Kitaifa
Mabwawa manne kuinua sekta kilimo, mifugo Tanzania
Kalenga. Ujenzi wa mabwawa manne ya kuvuna maji ya mvua yaliyojengwa katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Mbeya yametajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa ukosefu wa maji kwa matumizi ya binadamu na kilimo.
Mabonde hayo yanajengwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji ili kuchochea sekta ya kilimo, ufugaji na kupunguza uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo.
Akizungumza katika ziara ya kujifunza ya waandishi wa habari Jumatano ya Machi 8, 2023waliofika Bwawa la Masaka, Wilaya ya Kalenga, Mkoa wa Iringa, Mhandisi wa Maji wa Bonde la Rufiji, Geofrey Simkonda alisema Bwawa la Masaka likianza kutumika litakuwa mkombozi kwa wananchi.
Alisema Bonde hilo lilianza kujengwa Mei mwaka jana kwa gharama ya Sh1.7 bilioni ambapo likijaa shughuli za kilimo na mifugo,”itakuwa mkombozi, wananchi wanaozunguka bwawa hili wataongeza vipato vyao.”
Mhandisi Simkonda alisema Bwawa hilo lenye uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya lita laki nne, litajaa ndani ya miaka miwili kama mvua zitakuwa za kutosha.
Naye Diwani wa Masaka (CCM), Methew Nganyagwa aliishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Bwawa hilo ambalo ni mkombozi kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.
“Kilimo kikifanyika, mazao yake yatakwenda kuuzwa maeneo mbalimbali nchini, huu ni uwekezaji mkubwa na wenye tija. Rais Samia ameonesha yeye ni mwamba kwenye mageuzi mbalimbali,” alisema
Kwa upande wake, Mkazi wa Makata, Betina Chang’a alisema bwawa hilo litakuwa na manufaa,”sana kwetu kina mama. Kwani maji haya yatatumika kwa kilimo na mifugo na itatuwezesha kupata maji kwa ajili ya kilimo, sasa tushindwe sisi tu kulima.”
“Kilimo sasa kitakuwa ni kila mara, kwani hatutategemea tena mvua. itatuongezea kipato mnajua mwanamke akiwa imara kiuchumi hata familia inakuwa imara kiuchumi,” aliema
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya wa Watumiaji Maji, Bonde Lupalama, Onesmo Nzulumi alisema,”kati ya vitu vilikuwa vinatuumiza ni kukosa maji ya uhakika. Sasa wananchi wataweza kulima kwa uhakika.”
Alibainisha wajibu wake mkuu ni kuhakikisha vyanzo vya maji haviharibiwi vyote, ukataji miti, kunyweshea maji mifugo na kuyatunza kwani,”utatuondolea uharibifu wa vyanzo vya maji kwani miaka mitano nyuma hali ilikuwa mbaya.”