ndugu yao kulazwa hospitali na kuwa wao walipata taarifa ya kushikiliwa kituo cha polisi, lakini walipopeleka chai asubuhi hawakumkuta ndugu yao mahabusu.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wananchi ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini kwa ajili ya usalama wao, walidai kitendo cha polisi kuanza kuwashambulia wananchi kwa kuwapiga risasi ndicho kilichosababisha wachome moto kituo hicho.
“Wananchi wamechoma kituo baada ya askari kuanza kuwapiga wananchi risasi na wawili hali zao ni mbaya sijui kama wapo hai au la.”
“…mwanzo walikuja na mabomu ya machozi walipiga, lakini wananchi hawakufanya vurugu, walipoona mabomu yameisha wakaanza kufyatua risasi zilizowapata wananchi wawili wakaanguka chini, hapo ndio hasira zikapanda wakashambulia kituo,” alisema mwananchi mmoja na kuongeza:
“Polisi wa Mganza wamezidi kuonea wananchi, kituo hiki kimekuwa biashara kwa askari, wanaweza kufanya msako jioni wanakamata vijana bila makosa yoyote wanawalaza mahabusu, asubuhi ili utoke unaambiwa ulipe 50,000, wananchi wamechoka na uonevu, sasa tukio la juzi ndio limetibua hasira zaidi na ndio haya yametokea.”
Hali ilivyokuwa
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Samuel Misalaba alilieleza gazeti hili kuwa wakiwa kwenye eneo la maziko, vurugu zilitokea wakati historia ya marehemu ikisomwa na kueleza marehemu amekufa kwa kuugua kifua, kitendo kilichopingwa na wananzengo’ (wanakijiji) waliokuwa wakijua kilichompata kabla ya mauti yake.
“Tulikubali kuzika, tumepeleka malaloni tumeshachimba kaburi, wakati wa historia ya marehemu msomaji alisoma amekufa kwa kuugua kifua, ndio wananchi wakakataa na kubeba jeneza na kuurudisha mwili wakitaka waelezwe kifo cha marehemu kimetokana na nini na ndio wakarudisha mwili kituoni polisi wakaanza kupiga mabomu ya machozi na wananchi wakaendelea kuandamana,” alisema ndugu huyo.
Alisema Polisi walibeba jeneza lenye mwili wa ndugu yao na kuondoka nalo ambapo ziliibuka vurugu zilizosababisha polisi kutumia mabomu ya machozi na kupiga risasi, jambo lililowapa wananchi hasira nao wakaanza kupiga mawe na baadaye kuchoma kituo moto.
Alichokisema mama
Bertha Malongo, mama mzazi wa Simon Misalaba alisema alipata taarifa kwa jirani yake saa mbili usiku akimueleza amemuona mwanaye akisukumwa kuingia kituo cha polisi lakini hakujua sababu za kukamatwa.
“Asubuhi kabla sijatoka akaja mwenga (mke wa marehemu) akinieleza mume wake amekamatwa na tukatoka ili tununue chai hotelini na tulipofika kituoni nilimkuta askari kituoni nikamwambia nimeleta chakula, akataka nionje nikaonja, nilipomaliza aliniambia nimimine kwenye kikombe nimpelekee mwanangu, akaita jina Enos, mahabusu wenzake wakadai hayupo alipelekwa usiku hospitali,” alisema mama huyo.
Alisema alifika kituo cha afya Mganza na kumkata mwanae amelazwa huku amefungwa pingu mkononi akipumua kwa shida na hata alipomuita hakuweza kuitika na daktari alifika na kutaka mmoja wa familia amfate na kumtaka akamnunulie mwanae dawa ili aweze kutibiwa.
“Daktari aliniambia nitoe Sh3000 ili aweze kutibiwa akarudi kwa ndugu na kuomba fedha hizo kwa mwanaeume anaedai kuibiwa betri akilalamika kuwa yeye hakumpiga bali alipigwa na askari na baada ya kuandikishwa kwenye jalada aliambiwa atoe sh 9000 ili aweze kununua dawa na kabla hajapewa dawa nesi mmoja alimfuata na kumtaka akae pembeni na alipoona hapewi aliamua kurudi wodini na muuguzi aliyemtaka kukaa alimtangulia na alipofika alimuuliza afya ya mwanae na kuambiwa amekufa”
Alisema mwanae hakuwa mgonjwa na wakati wauhai wake alikuwa dereva wa bodaboda na wakati mwingine huendesha bajaji na hakuambiwa kilichosababisha kifo cha mwanae.
Mke wa marehemu
Regina Mathias alisema siku ya jumapili walikuja polisi pamoja na mgambo na mtu aliyedai kuibiwa betri walifika na kufanya upekuzi ndani na kuchukua betri iliyokuwa ikitumika nyumbani na kuondoka na mumewe majira ya saa saba mchana.
Alisema mumewe alimtaka asiwe na wasiwasi kwakuwa hajaiba kitu na kumtaka asimfuate kwakuwa atarudi lakini hakurudi na asubuhi alitoka na kuambatana na mama mkwe kwa ajili ya kupeleka chai na walipofika kituoni hawakumkutana badala yake walielezwa amepelekwa hospitali.
Alisema walimkuta amelazwa akiwa amevimba miguu akiwa kwenye hali mbaya huku akipumua kwa shida.