Kitaifa
Wawili wakutwa na maambukizi ya Mpox Tanzania

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imesema imewabaini watu wawili kuwa na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox. Hii ni mara ya kwanza ugonjwa wa Mpox kuingia nchini.
Taarifa hiyo inakuja siku tatu tangu picha mjongeo iliyosambaa katika makundi ya sogozi, ikionyesha watu wawili wakiwa wamejirekodi na kudai kuwa na ugonjwa wa mlipuko wakiwa wametengwa eneo la Majani ya Chai, Kipawa, Wilaya ya Ilala.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, leo Jumatatu, Machi 10, 2025, imebainika kuwa watu wawili waliohisiwa na kutengwa kwa ajili ya matibabu wamebainika na ugonjwa huo.
Amesema, Machi 7, 2025, Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni, na sehemu nyingine za mwili.
Dalili hizo ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo
“Kati ya wahisiwa hao, mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam. Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa kwa uchunguzi.
“Machi 9, uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox,” amesema Waziri Mhagama.
Amesema hadi sasa jumla ya wahisiwa wawili wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini.
Waziri Mhagama amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na vituo vyote vya kutolea huduma za afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki.
Amesema chanzo cha ugonjwa huo ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu huweza kuupata kutokana na shughuli zinazoweza kusababisha kugusana na wanyama, majimaji au nyama za wanyama wenye maambukizi.
Aidha, endapo binadamu akipata maambukizi hayo anaweza kumwambukiza mtu mwingine kwa kugusana moja kwa moja.
Amesema Wizara ya Afya inawahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huo, hasa kutokana na uzoefu walionao wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
“Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa watu wanaoingia na kutoka kupitia mipaka ya nchi, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya na kuhamasisha jamii ili kuwawezesha wananchi kuchukua hatua za kujikinga,” amesema.
Mhagama amesema kwa kuzingatia kuwa magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi hayana tiba mahususi ila mgonjwa anahudumiwa kulingana na dalili alizonazo, Wizara inawasihi na kuwasisitiza wananchi wote kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga.
Amewataka wananchi kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu unapoona mojawapo ya dalili za ugonjwa wa Mpox au piga simu nambari 199 bila malipo.
Pia kuepuka kuchangia vitu kama nguo na matandiko ambavyo vimetumiwa na mtu mwenye dalili za Mpox.
Kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox. Kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Mpox. Kuepuka kumuhudumia mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox bila kuchukua tahadhari.
“Watumishi wa afya kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa wakati wote wanapowahudumia wagonjwa, ikiwemo wenye dalili za vipele na homa.
“Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono. Wizara ya Afya itaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huu, kadri taarifa za ufuatiliaji na uchunguzi zitakavyopatikana,” amesema Waziri.
Aidha, amesema wizara inashauri wananchi kuendelea na shughuli za kila siku kwa kuzingatia tahadhari za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.
Vilevile, ametoa taarifa kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Marburg, akisema umedhibitiwa na hadi kufikia leo Machi 10, 2025, zimetimia siku 41 bila kuwa na mgonjwa mpya.
