Connect with us

Kitaifa

Shilingi bilioni 5 zazua balaa Jatu Saccos, wanachama waja juu

Dar es Salaam. Taarifa ya ukaguzi wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) kwa Jatu Saccos, umeibua mjadala miongoni mwa wanachama baada ya kuonyesha kuwepo kwa mkopo wa zaidi ya Sh5.172 bilioni usio na maelezo ya kueleweka.

Utata wa fedha hizo uliibuliwa juzi na Mkaguzi wa Coasco Mkoa wa Dar es Salaam, Brighton Mwang’onda alipotoa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za mwaka 2021 za ushirika huo katika mkutano mkuu uliofanyika jijini hapa.

Alisema ukaguzi huo umeupa ushirika huo hati isiyoridhisha kutokana na upungufu uliojitokeza kwenye hesabu zake.

“Sababu zilizochangia kuwepo kwa hati isiyoridhisha ni upungufu katika mikopo ya kilimo yenye thamani ya Sh5.172 bilioni kutokana na kutothibitishwa kwa ukubwa, thamani na ukweli halisi wa mashamba ya Jatu, hiyo imesababisha chama kupata hati isiyoridhisha.

“Hali hii imenifanya nishindwe kuthibitisha uhalisia na msingi wa mikopo hiyo, lakini orodha hiyo imekosa uhalisia kama zilivyo ledger ndogo ndogo za wanachama,” alisema.

Awali akieleza mapato ya chama hicho, Mwang’onda alisema kwa mwaka 2021 yalikuwa zaidi ya Sh158.62 milioni, yakiwa yameongezeka kwa zaidi ya Sh59.64 tangu mwaka 2020 ambapo mapato yalikuwa ni zaidi ya Sh98.67, kukiwa na ongezeko la asilimia 60.2. Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wanachama wa Jatu Saccos walidai kunyimwa mikopo licha ya kutimiza masharti ya dhamana. “Mimi nina akiba zangu za kutosha, lakini nimeahangaika sipati mkopo, sijui huwa mnamkopesha nani? Mlisema wenye hati za mashamba ya parachichi, lakini nimekuja pale mara tatu nakataliwa,” alisema Mary Kibinga katika mkutano huo.

Hata Hivyo, Mwenyekiti wa bodi ya Saccos hiyo, Nicholaus Fuime alikanusha akisema ipo orodha ya wanachama waliokopeshwa.

“Mkisema mikopo haitoki si kweli, nina orodha ya waliokopa. Suala la hati sio upande wetu sisi Jatu Saccos, ni upande wa Jatu PLC,” alisema.

Kauli hiyo ilikatishwa na mwanachama Janeth Mwanga aliyesisitiza kuwepo kwa urasimu katika mikopo.

“Mwenyekiti usitufanye sisi kama sio watu wazima, tuliowekeza kule Jatu PLC na ndio hao hao tuko Jatu Saccos. Kule tunakutambua wewe kama meneja miradi, wewe ndio kinara.

Naye Fuime akijibu hoja hiyo alisema Saccos hiyo inaongozwa na vikao vilivyoruhusu matumizi ya hati hizo.

“Ni kweli mimi niliajiriwa na mkataba wangu uliisha nikahuisha nikaongeza tena, lakini hapa Saccos nimechaguliwa,” alisema. Hoja ya kuchanganyika kwa Jatu PLC na Jatu Saccos nayo iliibuliwa na Moses Lyimo akisema ndiyo inasababisha utata zaidi.

“Je, tuna uwezo wa kuiondoa Jatu PLC? Kwa kuwa hii ndoa haiwezi kufanya tena kazi tutaiondoa PLC na tutaweka Bodi ya Saccos watueleze kwa nini wametufikisha hapa. Baada ya majibu hayo tufanye uamuzi,” alisema.

Kwa upande wake, Msafiri Juma alihoji ilipo ofisi ya Saccos, baada ya kuhamishwa eneo la Sabasaba. Akijibu maswahi hayo, Fuime alisema baada ya ya ofisi zao kuondolewa eneo la Sabasaba walihamishia njia panda ya Kinyerezi.

Naye Elizabeth Temu aliyekuwa mfanyakazi wa Jatu Saccos, alisema alilazimika kuondoka na kompyuta mpakato ya ushirika huo baada ya kukaa miezi minne bila mishahara na bila mawasiliano na mabosi wake. Hata hivyo, alisema alishitakiwa Polisi na alikwenda kujieleza kuhusu madai hayo. Kutokana na malalamiko hayo, James Mushi alishauri mkutano huo uvunje bodi iliyopo na kuunda kamati ya kufuatilia madai yao.

Licha hoja hiyo kuungwa mkono na wanachama wengi, Mrajisi Msaidizi wa Dar es Salaam, Angela Nalime alishauri bodi hiyo isivunjwe akisema itasababisha kupotea kwa taarifa.

Baada ya mvutano huo, mkutano ulikubaliana kuanzisha kamati ya watu watano watakaosaidia na bodi iliyopo kufuatilia malalamiko hayo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi