Makala
Uhalisia, katikati ya sheria ya utoaji mimba

Dar es Salaam. Wakati sheria ya Tanzania ikitaja utoaji mimba ni kosa kisheria, imegundulika baadhi ya wanawake na wasichana nchini wamekuwa wakifika katika vituo vya afya kupata huduma baada ya kuharibika kwa mimba.
Hata hivyo, baadhi yao, hufika kuhitaji usaidizi baada ya jaribio la kutoa mimba kugonga mwamba.
Hali hiyo ni kinyume na makatazo ya sheria yaliyofafanuliwa kwenye vifungu namba 150, 152 na 230 vya kanuni ya adhabu sura ya 16 (Marekebisho ya 2022).
Ukosekanaji wa huduma salama za utoaji mimba, husababishwa na mazuio ya kisheria ambayo yamefafanuliwa kwenye vifungu hivyo.
“Nilitumia tembe (jina linahifadhiwa) ambazo niliambiwa na mtu kuwa zingenisaidia kutoa mimba. Licha ya kutumia kwa usahihi saa kadhaa nilisikia tumbo limenyonga na ghafla damu zilianza kutoka mfululizo, kadri muda unavyoenda ziliongezeka na baadaye yalianza kutoka magonge ya damu,” amesimulia Rehema (22).
Mkazi huyo wa jiji la Dar es Salaam amesema hali ilivyozidi kuwa mbaya aliishiwa nguvu na kuanguka chini.
“Nilikimbizwa zahanati. Huko walinifanyia huduma ya kunisafisha bila gharama yoyote, kisha nikaruhusiwa kurudi nyumbani.”
Rehema ni miongoni mwa wanawake na wasichana wengi nchini, ambao hufika hospitali kupata huduma baada ya kuharibika kwa mimba, wakiwa tayari walijaribu kuichomoa.
Kwa mujibu wa daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Isaya Mhando kuna aina mbili ya kuharibika kwa mimba.
“Mimba inayotoka yenyewe kutokana na sababu ya matatizo ya mama chini ya wiki 12 asilimia 50 hutokana na matatizo ya vinasaba na sababu nyingine ni magonjwa kama rubella, kuganda kwa damu na mengineyo.
“Za kuchokonolewa tunaita ‘criminal abortion’ inaweza kutolewa katika mazingira salama na yasiyo salama. Kutokana na kuwepo kwa ile sheria wengi hufanya mambo kwa kujificha wanakutana na watu wasio sahihi wanapata changamoto inayokuja na maambukizi,” amesema Dk Mhando.
Amesema kwa uzoefu wa madaktari mimba nyingi zinazochokonolewa. “Mgonjwa hufika anavuja damu, kichwa kinauma, homa kali hali ambazo tayari huwa amepata maambukizi.
“Utamuuliza kupata historia, unapofuata miongozo unagundua nini alifanya, wengi ukimbana anakwambia ukweli, anakuwa na hali ngumu na ukichelewa kumsaidia inaathiri mpaka figo. Mwongozo lazima umsaidie kuokoa maisha,” amesema Dk Mhando.
Takwimu za Wizara ya Afya, zinaonesha wanawake 181,071 walipata huduma ya kusafishwa na wengine 32,512 walilazwa baada ya mimba kuharibika mwaka 2024.
Hata hivyo, Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS mwaka 2023 ilionesha Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa asilimia 23 ya mimba huharibika.
Kufuatia hilo, Mwanasheria na Ofisa Miradi kutoka (LEAT) Clay Mwaifani, amesema sheria na sera ya utoaji mimba nchini ina utata na inachanganya.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Februari 11, 2024 katika mahojiano maalumu amesema ni haki kwa mwanamke yeyote au msichana ambaye atafika kituo cha afya akiwa ameharibikiwa mimba kupewa huduma ya kusafishwa.
“Sheria yetu licha ya kwamba inazuia utoaji mimba, huduma baada ya kuharibika kwa mimba kwa mtu yeyote ambaye labda imetoka yenyewe, ametolewa kitaalamu, amefanya itoke ni kosa la jinai; wote hawa mimba ikiwa imetoka kufika hospitali kupatiwa huduma ya kusafishwa ni haki yake,” amesema Wakili Mwaifani.
Amesema hiyo ndiyo sababu Wizara ya Afya inapata takwimu, kwani licha ya utoaji wa mimba kuwa suala la kificho, kusafishwa si suala la kificho.
“Utoaji mimba unaweza kufanyika famasi, gereji, nyumbani, uchochoroni lakini usafishwaji anaenda hospitali. Ni wanawake wachache ambao mimba huharibika kutokana na mazingira mbalimbali ambayo hawakuyatarajia,” amesema.
Wakili Mwaifani amesema kitendo cha Serikali kuwa na takwimu kubwa za wanaosafishwa, ina maana utoaji mimba unatokea.
“Kwa hiyo hatuwezi kujifanya hatuoni, hiyo ndiyo hoja ya msingi ni sawa na mzazi anayeogopa kuongea na binti yake masuala ya afya ya uzazi, matokeo yake ni mimba isiyotarajiwa au magonjwa. Tutoke kwenye kivuli cha mwiko kwamba haya mambo hayajadiliwi, ama sivyo tutaendelea kukumbana na vifo vitokanavyo na masuala ya uzazi na ugumba,” amesema.
Amesema sheria ya makosa ya jinai huidhinisha utoaji mimba ili kuokoa maisha ya mwanamke, lakini haijaweka wazi kama utaratibu huu utalinda afya ya mwili na akili ya mwanamke.
Hofu ya kushtakiwa, ambayo ipo kwa wanawake na watoa huduma ya afya pia, husababisha wanawake watoe mimba kwa siri kwa njia ambazo mara nyingi huwa si salama.
“Ukiongelea hili, kuna watu wanahisi unapigania ajenda ya wazungu ni mara nyingi hoja zinaibuliwa na wengi wanaona si kipaumbele cha wananchi, kwahiyo unailetaje katika lugha rahisi? Ukirejea taarifa muhimu kama sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, 2012 na 2022 utagundua Tanzania ni Taifa ambalo kila baada ya miaka 20 idadi yake inaongezeka mara mbili,” amesema.
Wakili Mwaifani amesema suala la vifo vitokanavyo na uzazi, ukihusianisha na makosa ya jinai na ya kimaadili, jambo hilo lieleweke na lijadiliwe miongoni mwa jamii.
Amesema wakati mijadala hiyo inaendelea ni muhimu watu waangalie, sheria inapotungwa inakwenda kutengeneza haki hivyo lazima kutakuwa na maswali.
“Mtu asije kuelewa kwamba hii sheria imetungwa kila mtu aliyebakwa akatoe mimba au ya maharimu, jibu ni hapana, haitakuwa amri kwa atakayetaka kutunza mimba ataweza kuitunza lakini wale ambao wanaona hawawezi sababu walibakwa wanaweza kuendeleza haifanyiki kuwa wajibu,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo cha Sayansi na Afya Shirikishi (Muhas), Dk Ali Said amesema utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionyesha mimba takribani milioni 2.9 hutungwa kila mwaka.
‘“Miongoni mwa hizo, utafiti ulionyesha mimba milioni 1.3 hazikupangwa, mimba 430,000 hutoka au kutolewa,” amesema Dk Said.
Ingawaje mimba zinazoharibiwa ambazo hurekodiwa ni 430,000 kwa mwaka, wataalamu hao wanasema idadi ni kubwa zaidi kwa sababu wanaofika vituoni kuhitaji msaada wa kitabibu ni wale waliopata madhara ya papo kwa hapo.
Bunge lagusia mabadiliko ya sheria
Januari 31, 2025 bungeni jijini Dodoma, mbunge wa viti maalumu Dodoma Mjini, Fatma Tawfiq aliuliza swali kuhusu wanawake na wasichana wangapi wameathirika na utoaji mimba usio salama nchini.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema kwa mwaka 2024 idadi ya wanawake na wasichana waliopata changamoto za kuharibikiwa na mimba na kupata huduma katika vituo vya afya na kuruhusiwa kurudi nyumbani walikuwa 181,071.
Dk Mollel alitaja wanawake na wasichana 32,512 ambao walipatiwa huduma wakiwa wamelazwa wodini kwa mwaka 2024.
Lakini katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024 wanawake 92 walipoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali zinasababishwa na kuharibika kwa mimba.
Majibu hayo yaliongeza swali la nyongeza kwa mbunge huyo akitaka kujua, nini mkakati wa Serikali wa kutoa elimu ili kupunguza idadi ya wanawake wanaotoa mimba au mimba kuharibika.
Aliongeza kuwa, baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakibakwa, hupata mimba ambazo hazikutarajiwa akitaka kujua nini hatima ya hilo.
Naibu Waziri alisema:“Mkakati wa Serikali ni endelevu, tumekuwa tukitoa elimu kupitia vyanzo mbalimbali na pia kupeleka elimu kupitia wananchi. Kama mjuavyo mwaka huu, Rais amejenga vituo zaidi ya 480 kupeleka huduma karibu na wananchi.”
Alisema kinamama kubakwa na kupata mimba ni suala linalohitaji elimu zaidi kisaikolojia baada ya hilo kutokea.
Majibu hayo yalimuibua Mbunge wa Nkasi kupitia Chadema, Aida Kenan akisema: “Wanawake wanaopoteza maisha ni Watanzania na ili tumalize tatizo, ni lazima tulijue tatizo, ningependa kufahamu mmefanya tathmini na kugundua nini kinasababisha utoaji mimba usio salama?”
Dk Mollel alijibu:“Suala hili ni nyeti, linaleta gharama kubwa anatibiwa yeyote anayehitaji huduma ili kuokoa maisha, unaona ni wananchi zaidi 181,000 ni mimba ambazo hazikupangiliwa, tuna kazi kubwa kulinda uadilifu na kutoa elimu kuanzia ngazi za chini.”
Hata hivyo, Mbunge Felista Njau alihoji:“Ni lini Serikali itakuja na sheria ya kumlinda mwanamke aliyepata mimba isiyotarajiwa, kwa kubakwa na ndugu/maharimu?”
Dk Mollel alijibu: “Sheria za kumlinda mwanamke zipo ni suala la jamii kuendelea kuwajibishana, uzalendo na mambo mengine.”
Majibu hayo yalimuibua Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akisema kama wawakilishi wa wananchi inabidi wapeleke ombi upande wa Serikali ili wataalamu watoe mafunzo kwa wabunge, kwa kuwa kutoa mimba bado ni kosa la jinai, pamoja na kwamba kuna hizo changamoto zinazojitokeza kwa wale wanaotoa mimba na zinazotoka.
“Sisi ndiyo tunaotunga sheria, lakini ni vizuri tukawa na uelewa mpana juu ya eneo hili kabla, tushauri labda sheria tubadilishe kwenye maeneo gani.”
