Connect with us

Kitaifa

ATCL yaibana Airbus ndege zake kutokuruka, yaifikisha AFRAA

Unguja. Sakata la ndege mbili za Airbus A220 za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutofanya kazi limefika Shirikisho la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) huku mashirika manne ya ndege Afrika yakishirikiana kuwabana watengenezaji wa ndege hizo ili kupatiwa ufumbuzi.

Hatua hiyo inakuja baada ya ndege hizo mbili kushindwa kufanya kazi tangu Oktoba mwaka jana kutokana na hitilafu ya injini zake ambapo kampuni iliyotengeneza ndege hizo imeshindwa kuwa na injini za ziada hivyo kuwasababishia hasara wateja wake wanaotumia ndege hizo, ikiwemo ATCL.

Kwa sasa ATCL ina ndege 12, kati ya hizo ndege zake tatu hazifanyi kazi kwa sababu hizo za kiufundi, zikiwemo Airbus mbili zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 120 na 160.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema pamoja na mipango waliyonayo kuhakikisha wanatoa huduma thabiti ya kukidhi mahitaji ya soko, dhamira hiyo imejikuta ikiingiliwa na tatizo hilo la ucheleweshaji wa safari kutokana na changamoto hiyo.

Matindi alitoa kauli hiyo jana, wakati wa kikao cha nne cha baraza la pili la wafanyakazi wa ATCL kilichofanyika Unguja, ambapo alisema wanaendelea kuwabana watengenezaji wa ndege hizo kwa kushirikiana na mashirika mengine barani Afrika zenye umiliki wa ndege za aina hiyo.

“Kwa kweli hili ni tatizo, lakini tunaendelea kuwabana, kwa sasa tunashirikiana na mashirika mengine yanayotumia ndege kama hizo, likiwemo la Air Senegal, Egypt ili kututatulia tatizo hili kwa haraka,” alisema

Matindi alisema kwa sasa Shirikisho la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) limeamua kuingilia kati kuongeza nguvu ili mashirika hayo yapate haki zake.

Alisema Misri wana ndege 12 za aina hiyo na ndege 10 hazifanyi kazi.

Alisema watengenezaji hao wanatakiwa kuwalipa ATCL fidia ambayo ipo kwenye mkataba, lakini imechukua muda mrefu sasa na sasa imekuwa si suala la fidia, bali wameharibiwa biashara na kufanya shirika lipoteze mapato zaidi.

Matindi alisema AFRAA limeitisha kikao, hivyo watakaa waone jinsi ya kuendelea kukabiliana nalo.

Kwa mujibu wa Matindi, ufumbuzi wa tatizo hilo ni kulipatia shirika injini nyingine au ndege zitakazofanya kazi kwa kipindi kifupi wakati wao wakiendelea kutatua changamoto hiyo kupata injini za ziada.

Katika hatua nyingine, Matindi alisema kuna ndege mpya tano zinakuja, ikiwemo boeing 767 yenye uwezo wa kubeba tani 54 itayokuwa ya kwanza kutumiwa nchini.

Alisema hivi sasa kuna mizigo mingi, huku Zanzibar pekee ikiwa na tani sita hadi nane kila wiki, lakini zinachukuliwa tani mbili, hasa katika mazao ya bahari ambayo yana soko kubwa nchini China.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi