Connect with us

Kitaifa

Nafasi za kozi za vyuo vikuu kufikia malengo ya Dira 2050

Takriban wanafunzi 125,000 ambao ni zaidi ya asilimia 99 ya waliofanya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka huu wamefaulu. Hivi sasa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu tayari zimefungua madirisha ya udahili na zinaendelea kupokea maombi ya wanafunzi wapya kwa mwaka wa masomo unaotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.

Hata hivyo, changamoto moja bado haijapata mwarobaini ambalo ni wimbi la wanafunzi ambao hawajui kozi gani wachague wala sababu ya kuichagua. Wapo si wachache, wanaopata ugumu kutambua ni fani gani za kitaaluma au kiufundi wanapaswa kuchagua kulingana na malengo yao ya baadaye.

Matokeo yake, ni kuchagua kozi bila kufanya uamuzi sahihi. Mwishowe, baadhi hujikuta wakisoma fani wasiyoipenda wala kuimudu, jambo linalopunguza hamasa ya kujifunza, ubunifu na ufanisi wa kitaaluma.

Baadhi ya waombaji niliozungumza nao wakati wa maandalizi ya makala haya, wengine walionesha huchagua kozi kwa kubahatisha. Mwingine alikiri kuchagua tu kwa sababu jina la kozi linapendeza, au kwa kuwa “ipo tu,” au marafiki zake wa karibu wameichagua.

Wengine waliichagua kwa sababu mtu fulani anayemfahamu aliwahi kuisoma. Kwa mtazamo wangu, huu si uchaguzi unaotokana na shauku binafsi au ushauri nasaha (career counselling), bali ni mwendelezo wa kuiga au kufuata mkumbo.

Wapo ambao pia huchaguliwa fani na familia zao. Hili siyo baya moja kwa moja endapo uchaguzi huo umezingatia weledi, uwezo, na hamasa ya anayekwenda kujifunza.

Tatizo hujitokeza pale ambapo mwanafunzi analazimishwa kusomea fani fulani, kwa mfano “soma udaktari,” hata kama hana uwezo wala mapenzi na taaluma hiyo.

Lakini pia wapo pia wengine ambao hawana msukumo wowote, wala hawajui wanapenda nini. Hali ambayo naweza kusema inatafakarisha zaidi: kwamba inawezekanaje kwa kijana kuwa na safari ya miaka 13 ya masomo bila kuwahi kuwa na ndoto yoyote ya maisha ya baadaye, au ya anachokipenda?

Aidha ni kwa mwanafunzi, au mfumo wetu wa kutoa maarifa, kuna kitu tunahitaji kuongeza kuwafanya wanafunzi wapate ndoto, wajue njia, na kufahamu njia hizo zinawapeleka wapi katika safari ya kujenga nguvu kazi ya kitaifa yenye maarifa na ujuzi stahiki.

Ikiwa hali hii ya wachache inatosha kuakisi uhalisia, na kama kweli ndiyo hali halisi ya wengi katika kundi hili, basi ni wazi kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050, dira inayolenga kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, uwezo wa kutumia teknolojia, na inayoweza kuchochea uvumbuzi, ushindani na kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tafiti katika masuala ya elimu zinaonesha kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya motisha ya ndani, umahiri wa kitaaluma, na mafanikio ya muda mrefu kwa anayejifunza.

Ryan na wenzake (2000), katika utafiti wao Self-Determination and the Facilitation of Intrinsic Motivation, wanaonesha kuwa wanafunzi wanaofuatilia taaluma kutokana na shauku ya kweli hujifunza kwa kina na hufanya vizuri zaidi kitaaluma. Kinyume chake, wanaochagua kozi bila nia ya ndani hubaki kusoma kwa ajili ya mitihani (“kusoma kwa ajili ya pepa”), badala ya kuelewa kwa undani na kutumia ujuzi huo katika maisha halisi.

Vivyo hivyo, De Lay na Swan (2014) wanaeleza kuwa uchaguzi wa fani usiotokana na msukumo wa ndani hupelekea kutojali, kupungua kwa bidii ya kujifunza, na hatimaye kuongezeka kwa utoro. Hali hizi huathiri moja kwa moja ufanisi wa mwanafunzi na ubora wa elimu anayopata. Hivyo, anaweza mtu kuwa na “digrii”, lakini kimaarifa, alivyo haendani na hadhi ya shahada yake.

Nchini Singapore, katika kukabili changamoto hii, Wizara ya Elimu imeanzisha Mwongozo Maalum wa Ushauri Elekezi kwa wanafunzi kuhusu uchaguzi wa fani za elimu na kazi. Mwongozo huu umeingizwa rasmi katika mitaala ya shule kuanzia ngazi ya msingi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye tovuti rasmi ya wizara hiyo, tangu mwaka 2012, wanafunzi huanza kupata mafunzo ya kupanga na kuchagua fani za kitaaluma wakiwa katika Darasa la Tatu (Primary 3) hadi sekondari, kupitia vipindi rasmi vya darasani. Aidha, wanafunzi hutumia jukwaa la mtandaoni linalojulikana kama MySkillsFuture kwa ajili ya kuchunguza taaluma mbalimbali na kuelewa njia za kuifikia.

Hapa kwetu nchini, ni muhimu kwa Wizara ya Elimu kuweka mpango wa kitaifa wa uhamasishaji wa taaluma wenye msisitizo maalum unaoanzia katika ngazi za chini hususan shule za msingi.

Kupitia mpango huo, wanafunzi waweze kukutana na wataalamu kutoka fani mbalimbali, kuchunguza taaluma tofauti, na kuelewa njia za masomo zinavyoweza kuwaongoza kwenye taaluma hizo. Ili kusaidia wanafunzi kufanya uamuzi sahihi kuhusu mustakabali wao wa kitaaluma.

Na vyuo vikuu viache kudhani waombaji wote wanajua na kuomba wanachotaka

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi