Kitaifa
Pinda: Adhabu ya kifo ifutwe nchini
Dar es Salaam. Hoja ya kufutwa kwa adhabu ya kunyongwa inazidi kupata nguvu, baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda kuungana na wadau wengine kutaka adhabu hiyo ifutwe na badala yake iwe kifungo cha maisha.
Mapendekezo ya Pinda yanaungana na wadau mbalimbali, wakiwamo mawakili, watetezi wa haki za binadamu na Baraza la Makanisa ya Kipentekosti Tanzania (CPCT) ambao wameshauri kufutwa kwa adhabu hiyo.
Pinda alizungumzia adhabu hiyo alipozungumza na wanahabari, baada ya kutoka kuwasilisha maoni na mapendekezo yake kwa Tume ya Haki Jinai.
Tume hiyo iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuangalia na kumshauri jinsi ya kuboresha mfumo na taasisi zinazohusika na suala la haki jinai.
Pinda alisema adhabu hiyo inampa tabu, kwa kuwa ni kufanya kosa juu ya kosa, na kwamba hadhani kama inatibu tatizo.
“Mimi adhabu ya kunyongwa inanipa taabu, kwa sababu ni kweli ametoa roho ya mtu katika mazingira yake, kwa hiyo sasa ili tumkomeshe, tumnyonge. Ni kosa juu ya kosa. Sidhani kama inatibu ugonjwa huo,” alisema Pinda na kuongeza:
“Adhabu hizi mara nyingi hazina tija sana kwa maana ya kuwafanya watu wasifanye hayo. Kinyume chake ni mkiwa na utaratibu unaowatia matumaini, wanaweza wakaona kumbe jambo hili ukilifanya ni baya, kwa nini tusirudi tu kwenye adhabu ya maisha?”
Alisema hata hao wa adhabu ya maisha kama baada ya miaka fulani huwa wanatoka kwa msamaha na kurejea uraiani, mtu huyo hawezi tena kwenda kuua isipokuwa kama ni mgonjwa wa akili.
“Kikubwa mimi ni hilo tu kwamba unaua na wewe unauawa. Kwa hiyo waliangalie tu. Nchi nyingi zilishaiondoa,” alisema Pinda.
Alisisitiza jibu la muuaji si kumuua kwa sababu kiuhalisia halisaidii kupunguza wauaji.
Ushauri kwa Magereza
Katika hatua nyingine, Pinda alipendekeza Jeshi la Magereza lijikite katika kurekebisha wafungwa ikiwa ni pamoja na kuwapa stadi mbalimbali na mafunzo ya kiufundi, ili wanapomaliza vifungo vyao, waweze kufuatilia kuona ni kwa namna gani wamebadilika.
“Katika maeneo mengi, hili la kurekebisha wafungwa limepewa nafasi kubwa. Mnamrekebisha mfungwa ili akitoka aweze kuwa ni raia mwema,” alisema Pinda.
Pia alipendekeza kinamama wajawazito wanapojifungua, watoto wasiachwe gerezani, ili wasiathirike na kushauri uandaliwe utaratibu wa kuwaondoa na kuwaunganisha na taasisi zinazolea watoto hadi wazazi wao watakapotoka.
Kilio kufutwa adhabu ya kifo
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa wakipendekeza kifungo cha maisha jela kinapaswa kuwa adhabu mbadala ya kifo baada ya mtu kuhukumiwa kunyongwa.
Aidha, kila Oktoba 10 wadau wa Mtandao wa Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani (WCADP), huadhimisha siku ya kupinga adhabu ya kifo, wakishinikiza kuwepo kwa adhabu mbadala.
Katika moja ya taarifa zake kwa umma, LHRC iliwahi kuandika: “Ni adhabu katili, haina lengo la kupunguza uhalifu. Pia mtu akihukumiwa kimakosa, haiwezekani tena kurejesha uhai wake.”
Mwaka 2017, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipendekeza kwa Serikali kupitia upya sheria inayotoa adhabu ya kunyongwa kwa kutenga muda maalumu wa kutekelezwa na ukipita, adhabu hiyo igeuke moja kwa moja kuwa kifungo cha maisha jela.
Kamati hiyo iliwataja marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kutotekeleza adhabu hiyo walipokuwa madarakani. Hata Rais John Magufuli alipoingia madarakani Novemba 2015 hadi anafariki Machi 2021, hakuwa ametekeleza adhabu hiyo.
Rais Magufuli alisema hataweka saini kwenye hati ya kunyonga mtu ambaye amehukumiwa na kupewa adhabu ya kifo.
Kauli ya Jaji Werema
Aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji mstaafu Fredrick Werema mara baada ya kutoka kutoa maoni yake, aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu adhabu hiyo, na kusema adhabu ya kifo haikuwa miongoni mwa mapendekezo yake kwa tume hiyo, lakini adhabu ya kunyongwa inatisha na lengo ni kufanya watu waogope, lakini hata hivyo makosa hayo ya mauaji yanaendelea.
Werema alisema adhabu hiyo ililetwa na Wazungu, lakini hata hivyo wenyewe walishaiondoa. Hata hivyo, alisema adhabu hiyo inaweza kubaki.
“Mimi ninachosema ni kwamba sisi kwetu hapa hatunyongi, mimi nataka iwe hivyohivyo ibaki kwenye statute (sheria), kwa sababu inaweza kutokea pia mahala ikabidi unyonge,” alisema Werema na kusisitiza:
“Kuna watu wanafanya mauaji ya kishenzi, kwa hiyo ukifika wakati huo, unaweza kutumia hiyo kuwaondoa katika jamii.”
Alisema maisha ya mtu siyo kama maisha ya kondoo na kwamba unapotoa damu ya mtu ambayo ndio uhai, lazima mtu awajibike.
Katika hatua nyingine, Jaji Werema alipendekeza Mahakama ifanye mabadiliko katika mfumo wa usikilizwaji wa kesi ili kuweka nguvu katika usikilizwaji wa kesi za jinai, badala ya kesi za madai kama ilivyo sasa. Pia, aliwataka majaji na mahakimu kutumia mamlaka yao bila kuogopa kwa mujibu wa sheria kuziondoa mahakamani kesi ambazo hazina ushahidi au zilizokaa mahakamani muda mrefu bila kuendelea.
Wakili Kambole
Katika mapendekezo yake aliyoyawasilisha kwa tume hiyo kwa maandishi, Wakili Jebra Kambole alidai kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu (Penal Code- PC), Sura 16, Marekebisho ya mwaka 2002, kinachotoa sharti la lazima la adhabu hiyo, kinakinzana na Katiba ya nchi.
Alifafanua masharti ya lazima ya adhabu ya kifo yanakinzana na Katiba, kwa sababu inaondoa haki mbalimbali za binadamu zinazolindwa na Katiba ya nchi.
Alizitaja haki hizo ni pamoja na haki ya kuishi, haki ya usikilizwaji kwa usawa na kutokubaguliwa kwa kuwa mtu aliyetiwa hatiani kwa kosa la mauaji haruhusiwi kujitetea dhidi ya adhabu, tofauti na washtakiwa wa makosa mengine ambao huruhusiwa kujitetea.
Pia alidai Mahakama inaondolewa haki yake ya uchambuzi sahihi na tathmini kabla ya kutoa adhabu, kinyume cha Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba. Hivyo alipendekeza mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo (Mahakama Kuu), iwe na mamlaka ya uchaguzi wa kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi na kwamba mtu aliyetiwa hatiani awe na haki kujitetea ili apewe adhabu ndogo. Wakili Kambole alifafanua mazingira yanayosababisha makosa ya mauaji, hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja na mwingine au tukio moja na lingine.
Awali, Wakili Kambole alijaribu kupinga sharti hilo kwa njia za kisheria baada ya kufungua kesi Mahakama Kuu bila mafanikio, kwani Mahakama hiyo iliitupilia mbali na hata alipokata rufaa Mahakama ya Rufani, pia iliitupilia mbali.
Mapendekezo ya CPCT
Mwanasheria na mjumbe wa Baraza la Makanisa ya Kipentekosti Tanzania (CPCT), Justine Kaleb aliwaambia wanahabari wamependekeza adhabu hiyo ifutwe kabisa, badala yake iwe ni adhabu ya kifungo.
Baraza hilo limependekeza kufutwa kwa adhabu hiyo kwa sababu ya kutotekelezwa, jambo linalosababisha mrundikano wa wafungwa hao magerezani na kwamba kuwepo kwa adhabu hiyo ni kuingilia kazi na mamlaka ya Mungu, kwani yeye pekee ndiye mwenye mamlaka na haki ya kuondoa uhai wa mtu.
Uamuzi wa AfCHRP
Mwaka 2019, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHRP) iliiamuru Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho katika sheria ya kanuni za adhabu, ili kuondoa sharti la lazima la adhabu ya kunyongwa kwa washtakiwa wanaopatikana na hatia katika kesi za mauaji.
Kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni za adhabu (Penal Code –PC), mtu anayepatikana na hatia katika kesi za mauaji, adhabu yake ni moja tu, yaani kunyongwa na haina mbadala.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema sharti la lazima la adhabu ya kunyonga, inakiuka haki ya kuishi inayolindwa na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ambao Tanzania imeuridhia na kuusaini.
Pia mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha ilisema utekelezaji wa adhabu hiyo ya kifo kwa kunyonga hukiuka haki ya utu.
Mahakama hiyo ilitoa amri hizo kwa Serikali ya Tanzania katika hukumu yake ya kesi ya kumbukumbu iliyofunguliwa na Watanzania watano; Ali Rajabu na wenzake wanne waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Serikali ilitetea adhabu hiyo kwamba ipo kwa mujibu wa sheria zake na kwamba iko sawasawa na kanuni za kimataifa ambazo hazizuii utolewaji wa adhabu hiyo.
Mahakama katika hukumu yake, ilitupilia mbali utetezi wa Serikali, badala yake ikakubaliana na hoja za wadai kuwa adhabu hiyo kwa jinsi ilivyo katika sheria za Tanzania, inapora haki ya kuishi kwa lazima na kwamba jinsi inavyotekelezwa, hukiuka haki ya utu.