Burudani
Bodi ya Ligi yaingilia kati sakata la Simba, yatoa kauli

Dar es Salaam. Sakata la Simba kugomea mchezo dhidi ya watani wao, Yanga, limechukua sura mpya baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutoa tamko kwamba mechi hiyo ipo palepale kama ilivyopangwa.
Simba ilitoa tamko usiku wa kuamkia leo ikisema haitaleta timu uwanjani kwenye mchezo huo kufuatia msafara wa kikosi chake kuzuiwa jana usiku kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao ndio utatumika kwenye mechi hiyo.
Simba ilizuiwa na kundi la watu wanaodhaniwa ni mashabiki wa Yanga maarufu kwa jina la makomandoo, huku pia ikimtaja meneja wa uwanja kudai hakuwa na taarifa kwamba Wekundu hao watakwenda kufanya mazoezi uwanjani hapo.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Steven Mnguto amesema licha ya Simba kudai haitaleta timu mchezo huo upo palepale huku akiwataka mashabiki waliokata tiketi kujipanga kwenda uwanjani.
“Matukio yote tumeyasikia na tunayafuatilia kuanzia hatua ambayo yalijiri, kuna ripoti za awali tumeshazipokea kwa wasimamizi mbalimbali na tunazifanyia kazi,” amesema Mnguto.
“Kwanza niwatoe wasiwasi mashabiki wa soka na wadau kwa ujumla. Mchezo upo palepale kama ambavyo kalenda yetu ya soka inavyosema, hakuna mabadiliko yoyote, mashabiki wajipange kuja kutazama mchezo.”
Mnguto ameongeza kuwa kufuatia taarifa hiyo ya Simba ameitisha kikao cha dharura cha kamati ya usimamizi wa ligi kitakachojadili tukio lililotokea jana usiku.
“Nimeitisha hiki kikao cha haraka kitafanyika asubuhi hii. Bahati mbaya sitaweza kushiriki, lakini nimemuagiza makamu wangu akisimamie tujadili matukio haya yaliyotokea jana na hii taarifa ya Simba,” amesema Mnguto.
“Tutatoa taarifa kamili mapema sana kwenda kwa wadau wote. Kwa hiyo tunaomba watu wawe na subira, lakini kama nilivyosema mchezo upo kama ambavyo umepangwa hakuna mabadiliko. Hayo mengine tutayatolea ufafanuzi zaidi mara baada ya kikao kukamilika.”
