Kitaifa
Siku saba za mtifuano wa vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Ni siku saba za mshikemshike kwa vyama vikubwa vya siasa nchini kupishana katika maeneo mbalimbali nchini vikijibizana na kurushiana vijembe, jambo ambalo linaongeza joto kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Vyama hivyo – CCM, Chadema na ACT Wazalendo vinaendelea na ziara mikoani ambako majukwaa yao yamekuwa yakitumika kuibua hoja mbalimbali na kujibu mashambulizi kutoka upande wa washindani.
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anaendelea na ziara yake katika Kanda ya Nyasa ambako tayari ametembelea mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa wakati makamu wake, John Heche naye akiendelea na ziara yake hukuhuko katika maeneo tofauti.
Kwa upande wa CCM, Makamu Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira amehitimisha ziara yake ya kukagua uhai wa chama aliyoianza Machi 14, 2025 na kuhitimisha Machi 30, 2025 katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Kagera, Shinyanga na Simiyu.
Kwa upande mwingine, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla naye amehitimisha ziara yake ya siku tatu aliyoianza Machi 27, 2025 na kuhitimisha Machi 30, 2025 akiwa ametembelea mikoa ya Mbeya na Iringa.
No reforms, no election yakolezwa
Lissu katika ziara hiyo hadi majimboni, anaedeleza lengo la kuelimisha umma kuhusu kampeni ya chama hicho – No reforms, no election inayolenga kuzuia uchaguzi ikiwa mabadiliko hayatafanyika kwenye mifumo ya uchaguzi, hoja ambayo imekuwa kama ya moto na kuwasukuma viongozi wa CCM kuijibu kila eneo.
Akiwa kwenye mikoa yote aliyotembelea, Lissu amejielekeza katika kueleza sababu za kutaka kuzuia uchaguzi ujao, huku akihusianisha changamoto wanazozipitia Watanzania na kukosekana kwa mifumo thabiti, inayowezesha upatikanaji wa viongozi bora waliochaguliwa na wananchi.
Akiwa Makongorosi, Chunya mkoani Mbeya, Lissu alisema uchaguzi ni namna pekee ya kupata viongozi. Alisema mawaziri wanaowaletea wananchi matatizo ni wabunge, na ili uwe mbunge lazima uchaguliwe na wananchi.
Alisisitiza kwamba Tanzania ikiwa na mifumo mizuri ya uchaguzi, watapatikana viongozi wazuri watakaotatua shida za wananchi badala ya kuziongeza. Alisema mfumo wa uchaguzi ni muhimu kwa wananchi kulifahamu na kulifanyia kazi.
Kauli kama hizo pia amekuwa akizitoa Heche katika maeneo anayopita, wote kwa nyakati tofauti wakionyesha kuwa wanataka uchaguzi wa kuaminika.
Akijibu hoja ya Chadema kuzuia uchaguzi akiwa Kahama mkoani Shinyanga, Wasira alihoji namna chama hicho kitakavyozuia uchaguzi wakati tayari mchakato wakeumeshaanza kwa kuboresha taarifa kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
Alisema pamoja na kampeni wanazoendelea kuzifanya, Chadema hawana uwezo wa kuzuia uchaguzi usifanyike kwa sababu tayari hatua ya kwanza ya uchaguzi huo imeanza kwa wananchi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
Wasira alisisitiza “hakuna mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi huo labda wawe wanaota ndoto ya mchana.”
Makalla atia timu
Akiwa mkoani Iringa, Makalla aliendelea kuinanga Chadema akidai kuna mgogoro unaondelea kufukuta ndani kati ya kambi ya mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe na kambi ya Lissu, zinazoendelea kunyukana tangu kumalizika kwa uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Januari 2025.
Makalla alihusisha kilichomtokea Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Siglada Mligo baada ya kudai kupigwa kwenye kikao cha ndani, akisema kuna vita kubwa ndani ya chama hicho.
Siglada anadaiwa kupigwa Machi 25, 2025 kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Milimani huko Njombe Mjini, kikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Heche, alikimbizwa na kulazwa hospitali.
Hata hivyo, Chadema kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, imesema kinafanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa jambo hilo.
Mbali na hilo katika maeneo mengine Makalla ametymia muda mrefu kujibu hoja za chadema kutaka uchaguzi usifanyike, akisisitiza kuwa mabadiliko wanayoyataka wamekwishafanyika kutipia baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda kikosi kazi.
Katika harakati hiyo, Makala alijikuta akitoa kauli yenye tuhuma iliyozusha sintofahamu na kusababisha wadau wakiwamo viongozi wa kisiasa kumvaa wakimtaka ajitokeze kutoa ushahidi au aombe radhi.
Makalla akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Simiyu alidai viongozi wa Chadema wamepanga kutumia fedha wanazochangisha kupitia kampeni yake ya Tone Tone kununua virusi vya Ebola na Mpox kisha kuvisambaza nchini, kauli ambayo imekosolewa, ikielezwa ni hatari kwa usalama na utalii.
Thamani ya kura
Wakati Chadema na CCM vikiendelea kurushiana maneno majimboni, ACT Wazalendo kimesema kipaumbele chake kwa sasa ni kupigania mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na kurejesha thamani ya kura ya kila Mtanzania kwenye uchaguzi.
Msimamo huo ulielezwa na Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la uzinduzi wa operesheni ya chama inayojulikana kama “Operesheni Linda Demokrasia” lililofanyika katika Jimbo la Lindi Mjini Machi 29, 2025.
Zitto alisisitiza kuwa hoja kuu ya operesheni hiyo ni mageuzi katika Tume ya Uchaguzi ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.
Alisema badala ya Wasira kuendelea kubishana na Chadema na ACT Wazalendo barabarani, CCM inapaswa kujua wanachohitaji vyama vya upinzani ni Tume Huru ya Uchaguzi, iliyopo ijiuzulu watu waombe upya.
Mwanasiasa huyo maarufu alisema vyama vya upinzani vinapigania mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, hasa kurejesha thamani ya kura ya kila Mtanzania kwenye chaguzi.
Alimshangaa Wasira kujibizana na Chadema badala ya kukaa na kuzungumza, wote wakiwa wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Akizungumza na wananchi Machi 30, 2025 akiwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Wasira alitumia nafasi hiyo kumjibu Zitto, akisema anaijua historia, hivyo anajua kwa nini anabishana na Chadema badala ya kuzungumza.
Akizungumza kuhusu madai ya Zitto kwamba CCM imekataa kukaa na Chadema, Wasira alisema si kweli kwa kuwa chama chake ni mwanachama wa TCD chini ya uenyekiti wa Lissu.
Aliongeza kuwa akiitisha kikao watakwenda maana wao ni watu wa amani, hawataki shari.
Wazungumzia mnyukano
Wakizungumzia mnyukano wa vyama hivyo, wananchi na wachambuzi wa siasa wameeleza kwamba kila chama kinapambana kuushawishi umma kwamba chenyewe ndiyo bora na kinasimamia jambo lenye masilahi kwa umma.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema siasa ni harakati zinazohitaji chama kuwashawishi wananchi na katika mchakato huo, chama kingine kinaweza kupotosha au kukosoa wanachofanya wenzao.
“Hili ni joto la uchaguzi, CCM wameona wakiwaachia Chadema wazunguke nchi nzima, watauaminisha umma kuhusu mabadiliko wanayoyataka, hivyo nao wametoka ili kueleza ya kwao na kuikabili Chadema,” anasema mwanazuoni huyo.
Mkazi wa Tabata, Isack Kanoni anasema amekuwa akifuatilia ziara za viongozi wa vyama vya siasa na kusikia majibizano yao ambayo anasema hayana tija kwa taifa.
Amesisitiza kwamba wananchi wanahitaji maisha bora.
“Siasa zao za majukwaani zinatuchanganya tu, wala hazina faida kwetu wananchi. Sisi tunataka familia zetu ziwe na maisha bora, wao huko majukwaani hawazungumzii watakavyoboresha maisha yetu, wanafikiria masilahi yao na vyama vyao tu,” anasema mwananchi huyo.
