Connect with us

Kitaifa

Lissu afikishwa mahakamani, akionyesha ishara ya vidole viwili juu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ndani ya gari aina ya Land Cruiser nyeupe ya Jeshi la Magereza.

Lissu amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu, Mei 19, 2025 saa 2:53 asubuhi na kutumia dakika tatu ndani ya gari kabla ya kushushwa.

Baada ya askari ambao walivalia kofia za kuzuia uso usionekane wakiwa kwa wingi, walimpeleka Lissu hadi mlango wa nyuma wa kuingia mahakamani hapo.

Mwananchi iliushuhudia mkono mmoja wa Lissu pekee ukiwa juu, akionyesha alama ya Chadema vidole viwili juu.

Lissu tayari ameingizwa ukumbini na askari Magereza, ambao wote walifanya juhudi za kuzuia waandishi wa habari kutomuona kiongozi huyo kwa namna yeyote.

Lissu anapandishwa kizimbani leo Mei 19, 2025 kusikiliza kesi mbili ikiwemo ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni zinazomkabili.

Mbali na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo, kesi nyingine inayomkabili kiongozi huyo ni kesi ya uhaini.

Hata hivyo, leo kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa YouTube, imeitwa kwa ajili ya Serikali kumsomea hoja za awali (PH), ili kesi hiyo iweze kuendelea na usikilizwaji wa mashahidi.

Tayari baadhi ya wananchi wamefika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo, huku askari wakiwa wametanda ndani na nje ya Mahakama wakiwa kwenye mstari.

Askari hao ambao wamevalia sare na kiraia, wamekuja na mtindo tofauti na kujipanga mahakamani hapo wakati nyakati za nyuma walikuwa wakifanya doria nje Mahakama.

Hatua hiyo ni kuimarisha ulinzi kwa wafuasi wa Chadema  na Watanzania waliojitokeza mahakamani hapo, kusikiliza kesi ya Lissu ambayo Mahakama hiyo Aprili 28, 2025 iliamuru kiongozi huyo afikishwe mahakamani kusikiliza kesi yake.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi