Kitaifa
Hivi ndivyo Kariakoo ya saa 24 itakavyokuwa

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 10 eneo la kibiashara Karikaoo jijini hapa kuanza kufanya kazi saa 24, wafanyabiashara wameeleza namna walivyojiandaa ukiwamo ushiriki katika ulinzi, usalama wao na wa wateja.
Januari 30, 2025 akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa Dar es Salam, Albert Chalamila alisema uzinduzi rasmi wa kufanyika biashara hizo kwa saa 24 utakuwa Februari 22, 2025 na utaanzia ofisini kwake hadi Kariakoo kwa kuwa na matukio tofauti tofauti.
Alisema ufanyaji huo wa biashara, unalenga kuimarisha uchumi wa mkoa, kuongeza mapato ya Serikali na kutoa fursa za ajira.
“Tunahakikisha mkoa wetu wa Dar es Salaam unakuwa na mazingira bora ya kufanya biashara muda wote na tayari tunashirikiana na viongozi wa manispaa kuimarisha maeneo yanayofaa kwa biashara za saa 24,” alisema Chalamila.
Hivi karibuni, Mwananchi imefuatilia maandalizi ya utekelezaji wa agizo hilo na kuona tayari umeanza, ikiwamo ufungaji wa taa za barabarani, huku baadhi ya barabara za kuingia katika Soko Kuu la Karikaoo zikiwa na nafasi za watu kupita ukilinganisha na zamani kulikuwa na msongamano mkubwa.
Katika barabara hizo, wamachinga wameonekana kusogea hatua chache nyuma na kuruhusu vyombo vya usafiri kupita na waenda kwa miguu kupitia kiurahisi, ikiwamo mitaa ya Sikukuu na Uhuru na Tandamti kuelekea Msimbazi japo Mtaa wa Congo na ule wa Mchikichi hali bado ipo vilevile.
Wafanyabiashara waeleza utayari
Akizungumza na Mwananchi kuhusu maandalizi hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Mkoa wa Dar er Salaam, Namoto Yusuph amesema wameshaandaa walinzi kwa ajili ya kuwalindia maeneo na mali zao.
Amesema wamefanya hivyo kwa kuwa sehemu nyingi zenye msongamano wahalifu pia hutumia kama fursa kufanya vitendo vya kihalifu.
“Tumeingia mkataba na kampuni ya ulinzi (anaitaja jina) tangu Januari mwaka huu ambao wametupa walinzi 90 watakaolinda meza na mali zilizopo za wamachinga,” amesema Yusuph.
Amesema walifikia uamuzi huo sio tu kwa ajili ya kuweka ulinzi, bali kuwapunguzia mzigo wa gharama wamachinga waliokuwa wakiwalipa wabeba mizigo kupeleka stoo na kurudisha maeneo ya biashara.
“Katika kuifanya kazi hii ni gharama ndogo ya Sh1,000 tofauti na wakati ambao machinga alikuwa akitumia Sh3,000 hadi Sh6,000 kutegemea na ukubwa wa mzigo kubebwa kwenda na kurudi,” amesema Yusuph.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severin Mushi amesema wapo tayari kuanza biashara na wanachosubiria ni hiyo siku ya uzinduzi.
Mushi amesema pia wanashukuru baadhi ya changamoto walizowahi kuzianisha zimeanza kufanyiwa kazi ikiwamo kukatika kwa umeme mara kwa mara ambao awali ulikuwa ukikatika hadi mara sita kwa siku lakini sasa unakatika mara moja hadi mara mbili na wakati mwingine haukatiki kabisa.
“Tunashukuru kilio chetu cha kukatika umeme kimefanyiwa kazi, ni eneo ambalo tulikuwa na wasiwasi nalo kuhusu usalama wetu na Tanesco wamekuwa karibu na sisi hata inapotokea hitilafu,” amesema Mushi.
Kuhusu malalamiko ya wamachinga kuwazibia nafasi wenye maduka, amesema wameona jitahada zikifanyika, isipokuwa ameshauri ulinzi uwepo muda wote wa kuhakikisha hawarejei, kwa kuwa baadhi ya maeneo licha ya kuondolewa wameanza kurejea hasa Mtaa wa Congo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Said Chenja amesema wamejipanga vizuri katika mapinduzi hayo na wana mpango wa kuwa na sare zao.
Chenja amesema sare hizo zipo katika hatua za mwisho kutengenezwa na mpaka Machi zitakuwa zimeshafika nchini.
“Jumla ya sare 20,000 zitakuja katika awamu ya kwanza na eneo la kwanza tunalolifikiria ni la Kariakoo, katika hizo tutawapa sare 6,000.
“Tunataka mtu akibebewa mzigo wake kama unaenda stendi ya Magufuli, stendi ya Magari ya Kusini Temeke, stesheni ufike salama au kama ni abiria mwenyewe naye iwe hivyo, hivyo kuwa na sare maalumu itasaidia yote haya, kila wilaya itakuwa na rangi yake na hadi kufika Agosti tunataka tuwe tumeshaleta sare 100,000,” amesema Chenja.
Amesema wanaendelea kuwasajili madereva wote na kuwaweka katika kanzi data yao na hadi sasa wameshafika zaidi ya bodaboda 250,000 huku Kariakoo pekee ikiwa na bodaboda 6,200.
Mama lishe waliozungumza na Mwananchi, wamesema hawakushirikishwa katika suala hilo.
“Tunasikia tu kuwa Kariakoo inaenda kufanya kazi saa 24, tunaomba tupatiwe maeneo maalumu ya kufanyiwa shughuli zetu kwa kuwa sasa hivi watu wamekuwa wakitegemea kukaa kwenye baraza za maduka ya watu usiku.
“Sasa baraza hizo za maduka tulizokuwa tunazitegemea wenyewe watakuwepo, hivyo badala ya kuwa fursa kwetu, itakuwa kero, hivyo kutengwa kwa eneo maalumu kwa ajili ya hili ni muhimu kwetu,”amesema Zena Ismail anayefanya shughuli zake eneo la Kariakoo.
Hata hivyo, Jane Nyanda anayefanya kazi eneo hilo kwa miaka 10 sasa, amepongeza hatua hiyo akisema utaratibu huo utaongeza biashara yao.
Maandalizi yalipofikia
Akizungumzia kuhusu maandalizi yalipofikia hadi sasa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema yapo vizuri ikiwa pamoja uwekaji wa taa za barabarani.
Mpogolo amesema kazi ya kufunga kamera itafanywa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) ambao wameshinda zabuni hiyo.
Kuhusu shughuli ya kufunga taa, amesema inafanywa na taasisi mbalimbali wakiwamo Halmashauri ya Ilala, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura).
“Ukiacha taasisi hizo za Serikali, pia wanaomiliki majengo eneo hilo tumewashirikisha katika hili, kuwa ni vema wakafunga taa katika nyumba zao na hata ikiwezekana kamera ili suala la ulinzi tulifanye kwa kushirikiana,” amesema Mpogolo.
Akizungumzia biashara ya mama lishe eneo la Kariakoo, Mpogolo amesema hakuna eneo maalumu kwa ajili ya mama na baba lishe kwa kuwa hata kwa sasa watu Kariakoo wanakula na hakuna eneo maalumu kwa ajili ya watu hao.
“Sisi tunachokifanya ni kuiweka Kariakoo usiku iwe kama mchana, hivyo kila anayeiona fursa kama alivyokuwa anaiona kwa mchana aitumie, maana kama ni watu kula chakula eneo hilo wanakula na wala hakuna maeneo rasmi ya baba na mama lishe,” amesema Mpogolo.
Kuhusu ulinzi, amesema umeimarishwa kwa saa 24.
“Nadhani mmekuwa mashahidi Kariakoo baadhi ya maeneo biashara zinafanyika hadi usiku ikiwamo za vyakula, hii ni kwa sababu hali ya usalama ni shwari kwa sasa,” amesema.
Wanaolala vibarazani matumbo joto
Mmoja wa vijana wanaolala katika baraza za maduka yaliyoyopo maeneo hayo, Frank John amesema kwao ni maumivu kwa kuwa sasa itabidi akatafute eneo jingine la kulala, pembezoni mwa mji.
“Baraza kiukweli wengine tusiokuwa na nyumba zilikuwa zikitusaidia usiku, sasa najiona kwenda kutafuta maeneo mengine ikiwamo kwenye madaraja au vituo vya daladala,”amesema John.
Akizungumzia hatua hiyo, Mchambuzi wa masuala ya uchumi na Mhadhiri wa Chuo cha Biashara(CBE), Profesa Dickson Pastory, amesema kuelekea kuanza biashara kwa saa 24, ipo haja ya watu kuwa waaminifu katika uuzaji wa bidhaa zao.
“Hapa namaanisha kwa kuwa Kariakoo ina kila kitu unachohitaji, isije ikawa bidhaa zinazouzwa mchana ni tofauti na zinazouzwa usiku, hivyo suala la uaminifu wakati wote wa biashara ni muhimu,”amesema.
Pia, amewataka Watanzania kujua kwamba, kuchangamka kwa biashara kwa nyakati hizo itachukua muda na kubainisha hata masoko katika majiji ya Tokyo Japan, New York Marekana na Hong Kong na China, iliwachukua muda mrefu mpaka sasa yamezoeleka.
