Connect with us

Kitaifa

Chuo cha kimataifa cha reli kujengwa Tabora

Tabora. Serikali ina mpango wa kujenga chuo kikubwa cha reli mkoani Tabora chenye kiwango cha kimataifa kupitia Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora-Isaka na tayari imetenga Sh44.8 bilioni.

Akizungumza leo mjini Tabora, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC), Amina Lumuli amesema chuo hicho kinatarajia kujengwa eneo la Malabi lenye ukubwa wa ekari 183.1.

Amesema mkandarasi amekamilisha michoro kwa kadiri ya mahitaji ya chuo na ujenzi wake unatarajia kuanza ndani ya mwaka wa fedha 2022/23.

“Chuo kinajengwa eneo la Malabi, Manispaa ya Tabora na mkandarasi amekamilisha mchoro kwa kadiri ya mahitaji,” amesema.

Ameeleza kuwa ujenzi wa chuo hicho utawezesha kutoa mafunzo katika teknolojia mpya ya reli nchini iliyoletwa na mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Ameeleza kuwa Shirika linaamini ujenzi wa chuo hicho ambacho ni cha kwanza kwa Afrika Mashariki, kuwa utawezesha Tanzania kuwa kituo cha ujuzi wa SGR kwa nchi za ukanda wa Maziwa makuu na zingine kama za Zambia, Rwanda, Burundi na DRC kwani itaunganishwa hadi Burundi kupitia ujenzi wa reli ya SGR kwa kipande cha kutoka Uvinza hadi Gitega na kwamba nchi kama Burundi itategemea wataalamu wa uendeshaji kutoka Tanzania ambayo ina uzoefu tayari.

Kwa upande wa Chuo cha Reli,mkuu wa Chuo hicho, Damas Mwajanga amesema kuwa kimepata ithibati ya kufundisha kozi ya usafirishaji kwenye njia ya reli (Shahada), teknolojia ya matengenezo ya mabehewa na astashaha ya awali ya teknolojia ya matengenezo ya miundombinu ya reli.

Ameeleza chuo hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 660 kwa Tabora 400 na Morogoro 260 lakini kwa sasa wapo jumla 387, Morogoro wakiwa 144 na Tabora wapo 243 ingawa kwa sasa wapo likizo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Uwekezaji, Jerry Silaa kwa niaba ya kamati, amekipongeza Chuo cha Reli kwa kufunza watumishi wanaokarabati mabehewa na vichwa vya treni.

Amelitaka Shirika la Reli (TRC), wajipange kubeba abiria na mizigo kwani reli bado ina uwezo mkubwa wa kubeba mizigo.

Amesema Kuna nchi zaidi ya nane zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam ambazo zinahitaji mizigo yao kutumia reli iliyopo.

“Mmepitia changamoto nyingi na sisi tunawapa moyo mfanye kazi kwa uzalendo,”amesema.

Wajumbe wa kamati hiyo wamemaliza majukumu yao mkoani Tabora leo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi