Connect with us

Kitaifa

Profesa Wajackoyah: Aeleza alivyoitorosha familia ya Lema mikononi mwa askari 300

Arusha. Simulizi ya safari ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema, kukimbia nchi Novemba mwaka 2020, kamwe haitasahaulika na mwanasiasa maarufu nchini Kenya, Profesa George Wajackoyah ambaye ndiye alimuokoa asirejeshwe nchini Tanzania.

Lema alikimbia nchi akiwa na familia yake, kutokana na kupokea vitisho juu ya usalama wa maisha, kupitia Nairobi nchini Kenya na baadaye alikwenda nchini Canada ambapo ameishi hadi Machi mosi mwaka huu aliporejea nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Profesa Wajackoyah anasema alipigiwa simu maisha ya Lema yapo hatarini, ndipo akapanga na watu wake kama majasusi kwenda kumchukua.

“Mke wa Lema na watoto wakapitia mpakani na Lema nikampitishia pembeni mwa mpaka kwa pikipiki na baadaye tulimpakia kwenye magari ambayo tayari nilikuwa nimeandaa,” anasema.

Anasema wakati wanaondoka walifika eneo la Kajiado wakakuta barabara imefungwa na kuna askari karibu 300, walivyowaona wakasema ndio hawa.

“Lema akasema sasa nimekufa, wakati huo mke wake alikuwa gari lingine lililokuwa nyuma ila alikuwa jasiri kidogo,” anasema.

Profesa Wajackoyah anasema alibaini kiongozi wa askari hao alikuwa anatoka Ikulu ya Kenya ambaye awali ndiye alifanya naye mazungumzo na kumuelewa wanakwenda kumuokoa Lema.

“Baada ya kuzuiwa pale niliwasiliana na Ubalozi wa Marekani nchini Kenya na watu wa Amnest International,” anasema.

Anasema wakati wapo kwenye kizuizi hicho, yule ofisa wa polisi alikuwa anaongea na simu na alibaini alikuwa anaongea na maofisa wa polisi wa Tanzania akiwaeleza tayari wamemkamata Lema.

“Nilizungumza na mkuu wa polisi na mkuu wa usalama nchini Kenya lakini nikaona hawatusaidii, kwani kulikuwa na maelekezo kutoka Ikulu kutokana na mawasiliano ya Rais John Magufuli na Rais Uhuru Kenyatta,” anasema.

Anasema baada ya kuzuiwa walipelekwa Kituo cha Polisi Kajiado ambapo walikaa kwa saa 18.

“Jioni hivi nikawauliza mbona mnamshikilia na huyu mama ambaye alipita kihalali mpaka wa Namanga, ndio nikapata taarifa kuwa Serikali ya Tanzania imetuma ndege kuja Nairobi kumchukuwa Lema.”

Anasema akapanga mpango wa kumuondoa mke wa Lema na watoto kituoni ambapo alitumia gari lake.

Nikawaondoa, kufika njiani gari ikanoki injini, lakini nikapata gari jingine nikamhifadhi sehemu. Siku inayofuata asubuhi saa 11 nilirejea polisi nikiwa na waandishi wa habari wengi, wakiwemo wa BBC na watu wa Amnest International.

“Nikawaeleza polisi kulingana na sheria mtu akikimbia nchi kwa kuhofia usalama wake, hamtakiwi kumrejesha nchi kwake, nilijua polisi hawajui sheria.

“Hata hivyo, niliendelea kuchukua hatua, ikiwemo kwenda mahakamani kuweka zuio la Lema kurejeshwa Tanzania.

“Baada ya majadiliano ndipo walinikabidhi Lema na kuondoka naye, nilikwenda kumhifadhi Kenya hadi atakapoondoka, kwani yule Mkuu wa polisi alisema Lema asichukue muda mrefu Nairobi.

“Tulikaa naye wiki tatu Nairobi tukishughulikia mipango ya kwenda Canada ambako nina ofisi ya uwakili, hivyo nilizungumza na marafiki zangu huko kufanikisha safari,” anasema.

Ampongeza Rais Samia

Akimzungumzia Rais Samia Suluhu, anasema ni kiongozi wa kuigwa Afrika kwa sasa, amekuwa ni mtetezi wa demokrasia na uhuru wa kujieleza. “Nampongeza mama Samia, mimi namuita simba wa demokrasia na napenda Kenya tumuige, kwani anafanya kazi nzuri kwa sasa ila sijui miaka ijayo,” anasema.

Katiba mpya

Akizungumzia Katiba mpya, anasema ni jambo zuri kwa Tanzania kuwa nayo, lakini akashauri wasiwe na haraka sana, kwani inahitaji maandalizi na kujifunza zaidi. Akizungumzia Chadema, anasema ni chama chenye sera nzuri ambazo hata katika chama chake ameanza kuchukua baadhi ya vitu ili kuboresha sera zao.

Wajackoyah ni nani

Ni mwanasiasa na aliyegombea urais nchini Kenya mwaka 2022 kupitia chama chake cha Roots.

Anatoka katika familia maskini, akiwa amepitia dhoruba kadhaa, ikiwepo kuwa mlinzi, polisi kabla ya kukimbia nchini Kenya na kwenda kuwa mchimba makaburi. Ana shahada tisa, anazungumza lugha 11.

Alizaliwa Oktoba 24, 1959. mjini Jinja Uganda. Wazazi wake ni raia wa Kenya. Alihamia Nairobi akiwa na umri wa miaka 16, baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi.

Aliishi kwa kutegemea wahisani kwenye barabara za jiji la Nairobi kabla ya kuchukuliwa na jamii ya Wahindi na kupewa jina la Balaram.

Alilipiwa karo ya shule ya upili na jumuiya ya Wahindi aliokuwa anaishi nao. Alisomea shule ya upili ya St Peters Mumias na kumaliza masomo hayo mwaka 1980.

Alisajiliwa kwa mafunzo ya polisi katika chuo cha polisi cha Kiganjo.

Alifanya kazi kama ofisa wa polisi hadi ngazi ya mkaguzi.

Alipewa majukumu ya kukusanya ushahidi kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Robert Ouko. Alitorokea Uingereza mwaka 1990 baada ya kutoka kizuizini kwa sababu hakujihisi salama nchini mwake.

Shahada zake

Akiwa Uingereza, Wajackoyah alijiunga na vyuo vikuu kadhaa kwa ajili ya masomo ya juu, vikiwamo Warwick, Westminster na UOL Birkbeck.

Alikuwa anachimba makaburi mchana huku akiwa mlinzi usiku ili kulipa karo. Ana shahada kadhaa katika masomo ya sheria kutoka vyuo vikuu mbalimbali. Amesoma pia lugha ya Kifaransa, masomo ya usalama na uchunguzi wa uhalifu wa jinai, uchumi, filosofia na masomo kuhusu Afrika.

Baada ya kupata shahada zake akiwa Uingereza alifungua ofisi na kufanya kazi kama wakili wa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kwa miongo mwili kabla ya kuhamia Marekani ambako aliendeela kusoma sheria katika Chuo Kikuu Baltimore. Alirudi Kenya mwaka 2010 na kufungua ofisi yake ya sheria kwa jina Luchiri & Co. Advocates.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi