Connect with us

Kitaifa

USAID kupunguza wafanyakazi kutoka 10,000 hadi 294 duniani

Mwanza. Serikali ya Marekani imepanga kupunguza idadi ya wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kutoka zaidi ya 10,000 hadi 294, hatua inayotarajiwa kuathiri shughuli zake duniani kote.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, ni wafanyakazi 294 pekee watakaobaki, wakiwemo 12 katika Idara ya Afrika na wanane katika idara ya Asia.

Hatua hii ni sehemu ya mpango wa mageuzi ya Serikali unaoongozwa na mfanyabiashara Elon Musk, mshirika wa karibu wa Rais Donald Trump. Mpango huo unalenga kuunganisha USAID na Wizara ya Mambo ya Nje chini ya uongozi wa Waziri Marco Rubio, ambaye kwa sasa ni kaimu msimamizi wa USAID.

“Huu uamuzi unakera,” amesema Brian Atwood, aliyewahi kuwa Mkuu wa USAID kwa miaka zaidi ya sita huku akitahadharisha kuwa kitendo cha kuwatemesha kazi watumishi kitahatarisha uhai wa shirika hilo ambao wamekuwa wakipambana usiku na mchana kunusuru maisha ya binadamu.

“Watu wengi watakufa,” amesema Atwood, ambaye sasa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kujitolea Chuo Kikuu cha Brown nchini Marekani.

Idara ya ndani ya Marekani haijatoa kauli yoyote kuhusiana na madai ya kupunguza watumishi hao.

Hata hivyo, Trump na Musk, wameendeleza machungu kwa watumishi waliokuwa wakifanya kazi katika Taasisi zinazofadhiriwa na USAID baada ya kuwapatia likizo ya lazima, mamia ya wafanyakazi wa muda wameachishwa kazi huku programimu lukuki zikisitishwa jambo linalotajwa kuhatarisha ustawi wa binadamu duniani.

Utawala wa Rais huyo ulitangaza Jumanne kuwa utawapatia likizo ya lazima wafanyakazi wote wa USAID duniani huku ukisitisha shughuli za shirika hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kuangalia programu maalumu ambayo hazipaswi kujumuishwa katika mpango huo, utaoathirisha Shirika hilo.

USAID linaendesha programu mbalimbali zikiwemo za kukabiliana na magonjwa, ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kupambana na changamoto ya umaskini.

Kutokana mpango huo wa Trump na Serikali yake, tayari taasisi zinazofadhiriwa na shirika hilo zimeanza kukumbana na changamoto katika uendeshaji wa shughuli zake baada ya Idara hiyo kusitisha ufadhiri na misaada.

Uamuzi huo siyo tu unatajwa kuwa utaathiri hali ya ustawi wa jamii na kukabiliana na magonjwa, pia utaathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja hususan ni wafanyakazi wanaotekeleza majukumu yao chini ya USAID duniani na familia zao.

Lengo la Trump ni kuiunganisha USAID na Wizara ya Mambo ya Nje inayoongozwa na Rubio, ambaye ametangazwa na Trump kuwa Kaimu Msimamizi Mkuu wa Shirika hilo.

Hata hivyo, bado haijaeleweka jinsi gani atatimiza azma hiyo kwani ili kuifungamanisha USAID na Wizara hiyo kunahitajika kupewa baraka kwa kupigiwa kura ya ‘Ndiyo’ na Bunge la Congress kwa sababu Shirika hilo lilianzidhwa kusheria hata kuvunjwa kwake kutazingatia sheria.

USAID ina watumishi zaidi ya 10,000 duniani, 2/3 (zaidi ya watumishi 7,500) wanafanya kazi nje ya Marekani kwa mujibu wa CRS. Shirika hilo lilitumia Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 40 kwa mwaka 2023, pekee.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Shirika hilo pia viliielez Reuters kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi wameshaanza kupewa barua ya kuachishwa kazi.

Hata hivyo, Tovuti ya USAID ilichapisha taarifa Ijumaa Februari 7, mwaka huu inayosomeka: “Waajiriwa wote USAID wanatakiwa kwenda likizo, isipokuwa wale tu ambao wanasimamia shughuli maalum za kiutawala ama masuala ya dharura katika mipango maalum.”

Tovuti hiyo pia ilisema kuwa wafanyakazi maalum wanaopaswa kuendelea kuwepo Ofisini watafahamishwa ifikapo Alhamisi Saa 5:00 usiku. USAID ilitoa misaada kwa mataifa zaidi ya 130 duniani mwaka 2023, hususan ni yanayokumbana na machafuko.

Mataifa makuu yaliyonufaika na USAID ni pamoja na Ukraine, ikifuatiwa na Ethiopia, Jordan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Somalia, Yemen na Afghanistan.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi