Connect with us

Kitaifa

Jinsi mawaziri wanavyopata tabu Wizara ya Maliasili na Utalii

Dar/Arusha. Wakati wadau wakishauri namna ya kuepuka mabadiliko ya mara kwa mara katika Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuimarisha utendaji wake, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesisitiza ushirikiano kati ya mawaziri na makatibu wakuu katika wizara zao.

Dk Mpango alitoa kauli hiyo jana wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwaapisha mawaziri na makatibu wakuu kutokana na mabadiliko aliyoyatangaza juzi kwa kumteua Mohamed Mchengerwa aliyekuwa waziri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kubadilishana nafasi na Balozi Pindi Chana aliyekuwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mabadiliko hayo yamewagusa makatibu wakuu wa wizara hizo pia, Dk Hassan Abbas aliyekuwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ameenda Wizara ya Utalii na Maliasili huku Said Othman Yakub akipanda kutoka kuwa naibu mpaka katibu mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika hafla hiyo ya uapisho iliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, Dk Mpango alisema ushirikiano baina ya watendaji ni changamoto. “Tumezungumza mara kadhaa na Rais Samia ameshalieleza hii mivutano kati ya waziri, naibu waziri au waziri na katibu mkuu haina tija, mkawe timu ya kuwaletea maendeleo Watanzania kwa sekta mnazoziongoza,” alisema:

“Ni sekta ambayo ina vishawishi vingi, nina uhakika Dk Pindi atakudokeza aliyokutana nayo katika kipindi chake. Mjiepushe na vishawishi hivi kama kwenye vitalu au mengineyo.”

Mchengerwa anatimiza siku ya tatu leo tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuongoza wizara hiyo ambayo mawaziri hawakai sana.

Kutokana na mazingira hayo, jana mawaziri waliowahi kuongoza wizara hiyo walishauri mamlaka za intelijensia na uchunguzi serikalini kushirikishwa katika uamuzi wa kutengua mawaziri kutokana na vita kubwa iliyopo.

Walisema wizara hiyo haikupaswa kuwa na mchango mdogo kwenye pato la Taifa na ukuaji wake unakwenda kwa kasi ndogo kutokana na mabadiliko ya muda mfupi yanayoathiri ubunifu wa waziri.

Kati ya mwaka 2005 hadi 2015, Rais Jakaya Kikwete alibadili mawaziri saba, wastani wa mwaka mmoja na nusu kwa kila mmoja. Hayati John Magufuli, aliyeongoza kwa miaka sita aliwabadili watatu sawa na wastani wa miaka miwili kila waziri.

Uteuzi wa Rais Samia aliyeingia madarakani Machi 2021, unamfanya Mchengerwa kuwa waziri wa tatu.

Akieleza uzoefu wake kuhusu mabadiliko ya mawaziri 10 ndani ya miaka 17 kuanzia mwaka 2005 mpaka 2023, aliyewahi kuitumikia wizara hiyo, Ezekiel Maige alishauri vyombo vya uchunguzi na Idara ya Usalama kuwa msaada kwa Serikali katika utoaji wa taarifa sahihi zinazohusisha utendaji wa wizara hiyo.

“Wizara hiyo ukiwa msafi ni tatizo, ukiwa mchafu ni tatizo. Ukiwa msafi utawindwa na waovu ambao ni wabaya wako kama waziri. Kwa mfano kipindi chetu (akiwa waziri) baraza la mawaziri liliendeshwa na nguvu ya Bunge, huwezi kujua kelele zipi zina ukweli,” alisema Maige ambaye ni mfanyabiashara kwa sasa.

“Haiwezekani mawaziri wote hao walikuwa dhaifu. Kwa mazingira hayo, hata matokeo chanya huwezi kuyaona kwani waziri anaingia kwanza aisome sera, sheria, miongozo, mipango, achunguze mifumo na afanye uchambuzi wake kabla ya kuanza kuingiza ubunifu wake halafu anaondoka ndani ya miaka miwili,” alisema.

Katika mawaziri 25 walioongoza wizara hiyo tangu Tanzania ipate uhuru, ni Zakhia Meghji pekee ndiye aliyedumu kwa mufa mrefu akihudumu kuanzia mwaka 1997 hadi 2005. Wizara hiyo inatizamwa zaidi kutokana na mchango wake wa zaidi ya asilimia 17 kwenye pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.

Mitazamo ya wadau

Wadau walisema sababu za kung’olewa kwa mawaziri hao ni migogoro ya mgao wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, migogoro ya ardhi maeneo ya hifadhi, migongano ya watendaji, ujangili, kasi ndogo ya ukuaji na malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA), Emmanuel Mollel alisema kutodumu kwa mawaziri kunarudisha nyuma maendeleo ya utalii.

“Nadhani imekuwa ikitokea bahati mbaya kutoijua vyema sekta hii hivyo wanatumia muda mrefu kujifunza na wakati wanataka kuanza kazi tayari wanajikuta kuna tatizo limetokea. Sasa hii inaifanya hii wizara kuwa kama training college (chuo cha mafunzo),” alisema Mollel.

Joseph Mahondo mzoefu katika uwindaji wa kitalii alisema “kitalu kimoja kinakodishwa kwa hadi dola 60,000 za Marekani (Sh139 milioni) na kuna maeneo ya utalii wa kimkakati ambayo wawekezaji wanalipa zaidi ya dola 100,000 (Sh230 milioni), kama waziri au katibu mkuu sio mwadilifu ni rahisi sana kurubuniwa na kuchangia migogoro maeneo ya WMA (Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori) bila kujua,” alisema.

Jumanne Hussein, mfanyabiashara wa wanyamapori alisema anaamini kitendo cha watendaji wa wizara kutosimamia usafirishaji wa mijusi, nyoka, kobe, ngedere na wengine ni miongoni mwa dosari inayowaondoa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Faustine Zakaria alisema wanaoteuliwa wajifunze haraka.

“Hii wizara ina mambo mengi na kosa moja linaligharimu Taifa na maisha ya watu hivyo umakini ni muhimu,” alisema.

Yaniki Ndoinyo, muhifadhi aliye masomoni nchini Uingereza alisema wizara hiyo imekuwa ikiwatumikia wawekezaji na masharika ya kimtaifa zaidi kuliko kusikiliza kero na matatizo ya wananchi hatua inayosababisha kero na mikasa mingi kwa Serikali.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi