Connect with us

Kitaifa

Hizi hapa Parokia 15 zilizomegwa Dar es Salaam kwenda Bagamoyo

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thadaeus Ruwa’ichi amezitaja Parokia zilizomegwa kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwenda Jimbo jipya la Bagamoyo.

Parokia hizo ni, Bahari Beach, ⁠Boko, Bunju, Kinondo, ⁠Madale, ⁠Mbopo, ⁠Mbweni Mpiji, ⁠Mbweni Teta, ⁠Mbweni, ⁠Mivumoni, ⁠Muungano, ⁠Nyakasangwe, Tegeta Kibaoni, ⁠Tegeta, ⁠Ununio, ⁠Wazo na ⁠Mbweni JKT (Parokia Teule).

Askofu Ruwa’ichi amesema mapadri waliopo kwenye parokia hizo pamoja na waumini wake watakuwa Jimbo la Bagamoyo chini ya uongozi mpya wa jimbo hilo na si kwake tena.

Askofu Ruwa’ichi amezitaja parokia hizo saa chache kupita tangu kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Fransisko kumteua Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Stephano Musomba kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Bagamoyo kuanzia jana Ijumaa, Machi 7, 2025.

Kuanzishwa kwa Jimbo la Bagamoyo kunafanya idadi ya majimbo yote Katoliki Tanzania kuwa 36. Aidha, uteuzi huo unalifanya Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam kubaki na maaskofu wawili ambao ni Askofu Mkuu, Ruwa’ichi na Askofu msaidizi, Mchamungu.

Kabla ya uteuzi huo, Askofu Musomba alikuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam tangu mwaka 2021. Musomba na Muchamungu waliteuliwa Julai 7, 2021 na Papa Fransisko kuwa maaskofu wasaidizi wa jimbo hilo.

Katika maelezo yake, Askofu Ruwa’ichi amesema: “Kwa kauli hiyo mapadri waliokuwa kwenye parokia hizo wanajikuta moja kwa moja katika Jimbo la Bagamoyo. Kama wewe ni Padri wa Jimbo basi unatakiwa kuwa pale ulipokutwa. Wale wa mashirika unajikuta kwenye jimbo jipya naomba mtoe ushirikiano bayana kwa jimbo jipya.”

Askofu huyo Mkuu amesema: “Mpaka sasa mmekuwa mkimtaja Askofu Musomba kwenye sala ya Ekaristi, sasa hamtamtaja tena kwenye Jimbo la Dar es Salaam kuanzia leo (jana) kule Bagamoyo mtamtaja, Askofu mteule Musomba kama Askofu wetu, mimi na Askofu Muchamungu hamtatutaja tena, imekula kwetu.”

Amesema tarehe ya kusimikwa zitatangazwa baadaye.

Askofu Musomba amezaliwa Septemba 25, 1969 Malonji jimboni Mbeya. Baada ya masomo yake ya upadri alipewa daraja takatifu la upadri Julai 24, 2003 na kuhudumu katika nafasi mbalimbali za utume shirikani, jimboni Dar es Salaam na Morogoro.

Salamu za pongezi zimetolewa maeneo mbalimbali zikiwamo za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyempongeza Askofu Musomba kwa jukumu hilo jipya alilokabidhiliwa.

“Pongezi za dhati kwa Askofu Stephano Lameck Musomba kwa kuteuliwa na Papa Francisko kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Nakutakia kila la kheri. Mwenyezi Mungu akuongoze katika majukumu yako,” amesema Rais Samia kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi