Kitaifa
JKT yataka vyeti vyake vitambulike rasmi VETA
Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeanza mchakato wa kuwezesha vyeti linavyotoa kwa vijana wanaomaliza mafunzo katika makambi mbalimbali vitambulike rasmi kwenye mfumo wa elimu ya mafunzo stadi.
Hali kadhalika, JKT inaendelea kuongeza miundombinu itakayowawezesha vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kupata mafunzo hayo yanayotolewa na jeshi hilo, hatua itakayoondoa malalamiko kwa vijana wenye vigezo vya kupata kazi kwenye majeshi ambao hawakupitia mafunzo hayo.
Mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Rajabu Mabele aliyasema hayo jana, wakati akizungumzia maadhimisho ya miaka 60 tangu kuasisiwa kwa JKT, yatakayoanza Julai mosi na kufikia kilele Julai 10, mwaka huu.
Alisema JKT imeanza mahusiano ya karibu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mamlaka ya Mafunzo Stadi (Veta), lengo likiwa ni kuwezesha elimu ya ufundi anayopatikana katika makambi ya jeshi hilo iweze kutambulika wanaporudi kwenye maeneo yao ya zamani.
“Hapa tunatoa elimu ya Veta, tunampa cheti, lakini cheti kile hakitambuliki kwenye mamlaka husika inayodhibiti ile elimu ya Veta. Kwa hiyo tumewahusisha Wizara ya Elimu, tumeshakutana nao katika makambi mbalimbali kuangalia mapungufu yaliyopo tuyarekebishe ili vyeti vile viweze kutambulika,” alisema.
Mkakati wa jeshi hilo kuongeza miundombinu kuchukua wahitimu wote wa kidato cha sita umekuja wakati baadhi ya wadau wamekuwa wakitaka wahitimu wote wapitie mafunzo hayo ili kuondoa ubaguzi wakati wa utafutaji wa ajira, tofauti na sasa ambapo wanaopata nafasi hizo ni wachache waliopita JKT.
Kuhusu maadhimisho ya miaka 60, Meja Jenerali Mabele alisema madhimisho hayo yatafanyika kupitia wiki ya JKT itakayoanza Julai mosi hadi Julai 9, 2023 kupitia shughuli mbalimbali.