Makala
Sababu wanawake kupenda kuwazawadia soksi, singlendi na ‘boxer’ wapenzi wao

Dar es Salaam. Je, umewahi kufikiria ni sababu zipi zinawasababishia baadhi ya wanawake kupendelea kuwanunulia wapenzi wao singlendi, soksi au nguo za ndani ‘boxer’ wanapotaka kuwapa zawadi?
Kwa mujibu wa wanawake mbalimbali waliozungumza na Mwananchi, wanadai unafuu wa gharama, urahisi wa upatikanaji pamoja na umuhimu wake kwa mwanaume ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma wakimbilie kuwanunulia wapenzi wao zawadi hizo.
Hata hivyo, jambo hilo limeonekana kuwachukiza baadhi ya wanaume na kuhoji nafasi zao kwa wapenzi wao.
kizungumza na Mwananchi, Nyasatu John, Mkazi wa Chamazi jijini Dar es Salaam, anasema wanawake wengi hupendelea kuwanunulia vitu hivyo kutokana na umuhimu wake katika maisha yao ya kila siku.
Nyasatu anasema sababu nyingine ni kutaka wapenzi wao kuonekana nadhifu.
“Soksi, singlendi na boxer ni mavazi yanayovaliwa kila siku, na mara nyingi wanaume husahau kununua au kubadili mavazi haya mara kwa mara, na ndiyo maana wapenzi wao huchukua jukumu hilo ili kuhakikisha wanakuwa nazo za kutosha,” anasema.
Naye, Mwanaisha Shabani, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema baadhi ya wanawake hupendelea kuwanunulia wapenzi au watu wao wa karibu aina hizo za zawadi kutokana na vitu hivyo kutozingatiwa na baadhi ya wanaume.
Mwanaisha anasema baadhi ya wanaume wanaponunua mahitaji yao muhimu, ikiwemo mavazi, ni mara chache hukumbuka kununua vitu hivyo.
“Kwa baadhi ya wanaume unakuta ana ‘boxer’ tatu pekee, singlendi tatu anarudia-rudia kila mara na wakati mwingine bila hata ya kuzifua. Kumnunulia vitu hivyo vinamfanya kuwa na machaguo mengi, hivyo kumfanya azidi kuongeza utanashati wake,” anasema.
Kwa upande wake, Penina Mwilongo, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, anasema baadhi ya wanawake hupendelelea kuwanunulia wapenzi wao zawadi hizo kutokana na unafuu wa gharama.
Penina anasema mahitaji mengi ya wanaume, ikiwemo nguo, viatu, kofia, huwa ni gharama, jambo linalowafanya wanawake kukimbilia kuwanunulia wapenzi au watu wao wa karibu zawadi hizo.
“Mfano kwa nguo za dukani za kiume mara nyingi huwa ni gharama, mfano suruali ya ‘jeans’ unaweza kununua kuanzia Sh30,000 na kuendelea, shati Sh15,000 hadi Sh35,000 na kuendelea, boxer ni Sh10,000 hadi 12,000. Hivyo tunafuata unafuu wa gharama,” anaeleza.
Walichokisema wanaume
Amiry Abdul, mkazi wa Kijitonyama, anasema aina hiyo ya zawadi imekuwa kama mazoea kwa wanawake wengi, jambo linalosababisha kupoteza mvuto.
“Kwenye siku yangu ya kuzaliwa atanunua singlendi, soksi na ‘boxer’, Valentine atarudia hizohizo, siku ya baba duniani kadhalika, hadi inapoteza mvuto wa zawadi,” anasema.
Kwa upande wake, Heri Hega anasema zawadi ni zawadi, unatakiwa kufurahia kile chochote ambacho mtu ameamua kukuzawadia kwa upendo.
“Pengine ndiyo uwezo wake unaishia hapo, huwezi kulazimisha. Cha muhimu ni kuthamini upendo ambao mtu ameamua kukuonyesha na kukumbuka kukununulia zawadi bila kujali ni ya thamani gani,” anaeleza.
Frank Baraka, mkazi wa Dodoma, anasema mpenzi wake amekuwa akimpa zaidi ambazo wakati mwingine zinamwacha na mshangao.
“Mimi bwana mwenzangu, utakuta ananiletea suti, viatu au nguo za michezo kwa sababu nacheza mpira. Yaani ananiletea vitu ambavyo napenda,” anasema Baraka.
Kitaalamu imekaaje
Mtaalam na mshauri wa masuala ya mahusiano, Eva Mrema, anasema kwa miaka ya nyuma zawadi hizo zilijizolea umaarufu kutokana na wanawake wengi walikuwa bado ni mama wa nyumbani.
Hivyo, vipato vyao walikuwa wanavipata kupitia fedha wanazoachiwa na waume zao, hivyo zawadi kama hizo ilikuwa ni nafuu kwao.
Anasema kwa sasa mambo yamebadilika, wanawake wengi wanajishughulisha na shughuli mbalimbali ambazo zinawaingizia kipato.
“Hata hivyo, bado zawadi za aina hizo zimeendelea kuwa vipaumbele kwa wanawake,” anasema.
Anaeleza hilo linachagizwa na mambo kadhaa, ikiwemo uoga wa baadhi ya wanawake kuwekeza zaidi kwa mwanaume na baadaye akamuacha.
Anasema baadhi ya wanawake wanakuwa na hofu kuwanunulia wapenzi wao zawadi za gharama kwa kuhofia pengine wanaweza kuachana.
“Pia, wanawake wana hulka ya kurudisha upendo kwa kiasi ambacho wamepatiwa,” anasema.
