Connect with us

Kitaifa

ACT yataka uchunguzi wa ‘miaka 7 ya giza’

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo jana kilizindua mikutano yake ya hadhara jijini hapa, ambapo pamoja na mambo mengine kiliitaka Serikali kufanya uchunguzi wa madudu yaliyofanyika katika kipindi cha “miaka saba ya giza’

Mbali na uchunguzi, chama hicho kimetaka hatua zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika katika maovu yaliyofanyika katika kipindi hicho ambacho vyama vya siasa havikuruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara.

Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alieleza hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mikutano ya hadhara kwa chama hicho, ambayo pia itafanyika Zanzibar na kuendelea katika mikoa mingine ya Tanzania Bara.

Alieleza kwamba katika kipindi hicho ambacho vyama vya siasa vilizuiliwa kuzungumza na wananchi, mambo mengi ya ajabu yalitokea na kwa kuwa wananchi walikuwa gizani, hawakuona wala kuambiwa mambo hayo.

Mwanasiasa huyo alisema katika kipindi hicho, Serikali ilikuwa inatumia mabilioni ya fedha kununua ndege ikiwaaminisha Watanzania kwamba kujenga Shirika la Ndege ni jambo la lazima kumbu nyuma yake kukiwa na madudu mengi.

Alisema nchi ilikuwa inatumia Sh500 bilioni kwa mwaka kwenye bajeti za Serikali za mwaka 2017, 2018 na 2019 kwa ajili ya kununua ndege.

Zitto alibainisha kwamba walipokuwa bungeni walihoji jambo hilo na Serikali ikaamua kuhamisha mchakato wa kununua ndege kuupeleka Ofisi ya Rais ili ukihoji uonekane unahoji masuala ya usalama wa Taifa.

“Hivi tunavyozungumza leo, katika ndege 12 za Shirika la Ndege la Taifa, ndege sita hazifanyi kazi, ziko chini kwa sababu zina kutu kutokana na manunuzi mabovu. Haya ni mabilioni ya fedha,” alidai Zitto.

Alisema hilo liliwezekana kwa kuwa nchi ilikuwa gizani na limewezekana kwa sababu mchakato wa kuzinunua hizo ndege ulifanywa na Ofisi ya Rais.

“Tunaitaka Serikali iweke wazi uchunguzi wa kina uliofanyika au unaofanyika kwa suala hili la ndege kukutwa na kutu. Nyinyi (wananchi) mna haki ya kufahamu mambo haya, nyinyi ndio walipakodi wa nchi hii, fedha zenu ndiyo zilinunua ndege zile.

“Tunataka Serikali iweke wazi bila kuficha nini kilitokea, hasara gani imetokea na hatua gani zimechukuliwa dhidi ya watu wote waliohusika na manunuzi haya kwa sababu wengine bado wapo, lazima wahukumiwe duniani ili haki iweze kutendeka,” alisisitiza Zitto.

Mara baada ya mkutano huo, Mwananchi liliwatafuta Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi ili kuzungumzia madai hayo lakini simu hazikupokewa.

Fedha za Plea Bargaining

Kiongozi huyo alisema Serikali iwaeleze pia Watanzania kuhusu fedha za watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya jinai walizozitoa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kuachiwa huru.

Alisema Rais Samia aliwaeleza Watanzania kwamba baadhi ya fedha hizo zilikutwa huko China, jambo ambalo liliwashangaza wengi na kuibua mjadala.

“Sisi kama chama tunasema haitoshi tu kuambiwa pesa zilipelekwa China, tunataka kuona uchunguzi wa kina wa nani alipekeka fedha hizo China, fedha hizo zilikwenda kwenye akaunti ya nani na wale ambao walihusika kuchukua fedha wachukuliwe hatua za kisheria.

“Wengine tunaambiwa bado ni majaji kwenye mahakama zetu, unawezaji kwenda mbele ya jaji ambaye alikuwa akipora mali za watu na kutegemea upate haki. Tunataka hatua zichukuliwe, watu hawa waondoke kwenye ofisi za umma.

“Hawastahili kuwemo kwenye ofisi za umma kwa sababu walitumia nguvu za dola, walitumia mamlaka waliyonayo, waliharibu ofisi zao kwa ajili ya kupora watu, kuumiza watu kwa sababu tu walikuwa na misimamo tofauti na Serikali,” alisema Zitto.

Alisisitiza kwamba watu ambao bado wako kwenye ofisi za umma, awe ni jaji au mtu yeyote, kama amehusika katika uporaji na kuumiza watu katika kipindi hicho, lazima wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

“Miaka saba ya kuwa gizani, Watanzania wanataka kuona haki ikitendeka na hatua ziweze kuchukuliwa. Hatutaki kusikia maneno matupu,” alisema Zitto huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Mabilioni bandarini

Zitto alisema Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa yake ya ukaguzi inayoishia Juni 2021, alieleza jinsi fedha zaidi ya Sh71 bilioni zilivyokuwa zinapelekwa bandari ya Mwanza bila maelezo yoyote.

“Watanzania wanataka kuona, yote haya yaliyotokea katika miaka saba ya gizani ambayo vyama vya siasa haviwezi kuja kwenu kuwaeleza namna gani nchi inaendeshwa, mambo haya yafanyiwe uchunguzi na hatua zichukuliwe. Hatuwezi kukaa kimya na kulindana, nchi haiwezi kwenda namna hiyo.

“Hakuna suala la funika kombe mwanaharamu apite katika masuala ya nchi, masuala ya nchi ni masuala yenu, tukifunika kombe leo atakuja mwingine atafanya vilevile, mtataka tena mfunike kombe. Nchi haitakwenda mbele.

“Ili nchi iende mbele lazima mambo yawekwe wazi, hatua zichukuliwe na kukomesha mambo kama hayo kutokea,” alisema Zitto.

Awali, Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji alisema kazi ya kupigania haki na uhuru, umoja na mshikamano haijasha huku akiomba ushirikiano kwa Watanzania.

Alisema ACT Wazalendo, ipo tayari katika harakati hizo, ndio maana kaulimbiu yake ni “Taifa la Wote, Masilahi ya Wote” iliyozinduliwa juzi ikitambulika kwa jina la “Brand Promise”.

“Nchi hii si ya CCM wala CUF, ACT Wazalendo wala Chadema bali ni Taifa la Watanzania, lazima tushirikiane ili kuleta maendeleo na maridhiano kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri,” alisema Duni.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud alisema wanaowaaminisha Watanzania kwamba chama hicho kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuwa CCM B, wameishiwa.

“Kwa masilahi mapana ya Taifa letu tuliamua kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hatukwenda kutafuta vyeo wala chochote, tuliangalia masilahi mapana ya taifa letu,” alisema Othman.

Naye Makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Dorothy Semu alisema chama hicho kinajiamini katika mazingira magumu ya siasa, ndiyo maana kilianzisha timu ya wasemaji wa kisekta ili kutoa mbadala wa mawazo yanayowasilishwa na Serikali.

“ACT Wazalendo ni chama cha siasa kinachokwenda na wakati, kinachagua namna ya kujiami na siasa ili kuendana na wakati husika. Kutokana na uchaguzi wa mwaka 2020 tuliamua kuunda baraza kivuli la mawaziri,” alisema Semu.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi